Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na pia nimshukuru Mwenyezi Mungu. Kwanza nianze na kumpongeza sana Dkt. Mpango kwa kuleta Mpango mzuri. Nimpongeze pia Dkt. Kijaji, nipongeze Makatibu na watendaji wote wa Wizara hii ambao wametuletea Mpango wetu na kutuwasilishia hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kweli ameweza kutekeleza mambo mengi sana ikiwepo miradi ya ujenzi wa reli ya kati, mradi wa kufufua umeme, kuimarisha ndege, ujenzi wa meli, ujenzi wa jengo la abiria na miradi mingi tu ambayo kwa kweli hii inaonesha ni jinsi gani Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotekelezeka. Sioni ajabu kuona kwamba watu wengine wameweza kuacha kuchukua fomu au wamejitoa katika chaguzi kwa sababu, miradi mingi sana imeonesha jinsi gani ambavyo tumekuwa makini Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee pia kutoa pongezi kwa mpango huu mzuri ambao umewasilishwa. Na hii ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha, kuweka nidhamu kwa watumishi, kwa kweli haya ni mambo ambayo yamesababisha Serikali yetu kuweza kuendelea kufanya vizuri na kuendeleza miradi mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze sasa kuchangia mpango wangu, naomba nijikite katika urahisi wa kufanya biashara, easy of doing busuness. Niipongeze Serikali kwa kuanza kuweka usajili katika mitandao, kwa kweli hii ni kazi nzuri na inafanywa kwa urahisi, lakini wako wafanyabisahara wengi wadogowadogo ambao sasa hawawezi kutumia mtandao ambao ni akinamama, vijana; sasa nione tu Serikali inaweka mpango gani kuhakikisha wanawafikia hawa wafanyabiashara wadogowadogo ili na wao wasajili biashara zao. Maana pengine kumekuwa na urasimu mkubwa sana wa kusajili hizi biashara kama hawana mtandao, sasa Serikali imejipangaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wekeni mpango mzuri kuhakikisha kwamba, tunapata wafanyabiashara wengi ambao wanasajili biashara ili tuweze kupata mapato na tuongeze pato katika huu mpango ambao mmetuletea. Na ikiwezekana kuwepo na stop centre ili watu hawa wasiwe wanasumbuliwa pengine wanaenda kwa afisa biashara, anaenda TRA, BRELA, OSHA, nini, sasa tuweke sehemu moja then baadaye Serikali iweze kutengeneza mkakati wa kuhakikisha wanagawana hayo mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee na mpango wetu. Pia naomba ujikite kuona umuhimu wa kutenga pesa ya utafiti kwa sababu, katika miradi mingi sana tumeona yaani tumetembelea kwenye vituo vingi vya utafiti na tuna watafiti wazuri sana katika sekta nyingi hazifanyi vizuri kwa sababu bado hatujaweka mkakati kuhakikisha tunatumia zile tafiti au watafiti wetu, ili sekta zetu zifanye vizuri. Sasa nilikuwa naomba Serikali iangalie umuhimu wa kutenga lile pato ile asilimia moja, ili ziende kenye utafiti kwa sababu tumeona nchi nyingi zilizoendelea na zinafanya vizuri katika miradi yake wameweka kipaumbele katika tafiti. Sasa nina imani tukiweka tafiti zetu bado tutafanya vizuri sana na tutakusanya mapato mengi katika sekta zote katika Wizara zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nilikuwa naomba mpango wetu pia ujikite katika kuwekeza zaidi katika vyuo vyetu hivi vya VETA. Tukiwekeza katika vyuo vya VETA tutapata wataalam wa kuweza kuendesha viwanda vyetu vidogovidogo, tutapata mafundi mchundo na tuweze kuwawezesha vijana kuanzisha viwanda vidogovidogo na akinamama kwa sababu, tukiwa na viwanda vidogovidogo tukichukulia katika nchi kwa mfano India, China, unaona viwanda vidogovidogo ni vingi sana kwa hiyo, tukiwa na viwanda vidogovidogo tutapata uchumi mkubwa. Kwa hiyo, kama tukisaidia hawa vijana wakapata ujuzi na kuanzisha hivi viwanda vidogovidogo basi tutasaidia Serikali yetu kuwa na mpango mzuri wa kupata pesa na kukusanya pesa ili sasa tuelekee kwenye huo uchumi wa viwanda ambao ndio tumejikitanao kwamba, sasa hivi tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda vidogovidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile nilikuwa naomba kuna pesa huwa inakatwa SDL asilimia nne kutoka kwenye viwanda. Ni kwa nini sasa hii pesa angalo kidogo isipelekwe SIDO, ili SIDO waweze kuwakopesha vijana wetu waweze kufungua biashara wakipata yale mafunzo; hii nilikuwa natoa tu kama wazo langu kwamba, kwa Serikali ile SDL ya asilimia nne kutoka katika viwanda basi ipelekwe pia SIDO iweze kuwasaidia wanaoanzisha viwanda vidogovidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa naomba mpango wetu ujikite katika ujenzi wa barabara za kiuchumi zilizopo katika mikoa yetu. Ikiwezekana zijengwe kwa kiwango cha lami ili ziweze kupitika muda wote kwa sababu nikichukulia mfano tu katika Mkoa wangu wa Iringa unakuta barabara nyingi sana za kiuchumi hazipitiki kwa muda wote. Wakati wa mvua kunakuwa barabara hazipitiki kwa hiyo, unaona kwamba, kwa mfano labda ukienda kule Mufindi malori yanakwama hata wiki nzima, Kilolo malori yanakwama, lakini pia tunao uchumi mwingine kwa mfano tukiimarisha uchumi katika Mbuga yetu ile ya Ruaha National Park nafikiri tunaweza tukapata ongezeko kubwa la watalii na tukaongeza pato la Taifa na pato la mkoa pia. Lakini ikiwepo na kuongezea TARURA pesa kwa sababu TARURA ndio sasa hivi wana kazi kubwa kuhakikisha kwamba, barabara za vijijini zinapitika muda wote na zinajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee katika mpango wetu. Katika miradi ya kimkakati nilikuwa naomba kwamba, miradi hii ya kimkakati ya kuongeza tija na mapato sasa tijikite kuwasaidia wakulima, wafugaji, wavuvi kwasababu, hii miradi ya kimkakati katika kila halmashauri ipo, sasa iangaliwe. Kama kuna halmashauri ambayo ina wakulima wengi basi ile miradi ya kimkakati ijikite katika kuwasaidia wakulima. Kama kuna wavuvi halmashauri basi ijikite kuhakikisha kwamba, wavuvi au wafugaji wanasaidiwa ili kusaidia pato katika halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoa tu mfano kwenye sekta ya uvuvi unaona mapato yamepanda kutoka bilioni 21 mpaka bilioni 72 kwa hiyo, hapo kuna ongezeko kama la bilioni 51 na mapato ya samaki nje ya nchi bilioni 379 mpaka bilioni 691 na bado sasa hapa hawajaweza kuwezeshwa vizuri. Niko katika Kamati ya Kilimo, tunatembelea wavuvi wana changamoto nyingi sana, kama tukijikita kuwasaidia hawa wavuvi wakafanya vizuri sana tutatengeneza mapto mengi ambayo yatasaidia nchi hii na tutaweza kuweza kusaidia mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo niseme kwanza vilevile niipongeze Serikali kwa kuweza kutoa pesa katika halmashauri zetu kwa ajili ya kuwakopesha akinamama, vijana na watu wenye ulemavu, lakini niombe hizi pesa wanavyopewa bila kupata elimu bado hatujawasaidia. Kwa sababu, hizi pesa unapowakopesha unakopesha zirudi na wengine wakope, lakini tuna imani wafanye vizuri zaidi wawe na biashara kubwa ambapo katika biashara zao tutasaidia sasa kuleta pato, walipe kodi kwa wingi ili tuweze kusaidia nchi yetu kuongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo ni kuwashukuru sana. Namuomba Mwenyezi Mungu aendelee kusaidia Tanzania na amsaidie Mheshimiwa Dkt. Magufuli, ili mwakani wanaosusa wasuse tuendelee kufanya vizuri zaidi, ahsante sana. (Makofi)