Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Joseph Osmund Mbilinyi

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbeya Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuchangia mpango huu. Lazima tukubalien kwamba hakuna mpango wa maendeleo bila Utawala Bora na Demokrasia na wakati naendelea kuchangia naomba tu ikumbukwe kwamba, nadhani wote tunakumbuka kwamba mwaka jana nilifungwa Gerezani kwa takribani miezi mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulitaarifu Bunge lako kwamba Mahakama Kuu ilitengua hukumu ile na ilisema kwamba mashitaka yalikuwa batili, mwenendo wa kesi ulikuwa batili na hukumu ilikuwa batili na hivyo kuthibitisha kwamba nilikuwa nimefungwa kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii kukipongeza sana Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Mwenyekiti wake, Kamati kuu yake pamoja na Viongozi wote kwa uamuzi wa busara waliofikia jana kujitoa kwenye uchaguzi ambao badala ya kuwa uchaguzi uligeuka kuwa uchafuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mbeya tuna Mitaa 181 hawa jamaa wametuengua wote wamebakiza wagombea 11 tu, Mitaa 181 halafu unasema eti wakakate rufaa na wapo wanajaribu kukata rufaa unakwenda unakuta Ofisi zimefungwa. Angalia sasa vipingamizi wanavyowawekea au sababu za kuwaengua; ukijaza na pen nyeusi wanasema ulitakiwa ujaze na blue, ukijaza na pen ya blue wanasema ulitakiwa ujaze na pen nyeusi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya kazi, mtu akiandika mkulima wanasema ulitakiwa uandike kilimo, akiandika kilimo wanasema ulitakiwa uandike mkulima sasa you guys are joke! You are a joke yaani mnafanya vitu vya ajabu kabisa na nawahakikishia mnachokitafuta mtakipata. Leteni Muswada Bungeni tunawaambia kabisa Serikali kwa sababu Bunge hili sijawahi kuona Mbunge ameleta Muswada halafu u-proceed. Serikali leteni Muswada Bungeni, Mheshimiwa Kangi wewe ndiyo kimbelembele wa kuleta utemi sijui uko wapi, walete Muswada mfute vyama vingi tuwe chama kimoja, kwani kuna shida gani? kwasababu ndiyo kitu mnachokitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika hili nimeona Wabunge wengi wa CCM waliomakini hawajafurahia, tunaongea nao nje hapo. Yaani unaona kabisa hata psychologically, facial expressions, body language unaona na kwa kauli zao unaona kabisa Wabunge wengi waliomakini kwa upande wa Chama cha Mapinduzi hawajafurahia ukiachia wale kama jamaa yangu Mheshimiwa Waitara ambaye anatetea mkate. Hata ningekuwa mimi labda kwa sababu si kapinduka halafu kapewa mkate lazima alinde mkate vinginevyo anakatwa na Makonda kaanza kumuingilia kule Ukonga kwa hiyo, lazima dish liyumbe kidogo, ayumbeyumbe ajaribu kutetea mkate. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini unawawezaje watu…

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …unawezaje kuacha…

MWENYEKITI: Mheshimiwa hebu taarifa.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpe taarifa Mheshimiwa Sugu Ndugu yangu na taarifa ya kwanza ni kwamba Sugu ubunge wake ana jasho langu nimemtengeneza mwenyewe…

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Weee mavi yako! Pumbavu wee! [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): ….nimefanyakazi kabla hujawa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, unasikia maneno hayo naamini kwamba utachukua hatua lakini nimpe taarifa kwamba uchaguzi huu una Kanuni na viongozi wa CHADEMA walipewa taarifa mapema, CCM walijipanga, wao hawakujipanga kuandaa watu wao kwa hiyo kutueleza habari iliyojazwa, amejaza mtu mwingine Sugu anazungumza humu ndani shule inamsumbua pia kwasababu aliyejaza form ndiyo anatakiwa a-clarify hicho ambacho anakisema humo ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpe taarifa kwamba Mheshimiwa Sugu kwamba sisi tunaendelea na mchakato na Kanuni zipo…

MWENYEKITI: Taarifa moja tu.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): …na utaratibu wa nchi hii ni kufuata Kanuni zilizopo.

MWENYEKITI: Ahsante.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Kwa hiyo, maneno mengine yote yale hayatafuta utaratibu wa Kanuni na Sheria zilizopo.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa kabla sijakuhoji kuhusiana na taarifa hiyo, Mheshimiwa Sugu nakuheshimu sana, nakuomba ufute kauli ya neno uliyotumia, naomba tu ulifute naamini ulimi umeteleza tu.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua humu ndani sisi tuna-discuss issue serious za hii nchi…

MWENYEKITI: Naelewa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …halafu hawa watu…

MWENYEKITI: Hapana.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …wanaleta mambo ya kulinda mkate, nafuta kwa heshima ya Kiti…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …lakini vinginevyo hawa watu wana nanihii sana…

MWENYEKITI: Ahsante

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …wanakera, we are very serious humu ndani…

MWENYEKITI: Unasemaje kuhusu na taarifa yake?

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …mtu anakaa tu Ubunge, Ubunge, hivi Sugu asipokuwa Mbunge wa Mbeya ndiyo hii Nchi itananihii…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sugu.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …itakamilisha mambo yao yote?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbilinyi unasema kuhusiana na taarifa unaikubali, unaikataa?

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Siwezi kupokea taarifa hiyo haina maana kabisa.

MWENYEKITI: Haya endelea kuchangia sasa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiangalie tulipoanguka…

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …tusiangalie tulipo…

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri hebu kaa tu, kaa tu, Mheshimiwa Waziri hebu kaa tu.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natumaini dakika zangu zinatunzwa, natumaini dakika zangu zinatunzwa.

Hebu tuwe wakweli, Attorney General yupo hapa, Waziri wa Utawala Bora hayuko lakini Naibu Waziri wa Utawala Bora yuko pale.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Changia tu hoja Mheshimiwa.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Changia tu hoja.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Taarifa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Nalihutubia Bunge linafanya fujo, kwa hiyo kwanza atolewe kwanza aliyefanya fujo yule…

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …kama tunavyotolewaga sisi.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mollel hebu kaa.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa kaa chini usibishane na mimi. Changoa hoja yako Mheshimiwa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Kama Messi, everybody anataka, utafikiri Messi niko uwanjani. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu turudi kuwa serious kidogo kwenye mambo ya nchi tusiangalie tulipoanguka, tuangalie tulipojikwaa. Yanayotokea haya kwa heshima zote, yanayotokea haya kwenye uchaguzi huu ni matokeo ya kauli ya Rais kwamba Mtendaji atakayemtangaza mpinzani wakati amempa gari, amempa mshahara, amempa sijui nyumba, sijui amempa nini atamfuta kazi, ndiyo matokeo haya. Unajua kauli ya Rais ni agizo. Kwa hiyo, ili twende sawa sawa… [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sugu hayo maelekezo ya Rais unayotaka kuiaminisha Kamati unaweza ukanipatia mimi sasa hivi ukaniletea hapa?

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Of course, najua utaratibu siwezi kuyaleta sasa hivi lakini ukinipa muda nitayaleta yapo.

MWENYEKITI: Kwa hiyo una-insist kwamba unayo?

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Yapo, naweza kuyaleta.

MWENYEKITI: Sasa Mheshimiwa mimi nakushi usiende kwenye territory hiyo, changia umalize mchango wako.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: I hope dakika zangu zinatunzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu kimoja, humu ndani kwa trend, utaratibu ulivyo, utamaduni, mazoea wanaorudi humu ni asilimia 30 tu, asilimia 70 tunabaki nje na huko nje hali ni mbaya kuliko mnavyoweza kufikiria. Kwa hiyo, mnayo nafasi ya kurekebisha wakati mkiwa humu ndani kuinyoosha Serikali. Msipoirekebisha 70 percent/80 percent mtabaki nje au niseme tutabaki nje tutakuwa hatuna tena pa kusemea kwa sababu ukisema nje unakamatwa unafungwa, angalau humu Bungeni tunayo nafasi ya kusema, hatutaki kusema sasa hivi. Kazi yetu sisi iwe kushauri siyo kusifia bila sababu. Unamsifia mtu kwa kitu ambacho hajafanya mpaka mwenyewe anashangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais amekuja kule Mbeya wanamsifia kwa jengo la radiolojia ambalo nimepambania mimi Mbunge kwa Katibu Mkuu wa Wizara.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …ili Bunge litenge fedha na Bunge likatenga fedha wanakuja wanamshukuru mtu mwingine badala…bajeti zinapitishwa humu ndani ya Bunge…

MWENYEKITI: Mheshimiwa...

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …kodi za wananchi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sugu.

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: …hizi fedha za nchi hii zinazonunua ndege, zinazofanya nini…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sugu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukisoma Katiba yako na kwenye eneo zima la bajeti ambayo tunaanza mapendekezo haya mpaka itakapofikia kilele mwezi Juni, bajeti hiyo anayeanzisha mchakato kupitia mamlaka aliyoipa ni Rais. Mipango hii ambayo tunaiongelea yote inawezesha pesa hiyo ije kwenye hicho chumba cha radiology ulichokisemea ni pesa ya Watanzania ambayo Rais amefanya kwahiyo anaposifiwa ni yeye, wewe ni catalyst tu ya kwenda kuhakikisha pesa inatumika vizuri. Kwa hiyo, unapokuja kusema kwamba wanampa sifa ambazo siyo zake wewe mwenyewe ulipaswa umpe sifa kama walivyompatia wananchi wengine. Na Rais ni muungwana nilisikia siku ile alivyokupa nafasi ya kuongea kwa wananchi wa Mbeya kama Mbunge wao, heshima kubwa. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. JOSEPH O. MBILINYI: Kwa kweli yaani sina tatizo na Rais, nina tatizo na hawa wapambe kwa sababu gani, Rais hata mimi nilimuunga mkono…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana muda wako umekwisha.