Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nakushukuru kwa kunipa fursa hii adhimu ya kuchangia Mpango huu. Pili, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya. Nitakuwa sijafanya sawa kama sitampongeza sana Jemedari wetu, Mheshimiwa Rais ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa ufanisi mkubwa katika kipindi kifupi cha miaka minne ya utendaji kama Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wengine tuliona mbali na tuliona ile kasi kwa mbali kabisa tukajua kwa mwendo huu wa Mheshimiwa Rais haya yanayotokea sasa tuliyajua kwamba yatakuja kutokea. Kwa hiyo tunampongeza sana Mheshimiwa Rais, lakini pili nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa aliyofanya na kwa kututengenezea njia ya kupita katika kujadili Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie maendeleo ya watu, kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu na nataka nijikite wenye eneo la mazingira. Katika mazingira hapa sisi maeneo ya mijini kule tunasumbuliwa sana na mafuriko, mito inakuja kuharibu miundombinu na wakati mwingine Dar es Salaam kuifanya inasimama kabisa. Kwa hiyo, katika hili napenda nijikite mfano mzuri katika Mto Msimbazi na mito mingine mingi ya Dar es Salaam. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri tunapokwenda kutengeneza Mpango huu tutolee macho katika ile mito inayotusumbua na hasa Mto Msimbazi. Najua kuna mipango inaendelea na najua kuna bajeti kubwa ambayo haiendani na uhalisia wa jambo lenyewe, lakini naamini Mheshimiwa Waziri atatupitisha vizuri hapa ili tukija kwenye bajeti tutokee vizuri tusikae hivi hivi, lazima tuje na suluhisho na hasa ninachozingatia ni kwa ajili ya kutengeneza mto na kulipa fidia kwa wananchi waondoke lile eneo tulitumie kisasa na kisayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, mazingira wezeshi, sisi watu wa Dar es Salaam pale tuna mpango wa kutengeneza barabara za kuondoa msongamano na kupunguza foleni. Mpango mzuri sana na kwa kweli tunaipongeza sana Serikali yetu na kwa kweli katika hili tumenufaika nalo sana kwa maana ya barabara, fly over Mfugale pale, hapa Ubungo, nyingine itakuja Magomeni, nyingine itakwenda Mwenge, nyingine zitasambaa. Kwa kweli tunapokwenda tunategemea sasa kwenye bajeti hii itakayokuja jambo hili lipewe uzito mkubwa kabisa ili tutakapoondoa msongamano na foleni Dar es Salaam tunakuza uchumi. Watu wakiweza kupita kutembea kurudi kufanya mambo yao kwa wakati uchumi wetu utaongezeka bila wasiwasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nisisitize katika ile mipango yetu ya kipaumbele mitatu, lazima tuweke fedha tuhakikishe tunamaliza kwa wakati. Kujenga Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere tukisuasua faida haitapatikana, itachelewa kwahiyo tuhakikishe tutakwenda kwa speed. Kujenga standard gauge tukisuasua reli inachelewa kufika Dodoma hatutapata matunda. Tukiwahi kufanya hivyo maana yake na uchumi wetu utachemka na hata mapato yetu yataongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimechungulia ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi katika kifungu cha 160(A), Serikali ilielezea ujenzi wa viwanja vya michezo cha Mwanza na cha Mbeya kwa hiyo, tusiondoke hapa lazima tufanye jambo. Mheshimiwa Rais anawapenda sana wasanii, anawapenda wana michezo. Lakini vilevile ukienda kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi, Fungu 162 tunazungumia ujenzi wa Arena wa jengo la changamano la michezo na ambalo hili nitafurahi sana tukilijenga Dar es salaam kwa ajili wasanii wako wengi, iddai ya watu wako wengi na jengo kama hili limejengwa Rwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jengo ambalo unaweza ukafanya ukumbi, ukafanya boxing, ni jengo ambalo ukaondoa ukaja uwanja wa mpira mkacheza, ni jengo ambalo ukaondoa ukafanya stage watu wakafanya burudani zao, miziki, vijana wakafanya Tamasha na hivi, ni jengo ambalo la kisasa. Na Mheshimiwa Rais aninavyomjua mie, vijana wake hawa anawapenda kweli kweli na sisi tumsaidie hili jambo lifanikiwe kwasababu ni jambo ambalo linagusa watu wengi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Utawala Bora; nimemsikiliza sana Mwenyekiti hapa, Mzee wangu Mzee Mheshimiwa Mbatia amezungumza mambo mazuri sana lakini mimi ninachosema tu, watuonyeshe mifano hawa wazee, waonyeshe mifano. Chama cha Mapinduzi
ndiyo chama pekee kimeonyesha demokrasia pana tunapofika mambo ya uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyama vingine hawana hiyo demokrasia. Wakati mwingine mambo haya yanawaharibikia kwasababu viongozi ni wale wale wa tangu tumeanza vyama vingi ni wale wale hawawapishi wengine sasa jamani kama utaratibu ndiyo utakuwa huu basi hata nyie wenyewe tu kujifanyia mabadiliko kwamba toke fulani, aje fulani, atoke fulani, hawa vijana mnawandaaje? Sasa viongozi wa vyama vya upinzani wanazeeka na wengine watakufa na vyama vyao kwasababu hakuna succession plan sasa anakuja kwenye Serikali ya Mtaa sehemu ambayo sisi tumeweka utaratibu, tumeweka Sheria, tumeweka miongozo wanafikiri Serikali ya Mtaa itakwenda kama wanavyofanya wao kule, haiwezekani. Huku kwenye Serikali za Mitaa kuna taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, watu wakijitoa mimi naona wameogopa aibu tu kwasababu pale kwangu tulikuwa na mitaa 52 na hawa waliojitoa wana mitaa miwili nilikuwa na hamu nao sana. Nilikuwa na hamu nao tuje kuwanyoosha. Wewe mitaa imepunguzwa, kwa mfano, kwangu kuna mitaa 20 tunakwenda kupiga kura sasa si ndiyo vizuri hiyo mitaa 20 ushinde yote ili uonekane mmenifanyia figisu. Mngeniachia mitaa mingi ningeshinda yote, mmeniachia 20 nimeshinda yote 20 hamna, wana mitaa miwili na kuna maeneo mengine mfano kwa Ndugu yangu pale Mheshimiwa Deo Ngalawa kule hawakuchukua hata form wanalalamika nini hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti ukienda kwa Kalanga kule wamekimbia, hapa kwa ndugu yangu hapa James Millya hapa wamekimbia sasa wakati mwingine lazima haya mambo tuyaangalie halafu mtu anakuja anasema kujenga amani, amani yetu, amani vipi? Sisi tunaolinda amani ndiyo unatusukumia tunafanya fujo na nyie mnaokata mahindi ya watu mnaonekana nyie ndiyo mnapenda amani, hili haliwezekani kwasababu kama nyie ndiyo mnakata mahindi ya watu, nyie ndiyo mnaokwenda kuvunja nyumba za watu, nyie ndiyo mnawafukuza watu kwenye upangaji halafu mkigeuka mkija hapa mnajisema nyie ndiyo mnalinda amani na siye tunafanyakazi ya kulinda amani usiku na mchana tunaonekana ndiyo tunaokuja kuleta vurugu hili jambo siyo fair. Nilikuwa nataka Mwenyekiti lazima awe fair asiwe anakionea tu Chama cha Mapinduzi, lazima tuwe fair.(Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo sijalielewa, tuna shida gani pale Liganga na Mchuchuma? Liganga na Mchuchuma tuna shida gani pale? Pale tunakwenda kutengeneza umeme wa Makaa ya Mawe, pale tunakwenda kutengeneza chuma, hivi ulimwengu wa sasa bila chuma viwanda hivi si vitakuwa viwanda vya juice tu?

Mhesheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nadhani sasa Mheshimiwa Dkt. Mpango aje ahakikishe tunakwenda kukwamuka pale Liganga na Mchuchuma kwasababu kwanza ule umeme unaotumika kwa ajili ya kutengeneza viwanda vya chuma tutaungeteneza pale kwenye Makaa ya Mawe. Kwa hiyo, ni jambo ambalo lina faida kubwa sana. Na tukianza kutengeneza chuma hata viwanda vikubwa vikubwa vitakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi imeelezea kufufua Shirika la uvuvi TAFICO. Mheshimiwa Dkt. Mpango nilikuwa naomba sasa tuje kwasababu tukifufua Shirika letu hili la uvuvi by automatic hata ile dhana ya kununua meli za uvuvi itapatikana. Tukishanunua meli za uvuvi viwanda vya samaki vitapatikana, tunakwama wapi? Kama tumeona kwenye Ndege, cha kwanza tulifufua Shirika la Ndege, tukishafufua Shirika la ndege tumeleta ndege na huku kwenye uvuvi tufufue lile Shirika letu la uvuvi tukishafufua Shirika letu la uvuvi tunakuja sasa na kununua meli za uvuvi hapo mimi nafikiri tutakuwa tumekwenda vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuja jambo lingine, tumeendelea sana kwenye mambo ya afya sasa hivi lakini lazima sasa tuje na uta…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.