Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Eng. James Fransis Mbatia

Sex

Male

Party

NCCR-Mageuzi

Constituent

Vunjo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia Mpango uliopo mbele yetu. Nami nitachangia hasa ule ukurasa wa 11 na 12, idadi ya watu na mwenendo wa umaskini wa Taifa letu na viashiria vya umaskini kwa ujumla wake. Nimetafakari kwa kina baada ya kuusoma Mpango wote na huu wa miaka mitano nikarejea kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwamba Mpango huu umejikita zaidi kwenye Dira ya Maendeleo ya 2020-2025, Malengo Wndelevu ya 2020-2030 na Mpango huu wa miaka mitano na huu wa sasa kuanzia 2016/2017-2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alituasa na imekuwa ni msingi wa kimaadili wa Taifa letu kwa baadhi ya wosia mbalimbali za Mwalimu Nyerere. Kati ya maneno ya Mwalimu Nyerere ni kwamba, siyo maneno, falsafa ya Mwalimu Nyerere ni kwamba ili tuendelee (maendeleo) Mpango, unatengeneza Mpango wako ili uendelee vizuri tunahitaji watu, tunahitaji ardhi, siasa safi na uongozi bora. Uongozi ukisoma kwenye malengo endelevu ya dunia ni uongozi shirikishi. Mpango unaanzia chini unaenda juu lakini kwingine maeneo mbalimbali unakuwa vice versa, unaweza ukaenda horizontal, au unaweza ukatoka juu ukaenda chini lakini hasa kushirikisha watu wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wetu ili ufanikiwe lazima msingi uimarike zaidi, hata nyumba yako ukijenga ili iweze ikasimama imara msingi ni jambo muhimu kuliko jambo lingine lolote. Msingi ulio imara katika kuhakikisha Mpango huu unafanikiwa inaelezea hapa katika mambo matatu inasema suala la usalama, amani, ulinzi na utengamano wa kijamii. Utengamano wa kijamii, jamii inapokuwa pamoja inafikiri pamoja, inashirikiana pamoja kwa sababu maendeleo ni yao. Dunia ya leo mpango au jambo lolote lenye tija limewekewa vigezo vikuu vinne, kigezo cha kwanza ni kukuza utu wa mwanadamu, utu! Kigezo cha pili ni utulivu wa fikra (piece of mind); kigezo cha tatu ni rasilimali muda; na kigezo cha rasilimali fedha. Unaweza ukakopa fedha, deni la Taifa limefikia trilioni 52.3 sawa na utazilipa kesho lakini huwezi ukakopa rasilimali muda, muda ukishaondoka umeondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 2002 tukiwa viongozi wa vyama tulisema ili tushirikiane na Serikali yetu vizuri, Mzee Mangula akiwa Katibu Mkuu wa CCM lazima tuandae Chuo cha Kitaifa cha Kuandaa Viongozi. Viongozi hawaokotwi kwenye majalala, viongozi huandaliwa. Naona hata debate inayoendelea sasa hivi ya namna gani ya umoja wa Kitaifa ukizingatia kwenye wimbo wetu wa Taifa ambao tayari tulishaandaliwa, je tunautumiaje. Kutumia hekima, umoja na amani ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye malengo endelevu ya dunia imeelezea kwanza lengo la kwanza namna ya kuondokana na umasikini, la pili linazungumzia kuhusu njaa, la tatu linazungumzia ustawi wa jamii na afya na afya ndiyo rasilimali kubwa, utajiri mkubwa kuliko wote wa binadamu. Ukisoma Yoshua Bin Sira, Sura ya 30:16, utajiri mkubwa kuliko wote kwa mwanadamu ni afya yake. Halafu unaenda ya nne inayozungumza nini, elimu bora, sawa, shirikishi kwa wote (quality) ili jamii iweze ikajitambua vizuri. Ukienda ya tano unazungumzia akinamama, usawa wa jinsia na unajua kama rasilimali na hasa akinamama ukiwapa uwezo zaidi ile electromagnetic force inayotoka kwenye mioyo yao ni tofauti na ya wanaume na hii ni sayansi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sayansi iliyofanyika miaka 300 iliyopita inajaribu kuchambua hisia ambazo zimekuwepo ulimwenguni zaidi ya miaka 5,000 iliyopita kabla ya Kristo kuhusu electromagnetic force ya hisia, kunuia na kunena. Hisia, kunuia na kunena (electromagnetic force). Hata sauti za akinamama zinavyozungumza tu ni tofauti na za wanaume hasa kwenye ile nguvu ya mioyo yao namna ya kuifanya jamii iweze ikashiriki maendeleo yao pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kwetu huu ni mwaka wa takribani wa 57 wa uhuru, rasilimali viongozi iko wapi? Huwezi ukasema kazi waliofanya labda Baba wa Taifa, akaja Mzee Mwinyi, akaja Mkapa, akaja Mheshimiwa Kikwete, na sasa hivi tunaye Mheshimiwa Magufuli, ni uongozi shirikishi na uongozi endelevu wa pamoja. Rasilimali viongozi ukiangalia hata debate inayoendelea, majibu yanayotoka kuhusu umoja wa Kitaifa yanatolewa majibu badala ya kutolewa majawabu yaliyo sahihi kwa ajili ya mustakabali wa Taifa letu. Najiuliza kwa mfano, mimi Mbunge wa Vunjo, Mbunge wa Vunjo maendeleo nayaangalia pale kijijini kwangu namna gani ile jamii naishirikisha kwenye msaragambo, kwenye mitaro yao, kwenye masuala yao ya elimu, masuala yao ya afya, namna gani wanashiriki kwenye maendeleo yao endelevu ya kila siku ambayo ni jamii inakaa pamoja wanaona fulani ndiyo anayefaa kutuongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii mimi Mbunge wa Vunjo niliyepata kura 73% ya wapiga kura wote pale Vunjo, yaani wagombea wote wa Chama cha NCCR Mageuzi ambao tulishawaingiza wamesajiliwa 1,008 hakuna mwenye sifa hata moja wameondoa wote, wote, kwamba hawafai na ni halmashauri yote ya Wilaya ya Moshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hayo maendeleo endelevu shirikishi ambayo Mbunge yuko tofauti na Madiwani, Madiwani wako tofauti na Wenyeviti wa Vijiji. Hayo maendeleo tusilichukulie hili jambo ni jepesi jepesi, soma lengo la 16 la malengo endelevu ya dunia. Linasema ili ku- transform the world lazima kuwe na justice, piece and strong institutions, tuwe na haki, amani na mifumo imara na endelevu. Siyo majibu yanayotoka hapa, unachonuia ile electromagnetic force. Tulichukulia amani ya Taifa letu, amani ya Mama Tanzania na leo ni Ijumaa, Mtume Mohammed (Swalla Allah Alayh Wasalaam) anatuhusia, ukiona uovu unatendeka zuia, ukishindwa kuzuia kemea, ukishindwa kukemea onesha basi hata hasira, onesha basi hata chuki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe tu Serikali kwa nia njema na Mpango huu ulivyoeleza, ili uweze ukawa endelevu na nzuri tukubali kuridhiana Taifa hili ni letu sote. Vyama vya Siasa ni vikundi tu katika jamii lakini vyama vya siasa vitasambaratika lakini Tanzania itabaki kuwa hii moja. Mama Tanzania apewe upendeleo na tumrutubishe zaidi aweze kunyonyesha kizazi hiki na vizazi vijavyo, amani yetu ipewe kipaumbele kuliko kitu kingine chochote. Tunazungumzia umasikini huku, watu wanakata mashamba unasikia mahindi yamekatwa, chuki inajengeka na mahali penye chuki panakuwa na woga na mahali penye woga amani inatoweka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba chonde chonde, ili haya yote tuweze tukayafanyia kazi vizuri na yakawa ni shirikishi kwa wote bila migongano ya aina yoyote, niombe viongozi, siasa safi na uongozi bora, ukimsoma kiongozi, usome Yakobo 3:18 anakuambia “Amani ni tunda la wapenda amani wanalolifia”, na hiyo mbegu ni ipi! Mbegu yenyewe ni ipi, ni haki na uadilifu, haki na uadilifu. Sasa tuone kizazi hiki tunarithisha nini vizazi vijavyo ili Mpango wetu huu wa kuondoa umaskini huu kila Mtanzania ashiriki. Let say, pale Vunjo kwa mfano, wanamchukia Mbatia, ana sura mbaya, hawamtaki na nini, lakini kumchukua Mbatia kusisababishe wana Vunjo wasishiriki kwenye maendeleo ya Taifa lao la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya maneno yanayosemwa tusiyachukulie wepesi wepesi, TCD ilipoanzishwa na Mzee Mkapa ilikuwa ni ya kuleta jamii kwa pamoja. Vyama vilivyo na wawakilishi Bungeni, tukae, tuzungumze, tuishauri Serikali na Katiba yetu. Wabunge tukae tuishauri Serikali, tuisimamie Serikali vizuri……

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.