Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mapendekezo ya Mpango kwa jioni ya leo na nimshukuru sana Mungu kwa kutupa kibali tena cha kukusanyika mahali hapa. Pili nikipongeze sana Chama cha Mapinduzi na Serikali yake kwa kuendelea kutekeleza shughuli zake kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania kwa kiwango kinachoridhisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mapendekezo ambayo tumeyasoma na tunampongeza Mheshimiwa Waziri, mimi naomba leo jioni hii nijikite katika maeneo makubwa matatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba uchumi wa nchi yetu unakua na miradi ya kimkakati inatekelezwa na kazi zinaonekana, lakini ni ukweli pia kwamba tunalo tatizo kubwa la ajira nchini. Mheshimiwa Waziri kama anakumbuka kabisa kwamba Serikali kama Serikali haiwezi kuajiri Watanzania wote yenyewe, lakini ajira tunayozungumza leo ni ajira ya sekta binafsi. Mheshimiwa Waziri pia anafahamu kwamba mabenki mengi yameweka masharti ya upatikanaji wa mikopo ili wananchi wengi waweze kujiajiri katika sekta binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri katika eneo hili, unajua Serikali inapeleka karibu bilioni 23 katika kutoa elimu bure katika maeneo yetu na katika historia ya nchi yetu karibu kila kata ina shule ya sekondari na katika shule hizi za sekondari kinachopatikana kule ni chakula, chumvi, nyanya, mahindi na maharage ambapo wananchi wetu ndio ambao wanalima katika maeneo yale. Hata hivyo, ukiangalia pamoja na Serikali kupeleka pesa shughuli hizi zinafanywa na wafanyabiashara wakubwa. Mheshimiwa Mpango ni muhimu tukaiona kama tunapeleka fedha katika shule ambazo wananchi wamejenga wenyewe unaachaje kuwapa vikundi vya akinamama na vijana ambao wako kule vijijini wafanye shughuli hiyo unawapa wafanyabiashara wakubwa wanafanya hata biashara ya chumvi. Hao vijana wanaotoka katika vyuo vikuu ambao hawana ajira watapataje ajira kama hata Serikali haiwezi kuwasimamia katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni eneo ambalo Mheshimiwa Waziri ni muhimu sana tukalitazama kwamba haiwezekani tunatengeneza vikundi vya ujasiriamali katika maeneo, tunatenga ile asilimia 10 ya halmashauri lakini hata mahali pa kufanya biashara na Serikali yake hakuna. Kwamba hata chumvi vijana wale hawawezi kupeleka, hata stationary vijana wale hawawezi kufanya. Kwa hiyo, nafikiri katika hili mpango huu wa fedha za elimu bure ambazo zinaenda katika shule zetu za kata, Serikali iweke utaratibu ambao wale wananchi na vijana ambao wamejiajiri katika vijiji wafanye shughuli zile ambazo wao wanaweza waka- supply ikiwepo chumvi, sukari hata ikiwepo basi upelekaji wa maziwa, nyama na vitu vingine ambavyo vinapatikana katika jamii yetu. Tukifanya hivyo tutakuwa tumewasaidia vijana wetu ambao wanamaliza vyuo ili wapate shughuli za kufanya katika maeneo yao na wakakuza uchumi wao. Tusipofanya hivyo haitawezekana kuwasaidia vijana ambao tunaona kuna tatizo kubwa la ajira nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hili tatizo la maji nchini, nafikiri tatizo sio fedha na unajua kwamba Serikali inapeleka fedha nyingi sana katika miradi ya maji, lakini tangu uhuru wa nchi hii pamoja na miradi mikubwa ya maji ambao imetengenezwa na Serikali haijawahi kupunguza tatizo kubwa la maji kwa kiwango hicho. Ni kwa nini? Ni kwa sababu miradi mingi ni hewa na haitekelezwi kwa kiwango kinachostahili kutekelezwa. Naiomba Serikali kabla ya kufanya mipango mingine ifanyie auditing ya miradi yote ya maji nchini kama ambavyo nimewahi kushauri ili tujue kwa nini tunapeleka fedha nyingi katika miradi ya maji, lakini tatizo la maji halipungui nchini. Hili ni tatizo kubwa sana, miradi ya kwanza inakwisha, lakini ikianza miradi mingine ile ya awali inakufa na haitoi maji. Kwa hiyo, ni lazima Serikali ipate nafasi ya kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ambalo linafanyika ni kwamba anayefanya tathmini ni Wizara ya Maji ambaye ndio mtekelezaji wa miradi, halafu unampa akafanye tathmini mwenyewe, unamwagiza Waziri akafanye tathmini, wataalam wale wale waliotekeleza miradi ndio wanafanya tathmini, hii haikubaliki. Ni muhimu katika hili tukafanya tathmini, kwa nini tatizo la maji nchini halipungui pamoja na kwamba Serikali inapeleka fedha nyingi katika maji, lazima tuone tatizo liko wapi katika utekelezaji wa miradi yetu. Aidha, ni miundombinu tunatengeneza vibaya au kuna uchakachuaji mwingi wa fedha katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kushauri katika eneo hili pia tujifunze Wizara ya Afya na TAMISEMI kwa kutumia force account ili fedha nyingi ziende kwenye shughuli za maji. Miradi mingi ya nchi yetu ya maji hakuna mradi unaoshuka chini ya bilioni moja, haina maana kama miradi ni ghali hivyo lakini wakandarasi wengi katika mfumo ule wa manunuzi, fedha nyingi zinaenda kwa wakandarasi na maji hayaendi kwa wananchi. Kwa hiyo naomba ikiwezekana tutumie force account katika kupanga mipango kwa mwaka unaokuja ili maji yaweze kupatikana katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo langu la mwisho ni tatizo la masoko ya mazao ya kilimo na mifugo. Wenzangu wamezungumza, lakini hivi ni kweli kwamba wananchi hawazalishi, la hasha! Hivi ni kweli hatuna mifugo bora, la hasha! Hivi ni kwamba wananchi hawazalishi pamba, la hasha! Tatizo kubwa ni upatikanaji wa soko la mazao hayo, kwa hiyo wananchi wetu wamekata tamaa katika kuzalisha. Naamini kama Serikali itaamua ikawekeza nguvu kubwa katika upatikanaji wa masoko katika mazao yanayotokana na wananchi wetu naamini kila mtu atazalisha kwa kiwango kinachotakiwa. Leo unakuta mtu anazalisha pamba, watu wanasema hiyo mikoa 17, lakini pamba inaoza nje, yule mwananchi mwakani ni lazima atabadilisha zao ataanza kuzalisha zao lingine, lakini kama tungekuwa na soko la uhakika la pamba kila mwanachi angezalisha kwa kiwango kinachostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali kwa sasa iweke nguvu kubwa katika maeneo ya kupatikana masoko ya uhakika ili wananchi wetu waweze kuzalisha kwa tija na kiwango kinachotakiwa. Ndio maana tunasema hata katika mifugo watu wengi wanahangaika kuhamisha mifugo na kusafirisha nje kwa kuvunja sharia, lakini kama tungekuwa na viwanda vya kutosha nchini vya mazao yanayotokana na mifugo kama viwanda vya maziwa, viwanda vya ngozi, hakika leo tusingekuwa tunapata watu wanaosafirisha ngozi kupeleka nje. Hivyo, kwa sababu masoko hayapatikani nchini na viwanda havipo ndio maana uzalishaji unakuwa mchache na watu wanatorosha mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuacha nchi yetu na wafugaji wetu na wakulima wakajihangaikia soko wenyewe wakati Serikali yao ipo. Ni lazima kama ambavyo tumewekeza katika miradi mingine mikubwa tuwekeze katika upatikanaji wa soko kwa ajili ya bidhaa na mazao ya kilimo kwa wananchi wetu tukifanya hivyo wananchi wetu watazalisha. Kwa hiyo naomba katika mpango unaokuja Serikali iweke mkakati na itueleze bayana kwamba ni kwa namna gani unamhakikishia mwananchi kwamba akizalisha, akilima pamba atapata soko la pamba, akilima kahawa atapata soko la kahawa. Tusipofanya hivyo kila mwaka tutakuwa na tatizo la uzalishaji kwa sababu mtu anaona kwamba zao hili halina soko, anaacha kuzalisha. Kwa hiyo Mheshimiwa Mpango hili ni eneo ambalo ni lazima tuhangaike, tusipofanya hivyo tutakuwa hatuwasaidii wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ndege tunazonunua, tunaipongeza Serikali kwa kununua ndege, kama hatutakuwa na shughuli zinazowasababisha wananchi wetu kutumia ndege hizo, hizo ndege hazitazalisha, lakini kama tutaendelea kuwa na shughuli ambazo wananchi wana- move kutoka sehemu moja kwenda nyingine lazima lile Shirika la Ndege litakuwa na ndege zetu zitaonekana za maana. Ndio maana nilikuwa nawaambia watu huwezi kufanya utalii bila ndege kwa sababu mtu akishuka Dar es Salaam ni rahisi kusafiri kwenda Arusha kwa ndege na yule anayefanya biashara lazima aende huko. Kwa hiyo lazima tuone kwamba faida za zile ndege ni kuwasaidia pia Watanzania kutoka sehemu moja kwenda nyingine kufanya biashara na moja ya biashara wanazofanya ni pamoja na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hakuna mzunguko wa fedha za shughuli anazofanya, shirika hili litakuwa haliwanufaishi Watanzania. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Mpango katika mpango unaokuja tuhakikishe basi kwamba masoko ya mazao ya wakulima yanapatikana ili ndege hizi tunazozinunua wananchi wasafiri wakauze mazao nje, wasafiri Dar es Salaam waende Mwanza na kwingine kwa sababu kuna biashara inayozunguka. Kama hakuna upatikanaji wa soko la uhakika hizi ndege hazitawasaidia watu wa chini na hakika ina maana kwamba haitakuwa na faida kwa mtu mmoja mmoja. Kwa sababu tumeshajenga miundombinu rahisi sasa ya upatikanaji wa ndege, barabara zinajengwa, ni lazima sasa tuwajengee wananchi wetu uchumi kwamba katika barabara hizo waweze kusafirisha bidhaa zao na pia wapate masoko. Kwa hiyo Mheshimiwa Mpango naomba katika eneo hilo tujitahidi sana ili na eneo hilo lipate suluhu la kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la mwisho, ni namna ambavyo biashara zetu zinakwama nchini. Naomba nitoe challenge kwenye Bunge na kwa Serikali, kwa nini tusifanye tathmini kwa miaka mine, hii ya biashara nchini, ni wapi tumekwama na tufanye nini ili basi tuweze kuendelea mbele na biashara zetu. Tunaangalia hapa upatikanaji wa mikopo binafsi imepungua kuliko mategemeo ya Serikali na kwa nini tunaona hata mabenki mengi mikopo imepungua. Lazima kama Serikali itusaidie Watanzania tufanye nini ili biashara zetu ziendelee kunawiri tusiendelee kukwama kama ambavyo tunaona. Kwa sababu tunaonekana kila mwaka hatufanyi vizuri, lakini tathmini yetu inatuelekeza nini kinatukwamisha katika biashara, mzunguko wa fedha unaonekana sio mkubwa sana, watu wanalalamika lakini ukweli biashara zinafanyika. Kwa nini tusifanye tathmini kuangalia ni nini ambacho kimekuwa kikwazo hasa katika biashara. Kama barabara zipo, kama miundombinu rafiki ipo, kama blue print ipo, ni kwa nini bado biashara zetu hazijatengemaa vizuri. Nafikiri katika mipango inayokuja ni muhimu sana Serikali ikafanya tathmini katika eneo hili kwa namna ambavyo inaweza kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, naipongeza sana Serikali, lazima tutembee kifua mbele kama Watanzania, miradi hii mikubwa inayofanyika ikiwepo ndege, barabara, ni kielelezo tosha kwamba nchi yetu inaenda kwenye mwelekeo mzuri sana. Wale unaowaona wanaopinga hilo ni kwa sababu tu wana chuki zao binafsi, lakini kazi tunaiona, Mheshimiwa Mpango kazi yake ni kubwa, anamsaidia Rais na sisi Wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wenye nia njema na Taifa hili tupo nyuma yake kumsaidia Rais na kumsaidia yeye maana uchumi huu anaoujenga si uchumi wake, ni uchumi wa Taifa letu hili na akila adui wa mipango ya Serikali ambayo ni ya kujenga uchumi, lazima wote tuwanyooshee vidole na kusema hapana haiwezekani katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunachowaomba hawa ambao wanatuongoza wazibe masikio, wasonge mbele, nchi yetu inaelekea kwenye mwelekeo, Rais anafanya kazi nzuri, nchi yetu ina maadili mazuri sana, miradi ipo na kazi inaonekana na kila mahali duniani Rais wetu anapongezwa kwa kazi nzuri. Tunachowaomba wasirudi nyuma, wasonge mbele kumsaidia Rais ili kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)