Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia Mapendekezo haya ya Mpango. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai kwa sababu wote tulio hapa tumebarikiwa kuweza kuzungumzia maendeleo ya nchi hii na wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kutamka rasmi kwa kweli kwamba Mpango huu ni mzuri na umeandaliwa kitaalam na kwenye Kamati tulipata fursa ya kuelimishwa. Sambamba na hilo, niseme mambo mengine yametekelezeka siku za nyuma ni bahati tu kwamba jambo likishatekelezeka haliwi tena motisha. Nasema hivyo kwa sababu hata guru mmoja wa management Maslow alisema: “once a need is satisfied is no longer motivation”. Hapo alikuwa anazungumzia mahitaji maalum ya mwanadamu katika maisha, ikiwemo chakula, mavazi, malazi yaani nyumba na pia labda esteem hierarchy of needs.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo? Tumekuwa na kipindi kizuri japo kwa kupambana lakini tumefuta maradhi. Kwenye Mpango wa kwanza kabisa walikuwa wamedhamiria kuondoa ujinga, umaskini na maradhi. Ujinga umeondolewa kwa jumla na sasa hivi Watanzania wanaweza wakaongea kama watu wanaoelewa. Siyo hayo tu, maradhi yaliyokuweko wakati tumepata uhuru hayapo tena. Hata awamu hii tumeona hospitali zimeboreshwa, madawa yamekuwepo, tunaona ni jambo la kawaida ambavyo siyo kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali kwa hatua hiyo. Niseme tusibweteke bali tuzidi kupambana na hapo ndiyo nasema kwamba kuna haja ya kila mmoja wetu hapa ndani kuleta mapendekezo ili kuboresha Mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunapanga? Tunapanga ili kutengeneza taswira ya siku za baadaye tunataka nini na iweje. Pia tunapanga kwa sababu rasilimali ni kidogo hatuwezi kwenda na vyote kwa mkupuo lazima tupange ili twende na vichache tupangue kila kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango huu nilitamani kuona jinsi gani mwananchi wa kawaida anapata fursa nzuri kufikia benki na ninaposema benki nina maana mabenki yaliyopo nchini. Mpaka sasa hivi tuna commercial banks zinazozidi 50 na zinakaribia 60 tuseme zaidi ya 57 lakini mabenki hayo pamoja na watu kupenda kuweka hela zao benki kwa usalama, kuweka katika amana ili waweze kuzifaidi siku za baadaye na ili ziweze kuongezewa, ukiweka kwenye amana unapata interest rate yaani unapata faida imekuwa ngumu kwa sababu gharama ambazo benki inatumia kuweka hela zile imezidi ile asilimia 3 ya amana inayolipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najiuliza mwananchi huyu wa kawaida ambaye hataki kulalia hela yake kama mto, hataki kuificha ikaja kuliwa na mende na panya au siafu, anafanyaje ili aweze kupata raha ya kuweka hela yake benki? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo mwananchi huyu huyu anapopeleka hela yake benki kuna mwingine ambaye yuko tayari mwenye uelewa zaidi anakwenda kukopa. Hapa kwenye ukopaji wako wa aina mbili, wako wakopaji ambao ni wa biashara, wakopaji wakubwa wakubwa au hata kama hakopi lakini wafanyabiashara wakubwa kama aliyekaa kushoto kwangu, lakini wako wakopaji wadogo kama mimi ambao tunakopa katika mishahara yetu na wafanyakazi wote wa nchi hii. Ukija kuangalia riba zao zinalingana anayekopa kwenda kufanya biashara ni asimilia 16 au 17 na anayekopa kutoka kwenye mshahara ni asilimia 16 au 17. Sasa najiuliza uhalali uko wapi? Natamani kuona Mpango huu wakati unaandaliwa mabenki hayo yanakaa chini na Serikali na kuona namna ya kuteremsha riba hii ya kukopa. Unakuta Benki Kuu iko vizuri, discount rate sasa hivi imefika 7 ambapo ndiyo gharama ya commercial banks kuchukua hela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka nadhani ni mwanzoni mwa mwaka huu au mwishoni mwa mwaka jana Serikali imeamua kuwa Treasury Single Account. Kwa hiyo, sasa hivi mabenki hayapati hela kiholela kutoka Serikali lakini hela hiyo pia haipatikana kwa gharama kubwa sana inapatikana kwa asilimia 7 tu, nilitaraji kuona anapokopa mtu wa kawaida ambaye ni mfanyakazi, Mbunge au mtu ambaye kulipa wakati wa re-payment hakuna gharama kubwa akopeshwe labda asilimia 3 juu ya ile ya Benki Kuu ya 7, kwa hiyo, iwe kwenye single digit kama asilimia 9. Katika Mpango huu ningetamani kuona hizo riba zinarekebishwa mapema iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nikirudi kwenye watu wa kawaida kuwa na account, nakwenda sasa kwenye mkulima wa korosho kwa sababu mwaka huu tumeelimishwa sana kwenye korosho anayefungua account katika benki wakati wa mauzo ya korosho. Mauzo ya korosho au kahawa yako kwa msimu, msimu ukiisha kashachukua hela yake amekwenda kujenga, amekwenda kufanya nini mpaka msimu mwingine tena wakati analipwa na lazima alipwe kwenye benki, anakuta ile account imeshakuwa dormant anaanza kuhangaika. Mzee huyu ametoka kijijini ametumia gari, amelala kule ili aweze ku-activate account, ni jinsi gani Serikali itaelekeza au itaongea na mabenki haya hizi account za hawa wakulima ziweze kuwa wazi bila gharama wala usumbufu leta barua kwa Mwenyekiti, leta kitambulisho hiki watu hawa account hizo ziwe wazi kila wanapokuja kuingiza hela yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kupendekeza jambo lingine ambalo ni kuhusu kujenga taifa lenye afya. Taifa zuri lenye afya ni taifa la leo na kesho. Wote hapa tuna afya nzuri kwa sababu wazazi wetu walitulea vizuri kati ya siku moja mpaka miaka mitatu. Sasa hivi unakuta utapiamlo bado uko katika maeneo yetu, hata maeneo ambayo unaweza ukafikiria labda wana vyakula sana na ambayo unaweza ukafikiria labda lishe ni bora ikiweko Kilimanjaro bado kuna utapiamlo, Mbeya bado kuna utapiamlo, hiyo ni Mikoa ambayo nina uhakika utapiamlo uko kati ya asilimia 29 mpaka 30. Sasa Mpango huu unatusaidiaje kuhakikisha kwamba tunafuta kabisa utapiamlo katika nchi hii kama tulivyodhamiria kufuta kabisa watu kutembea bila viatu, tumeweza tukafuta watu hao hao wakaweza kuwa na afya bora, tukawa tunatoa dawa za minyoo shuleni, tunakwenda tunatoa vaccination shuleni, nakadhalika na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiitumia Wizara ya Mifugo na Wizara ya Kilimo tunaweza tukafuta utapiamlo. Wananchi wakielimishwa kuwalisha watoto wao vizuri na sasa hivi Waziri wa Afya anasema kabisa mtoto wako asile chochote mpaka miezi sita na kila binti anayejifungua sasa anatamani kunyonyesha kwa sababu pia binti ukionekana hunyonyeshi tayari unaonekana una yale maradhi, kwa hiyo, siku hizi wananyonyesha. Baada ya muda wa kunyonyeshwa mtoto huyu aendelee kupata chakula kizuri hata ule uji unaopikwa mashuleni uwe mzuri, uwe na maziwa, yagawanywe shuleni watoto wale wadogo wanywe uji wa maziwa mazuri na mayai yagaiwe shuleni, yai moja moja kila mtoto, watoto wetu wale vyakula vizuri waondokane na utapiamlo. Mama mjamzito ale vizuri kwa sababu mtoto anaanza kupata virutubisho akiwa ndani ya mama na siyo nje. Mama akila vizuri anachokula kinaenda kwa mtoto na baada ya kujifungua hicho hicho ndiyo mtoto anaendelea kunyonya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo niombe kabisa Mpango huu uonyeshe jinsi gani mama atatuliwa ndoo ya maji ifikapo 2020/2021. Tumelipigia kelele huku Bungeni hata tumeomba iongweze shilingi 50 lakini bado kuna maeneo hayajawezekana. Kuna maeneo ambayo yamefika asilimia 90 nayo ni mjini lakini vijijini maji safi na salama hakuna kiasi hicho. Naomba tunapoelekea kumaliza Bunge hili turudi tukisema angalau tulizungumzia maji na sasa Tanzania nzima ina maji safi na salama na hakuna mwanamke anayejitwisha ndoo umbali mrefu, muda ule wa kwenda kubeba maji anautumia kulea familia na kwa kazi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusu mazingira. Natamani kuona ifikapo mwisho wa Mpango huu hakuna mwanamke anayepikia kuni, wala mkaa ila wote tunatumia NLG (gas) na tupewe mafundisho ya kutumia gesi ili zisije kuleta madhara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge tuko hapa tunatamani kusaidika na sisi tukasaidie watu wetu, naomba sana chondechonde viingie kwenye Mpango. Ahsante kwa nafasi hii nashukuru. (Makofi)