Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii niweze kuchangia Mpango ambao ni wa awamu ya pili kati ya Awamu Tatu za Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Nilikuwa najaribu kupitia Mpango huu wa 2016/2017 - 2020/2021, nilikuwa najaribu kupita kwenye maeneo ambayo yamefanyiwa utekelezaji na kwa kiasi kikubwa naweza kusema tuipigie Serikali makofi kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo siri, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, tunakaa tuna-negotiate mambo mbalimbali kwenye kikao, kwa kweli nchi yetu kwa miradi mikubwa ambayo inafanyika imetubeba sana. Na mimi niwaambie Wabunge wa CCM kama kuna wakati mmefanya mambo mpaka yamefilisi upande wa kule kwenye hoja ni kipindi hiki. Mambo mazito kweli kweli! Siku moja nilikuwa namsikiliza kiongozi mmoja anasema, unajua uamuzi wa kununua ndege; ziko ndege ngapi? Kununua ndege saba…

MBUNGE FULANI: Nane.

MHE. MARWA R. CHACHA: Nane eeh!

MBUNGE FULANI: Eeh!

MHE. MARWA R. CHACHA: Siyo mchezo! Ni maamuzi magumu, lazima mtu awe ameamua kweli kweli. Mtu mwepesi mwepesi hawezi. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa maamuzi yake. Nilikuwa nasikia asubuhi kwenye Ripoti ya Kambi ya Upinzani wanasema Mpango haufuatwi, haujatungiwa sheria, ni maamuzi ya mtu mmoja.

Mheshimiwa Spika, nikawa najiuliza, nikawa napita kwenye Mpango humu nione uamuzi wa mtu mmoja ambao umetekelezwa ambao uko nje ya Mpango ni upi? Nikakuta Bandari imo kwenye Mpango, reli iko kwenye Mpango, ndege ziko kwenye Mpango. Sasa nitamwomba rafiki yangu Mheshimiwa Silinde atuoneshe kitu hata kimoja tu ambacho humu hakimo ambacho kimefanyiwa maamuzi yaliyo kinyume na Katiba na Sheria za Nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-chip in kidogo baadhi ya maeneo ambayo ninadhani tuyarekebishe ambayo kimsingi kwenye utekelezaji wa Mpango nimeona yana shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo. Ukisikia watu wanalia hawana hela mfukoni, ujue kwamba kuna shida kwenye Sekta ya Kilimo. Kama kuna eneo ambalo kiukweli tunahitaji kupeleka nguvu kubwa, kuwekeza ni kwenye kilimo. Mfano, kule ninakotokea Jimboni kwangu Serengeti, wananchi wa Serengeti walikuwa wanalima tumbaku. Kulikuwa na Kampuni ya Alliance One, wakilima tumbaku, wakivuna wakiuza, shilingi bilioni 20 zinazungua ndani ya Wilaya. Unakuta watu mifukoni wana pesa. Tangu kampuni ilivyoondoka, pesa hakuna. Kwa nini? Kampuni imeondoka. Kwa hiyo, jambo hili la kilimo lazima tulitazame kwa upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mpango huu tuna mikoa 17 inayolima pamba. Nimekuwa nikijiuliza, hivi ni lazima sisi Tanzania twende kuuza pamba ghafi nje? Kwamba mikoa 17 izalishe pamba, sisi tuwe watu wa ku-export pamba, hii itatuchukua mpaka lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka enzi za Mwalimu Nyerere kulikuwa na viwanda vingi sana vilivyokuwa vinachakata pamba, kwa mfano, MWATEX, KILTEX, MUTEX na vingine vingi. Sasa mimi nikadhani Serikali ukiiuliza inasema mambo ya viwanda ni Sekta Binafsi inatakiwa ijenge, lakini kuna viwanda vingine lazima Serikali iingilie kati kuangalia namna ya kusaidia Sekta Binafsi kujenga viwanda. Maana ukijenga kiwanda cha ku-process pamba, leo utaokoa wananchi wa mikoa 17. Siyo jambo dogo!

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Serikali inaweza kutoa mabilioni ya pesa ikajenga miundombinu kwa mfano, ukanunua ndege hata moja, ni billions of money lakini kumbe unaweza uka-finance sekta binafsi kwa kutumia Mfumo wa PPP ikasaidia kujenga kiwanda cha ku-process pamba ambacho kiwanda hicho kitaokoa wakulima wa mikoa 17.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mawaziri husika, jambo hili la kilimo cha pamba liangaliwe kwa upya, kwa undani. Kama ambavyo tumeingia PPP kwenye miradi mingine, tunaweza kuingia PPP kwenye kiwanda cha kuchakata pamba tukaleta ajira kwa wananchi wetu ambao wengi wanategemea pamba. Hilo lilikuwa wazo langu kwenye kilimo cha pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kwenye barabara. Unakumbuka kilianzishwa chombo kinaitwa TARURA kwa ajili ya kusimamia utengenezaji wa barabara mjini na vijijini na sababu ilikuwa ni kwamba wakati fedha zikienda kwenye Halmashauri zimekuwa hazitengenezi barabara zetu kwa kiwango kinachotakiwa. Iliamuliwa kwamba kingeundwa chombo hiki kikasimamia utengenezaji wa barabara za vijijini na mijini, barabara zingekuwa za kiwango, lakini hali imekuwa sivyo. Kwa nini hali imekuwa sivyo? Ni kwa sababu TARURA wanapata pesa kidogo, pesa wanayopata ni ile ile ambayo Halmashauri za Wilaya zilikuwa zikipata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumbuka kwa sasa TARURA hawako chini ya Halmashauri, wana Ofisi wamepanga mitaani, kwa hiyo, wanalipa bill za majengo. Wanatumia gharama kubwa kwa ajili ya bill za ku-rent majengo. Kwa hiyo, ni gharama kubwa kwanza kuendesha chombo hiki. La pili, pesa wanayopata ni ile ile. Kwa mfano, nchi nzima TARURA inahudumia kilometa zaidi ya 100,000, wanapewa shilingi bilioni 250, hazitoshi hata kidogo. Hizi shilingi bilioni 250 ni pamoja na barabara za lami kwenye Majimbo mbalimbali. Kwa hiyo, unaweza kuona ni hela kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri, TARURA na TANROADS kutegemea Mfuko wa Barabara, shilingi 100 ya mafuta peke yake haitoshi, lazima Serikali ije na financing nyingine ya kuisaidia TARURA kusimamia barabara. Kwa wale Wabunge wa Majimbo tunaotokea huko Majimboni, hali ni mbaya kwenye vijiji kiasi kwamba mazao ya kilimo kutoka vijiji fulani kwenda sokoni inashindikana. Magari yanashindwa kwenda kuchukua mazao kwenye vijiji hivyo. Kwa hiyo, naomba Wizara, mbali na Mfuko wa Barabara tutafute chanzo kingine cha ku-finance TARURA ama tuongeze shilingi 50/= kwa ajili ya TARURA peke yake ili tuweze kuhudumia barabara za vijijini na mijini ambazo ziko chini ya TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vinginevyo kama hakuna chanzo kingine cha kuisaidia TARURA ni bora Serikali ikubali kuchukua maamuzi magumu kwamba popote kila Wilaya ilipo, TARURA waruhusiwe ama wakopeshwe fedha wawe na vifaa vya kutengeneza barabara ili fedha ambayo ni ruzuku wanayoipata ya Mfuko wa Barabara watengeneze wenyewe, vinginevyo barabara zetu zitaendelea kuwa mbaya sana. Kwa hiyo, huo ni ushauri wangu ili TARURA ikae vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni Sekta ya Utalii. Sekta ya Utalii ni moja ya Sekta nzuri sana ambayo inachangia asilimia 24 ya mauzo ya huduma nje ya nchi. Ni moja ya Sekta ambayo inachangia kwenye GDP ya Taifa letu asilimia 17.2. Kwa hiyo, siyo sekta ya kubeza ni sekta ambayo inahitaji tuitazame kwa macho mangapi mangapi ili iweze ku-boom.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii na Naibu Waziri kama wako hapa, kwa kuamua kujenga uwanja wa Serengeti uliopo Mugumu kutoka kwenye ule wa Seronera. Ni jambo zuri sana kwa sababu ndege zilikuwa zimejazana sana mle hifadhini na mnafahamu mpaka ikatokea ile ajali ni kwa sababu ndege zimekuwa nyingi. Nawapongeza sana watu wa TANAPA na Bodi ya TANAPA kwa kuridhia kwamba sasa wahamie kwenye uwanja ambao uko Mugumu. Nasi kama Halmashauri tuna hatimiliki tayari, tuna kibali cha NEM na TAA kwa ajili ya ujenzi wa uwanja ule wa ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, Mheshimiwa Mpango, kile kiwanja ni kiwanja kizuri sana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba upande wa Magharibi wa Hifadhi ya Serengeti unakuwa kiutalii. Sasa ni vizuri Serikali itazame namna ya kuwasaidia TANAPA, namna ya kuisaidia Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuboresha ule uwanja uwe katika kiwango ambacho kinatakiwa kwa sababu ndege zinaruka almost zaidi ya 200 kwa siku, siyo kitu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie barabara za kuunganisha mikoa na mikoa na hususan barabara ya kuunganisha Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha, barabara ya Makutano - Sanzate – Nata - Mugumu - Tabora B, Kilensi – Loliondo - Mtu wa Mbu. Hii ni barabara muhimu sana ya kiutalii na barabara ya kuanzia Sirari – Tarime - Mugumu ni barabara nzuri za kiuchumi kwa sababu unakuta watalii wengi wanaoshukia Kenyatta International Airport lazima waingie Sirari, Tarime. Sasa ni vizuri barabara hizi ziboreshwe kwa kiwango cha lami maana ni barabara ambazo zina fursa ya kiuchumi ili ziweze ku-boost uchumi kwa wale watalii ambao wanatembelea Hifadhi ya Serengeti pamoja na Ngorongoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni maji. Maji bado financing yake pia haijakaa vizuri. Ni vizuri kwenye Mpango unaokuja, Mheshimiwa Mpango, mwangalia namna ya kupata fund nyingine ili kusaidia huduma ya maji vijijini. Maana huduma ya maji vijijini na yenyewe ikitegemea Mfuko wa Maji shilingi 50/=, haitoshi. La sivyo, tuongeze ziwe shilingi 100 ili ziweze kusaidia. Kwa hiyo, nadhani kwenye hili ni vizuri mkaliangalia ili kuwepo na upatikanaji wa maji vijijini, kwani bado maji vijijini hali yake siyo nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na nimpongeze Waziri wa Fedha kwa kazi nzuri, naipongeza Serikai ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri. Naona kila sehemu Wenyeviti wa Vijiji wanapita bila kupingwa. Naona wenzetu wanalialia tu hawasimamishi sijui kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)