Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nianze na suala la minazi; kwetu sisi watu wa Mwambao wa Bahari ya Hindi nazi ni chakula, lakini pia inatumika kupamba miji yetu. Ukifika Lindi, Kilwa, Bagamoyo, Pangani na maeneo mengine, miji inapendeza kwa kuwa na minazi. Minazi inakufa; mwaka jana nilizungumza humu na bahati nzuri wakati fulani dada yangu pale, Mheshimiwa Dkt. Mwanjelwa, wakati akiwa Naibu Waziri wa Kilimo nilizungumza naye nikiwa jimboni kumwonesha masikitiko makubwa ya wananchi ambavyo mashamba yao ya minazi yanakufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Wizara ya Kilimo na hili nalo linawashinda? Yapo maeneo ambayo nitakutajia, kwa mfano jimboni kwangu minazi sasa imekufa kabisa. maeneo yale ya Kilangala, Mchinga, Milola, Lutamba, maeneo ya Sinde, lakini hata Kilwa kwa Mheshimiwa Ngombale hapa ukifika Miteja, nenda Kisiju, minazi imekufa, nenda kule Mafia, ukienda Pangani minazi inakufa. Hili nalo linawashinda? Naomba Mheshimiwa Waziri aje na jibu. Waende wakafanye utafiti tujue minazi hii inakufa kwa sababu gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ufuta; Mkoa wa Lindi ni wakulima wazuri sana wa ufuta na ufuta wetu ni ufuta mzuri, una mafuta mazuri, mengi. Wananchi baada ya dhoruba kubwa tuliyopigwa kwenye korosho, mategemeo yetu yalibakia kwenye ufuta, tunaanza kutaka kukata tamaa. Kuna jambo limeingizwa katika mfumo wa ununuzi wa ufuta, jambo hili linakwenda kuwaumiza wananchi wakulima wa ufuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na matajiri wale kutakiwa kukata vibali kulipa leseni zote, wameandikiwa barua na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa walipe shilingi milioni mbili ya kuchangia Mwenge. Suala la kuchangia Mwenge walilifanya liwe kwenye biashara? Hivi kuna mfanyabiashara gani atalipa shilingi milioni mbili, milioni mbili hii asiihamishie kwa wananchi? Kwa hiyo kuja kuzima Mwenge Lindi mwaka huu wanakwenda kuwatoza wananchi kulipia Mwenge?

Mheshimiwa Mwenyekiti, this is not fair. Jambo hili lazima Mheshimiwa Waziri ulitolee maelezo na ni kwamba hatutakubali, Mheshimiwa Waziri lazima uwe ukweli, kwamba sisi tutawaambia wananchi wasikubali na hawatauza ufuta wenyewe kwa sababu kwenye korosho watu wana vidonda vikubwa na nitavisema hapa. Sasa wakitaka kuturudisha na huku kwenye ufuta haya mambo kwa kweli Mheshimiwa Waziri wayaangalie vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barua aliyoandika Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kuwaandikia matajiri wanaokwenda kununua ufuta ambao msimu utafunguliwa tarehe 25, mwezi huu, ile barua suala la kuwaambia walipe shilingi milioni mbili mchango wa Mwenge ufe. Hebu imagine kukiwa na matajiri 50 watachangia milioni 100, milioni 100 hii inahamia kwa wakulima, inahamia kwa halmashauri, na mfumo wenyewe mwaka huu tunakwenda kuuza kwa mfumo wa mnada. Kwa hiyo lazima hii tozo itahamia kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, kuhusu korosho; Bunge lako hili tarehe 14, Mwezi Novemba, lilipitisha Azimio la Kuunga Mkono Serikali Kununua Korosho, humu ndani mwaka jana na tukapongeza lile jambo. Leo ukiwaambia Wabunge wanaotoka maeneo yanayolima korosho tulete orodha ya wananchi ambao bado hawajalipwa, orodha hapa tutasoma majina siku nzima. Watu wengi hawajalipwa. Mimi mwenyewe nimeuza korosho zangu, katika milioni 30 nimelipwa milioni tatu, milioni 27 nitalipwa lini, sijui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa ninavyoongea, nimetoka jimboni juzi, tayari mikorosho imeanza, msimu wa palizi umeanza na tayari kuna baadhi ya mikorosho imeshaanza kutaka kuonesha kutaka kuzaa. Kama jimboni kwangu wananchi hawajasafisha kabisa na kilio chao kikubwa watu hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mtwara kuliwekwa centre ya kulipa wakulima; wakulima walikuwa wanapiga simu pale Mtwara. Sasa hivi nasikia ile centre imefungwa kabisa, kwahiyo matumaini kwamba tutalipwa hayapo; na kwa Lindi tumeombwa radhi na Mkuu wa Mkoa kwamba tunawaombeni radhi wakulima wa korosho. Sasa hii inamaanisha nini? Mimi nawaambia, suala la korosho kwetu sisi ndiyo maisha yetu. Leo madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi ninakotoka mimi wana miezi sita hawajalipwa posho, wana miezi sita; wanakwenda wanafanya vikao ile posho yao ya mwezi hawajalipwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendeshaje halmashauri hizi? Halmashauri yetu mpaka leo makusanyo yake mpaka sasa ni asilimia 20, sasa tutatatuaje changamoto za wananchi endapo fedha za ushuru wa korosho hazitapelekwa halmashauri? Kwahiyo hili suala la korosho tusilifanyie siasa kwa mtindo huo maana kila siku tunaambiwa maneno. Jana nimeona Mheshimiwa Waziri wa Biashara anatuambia watu wa Lindi na Mtwara tunazaana sana kwasababu tunakula korosho; huu ni mzaha. Tulipeni fedha zetu, walipeni wakulima wa korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais amekuja Mtwara akasema fedha zitapelekwa bilioni 58, alivyotoka pesa zimepelekwa bilioni 18. Kwa utaratibu huu zitakwisha lini kulipwa? Wengine tuliongea humu ndani ya Bunge kuhusu suala hili tukatolewa humu Bungeni; kwamba huku tunakokwenda siko. Tukapiga na vigelegele, hivi hata Bunge halitaki kujua hatua ambayo Serikali imechukua? Mimi napendekeza kama itakufaa Bunge liunde tume iende ikachunguze, kwenye korosho kuna mambo makubwa, watu hawajalipwa, watu wametiwa umasikini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nakushauri jambo linguine; kwa kuwa msimu umeanza, basi nendeni Benki mkawakopee hawa watu basi walau waweze kufanya palizi; au mkawape bondi waweze kukopesheka. Mtu ana hela zake milioni 30, milioni 20, milioni 10 anashindwa milioni moja ya kufanya palizi shamba lake; nendeni mkawawekee bondi basi Benki waweze kuwakopesha ili kilimo kiendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza suala la korosho tunazungumza maisha yetu. Baadaye mtakuja kutuambia hapa watu wa Lindi na Mtwara tunafeli; watu hawasomi kwasababu wana-frustrations nyingi ikiwemo na ya korosho. Mtoto akienda shuleni hawezi akafanya vizuri wakati nyumbani baba analalamika hajalipwa korosho. Jambo hili Bunge lazima liingilie kati, Serikali inaonesha wazi kwamba imeshindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.