Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya na kuweza kusimama ndani ya Bunge hili Tukufu kuweza kuchangia mjadala huu wa bajeti ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri wanayoifanya na ambayo wanaendelea kuifanya ya usajili wa wakulima. Kwa sababu naamini kwa kufanya usajili wa wakulima kutatupelekea tuwe na takwimu sahihi ambayo itatusaidia kujua mahitaji sahihi ya wakulima katika masuala ya pembejeo, masuala ya masoko, lakini vilevile na miundombinu ya kilimo kwa maana ya maghala. Kwa kuwa tutakuwa na takwimu sahihi itatusaidia kupanga mipango sahihi ya kutatua changamoto mbalimbali za wakulima pamoja na wadau wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwapongeze kwa kuanza kufanya tathmini ya afya ya udongo, kwa sababu kwa kufanya tathimini ya afya ya udongo itawasaidia wakulima wetu kulima mazao sahihi, sehemu sahihi na vilevile kutumia pembejeo sahihi katika maeneo yao ambayo itawezesha kuongeza uzalishaji na vilevile kuongezeka kwa kipato cha mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nilikuwa napenda sasa niishauri Serikali katika maeneo mbalimbali, nitaanza na kilimo cha biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kubadilika ni lazima kabisa tuachane na kilimo cha jembe la mkono tujikite kwenye commercial farming. Niseme tu, isiwe large scale tuwekeze kwenye small scale ili kuweza kuwalenga kundi kubwa la wakulima wadogo nao waweze kutumia nyenzo za kisasa wakati wanafanya shughuli za kilimo kwa maana ya kutumia matrekta, lakini vilevile waweze kufanya kilimo cha umwagiliaji ambacho wataweza kuvuna na kulima zaidi ya mara mbili kwa mwaka. Hivyo basi Serikali ione umuhimu wa kuweza kuchimba malambo maeneo mbalimbali ya nchi yetu ili wakulima hawa waweze kupata fursa ya kuweza kufanya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la kilimo chenye tija; na utakubaliana na mimi kabisa kwamba wakulima wetu wanatumia gharama kubwa sana katika uzalishaji kuliko kile kivuno wanachokipata. Wakulima wengi wanapata mavuno machache hivyo basi inawapelekea pia hata faida ile ya kilimo chao kuwa faida ndogo. Ningependa niishauri Serikali; kwanza kabisa muhakikishe kwamba hili zoezi la tathimini ya afya ya udongo linakamilika mapema ili kuweza kusaidia kilimo chetu kiweze kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niiombe Wizara hii ya Kilimo ikae na Wizara ya Viwanda ione namna bora ya kutengeneza vivutio kwa wawekezaji ambao wanawekeza katika viwanda vya pembejeo, kwa maana ya viwanda vya mbolea, ili kusudi wakiwekeza kwa wingi, wakifungua viwanda vingi vya mbolea ndani ya nchi yetu hii itapelekea wakulima wetu kupata mbolea kwa bei nafuu lakini vilevile itawasaidia wakulima wetu kuwa na uhakika wa mbolea pindi wanapokuwa wanahitaji na vilevile itakuwa kichocheo cha wakulima wengi kutumia mbolea na matokeo yake kilimo chetu kitaenda kuwa na tija, uzalishaji utaongezeka kipato cha mtu mmoja mmoja kitaongezeka na taifa kwa ujumla. Vilevile tukumbuke pia uanzishwaji wa viwanda hivyo vya mbolea italeta ajira kwa vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende pia kuishauri Serikali katika suala zima la ushuru wa pembejeo za kilimo. Niishauri Serikali itoe ushuru katika pembejeo za kilimo, kwa maana ya mbolea na viuwadudu, ili kumpa nafuu mkulima aweze kununua pembejeo hizi kwa gharama nafuu na kuweza kuzalisha kwa gharama nafuu na kuweza kupata faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mbegu, naendelea kuishauri Serikali itumie vituo vya utafiti vya mbegu na kuviimarishavituo ili kuhakikisha kwamba wanazalisha mbegu bora ili wakulima wetu waweze kupata mbegu bora na kuweza kuzalisha mazao bora na kuweza kupata faida. Vilevile waangalie mbegu hizo zinaenda mahali gani, kwa mfano kwenye sehemu ambazo zina ukame wahakikishe kwamba mbegu wanazozipeleka kule ziwe zinakubaliana na hali halisi ya ukame. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuzungumzia zao la parachichi ndani ya Mkoa wa Njombe. Kwanza kabisa nimpongeza Mheshimiwa Rais, alipokuja Mkoa wa Njombe kwenye ziara yake ailituhakikishia kwamba tutapata ndege ya mizigo ambayo itakuwa inatua Songwe na kuweza kubeba parachichi zetu sisi wakazi wa Mkoa wa Njombe, lakini vilevile na wa Songwe na wa Mbeya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii fursa ya zao la parachichi sisi wananchi wa Mkoa wa Njombe tumeipokea vizuri, tunalima kwa wingi, hivyo basi nilipenda kumshauri Mheshimiwa Waziri wa Kilimo akae pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi waone namna bora ya kuweza kutumia reli ya TAZARA kwenye, yale mabehewa ya mizigo baadhi yao watengenezewe mfumo wa ubaridi na upoozwaji, kwa maana ya cold room, ili wakulima wengi watumie njia ya reli ya usafirishaji ambayo ni rahisi zaidi uki-compare na njia zingine. Hivyo basi nawashauri Wizara hii ikae na Wizara ya ujenzi ione namna bora ya kutumia ile reli ya TAZARA ili tuweze kusafirisha mazao yetu ya parachichi na yaweze kufika kwa mlaji wa ndani na wa nje yakiwa na ubora ili tuweze kuuza kwa bei nzuri na kuweza kulipa kodi na kuchangia Pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nilikuwa napenda kumwambia Mheshimiwa Waziri; hii fursa ya parachichi; maana kila mtu sasa hivi anajua kwamba parachichi sasa hivi ulimwenguni inaitwa green gold kwa sababu ina thamani kubwa sana na kila mtu sasa hivi amehamasika kulima parachichi. Lakini ningependa kumwambia Mheshimiwa Waziri, tukumbuke kwamba hii fursa ambayo sisi Watanzania hususani Mkoa wa Njombe tumeiona na Nyanda za Juu Kusini kwa maana ya Iringa na Mbeya tumeiona ya kulima parachichi na nchi zingine nayo wanaiona fursa hii, hivyo nilikuwa napenda kuishauri Serikali muhakikishe kwamba mnaingia mkataba mzuri na nchi walaji katika masuala ya masoko ili kuweza kulinda soko la mkulima wa parachichi ndani ya Tanzania yetu. Kwa sababu mnaona kwamba demand ya parachichi ni kubwa lakini kadri muda unavyozidi kuendelea kwa sababu fursa hii imeonwa na nchi nyingi baadaye supply ya parachichi itakuja kuwa kubwa na demand itakuwa iko pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi kumsaidia mkulima wa parachichi wa Mkoa wa Njombe na mikoa mingine ambayo inalima parachichi ndani ya Tanzania ni vyema basi mkaweka mikataba mizuri kwa nchi walaji ili kuweza kulinda soko la parachichi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja (Makofi)