Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana mtoa hoja kwa wasilisho zuri asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha Mheshimiwa Waziri katika ukurasa wa 10 anazungumzia kuhusu mpaka wa Mashariki ya Tanzania ambapo tunapakana na Bahari ya Hindi. Ukanda huu wa Pwani wenye urefu wa kilometa 1,424 ndipo Kisiwa cha Mafia kinapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali tete ya usalama katika eneo hili ikiwemo tishio la magaidi kutoka nchi jirani, naleta ombi maalum kwa Serikali pawepo na kikosi cha wanamaji katika Kisiwa cha Mafia ili kujikinga na matishio hayo kwa sasa hapo kikosi kidogo (detach) ambacho kina vifaa duni na hawawezi kwenda maeneo ya bahari kuu ambapo uharamia unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 21 wa kitabu unazungumzia mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa vijana. Jeshi limeweka utaratibu mzuri na kila Wilaya kupewa nafasi kwa vijana kujiunga na Jeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Mafia kila mwaka kumekuwa na tatizo la vijana kutoka nje ya Mafia wanaoletwa kuchukua nafasi hizo. Nia nzuri ya Serikali ni kuhakikisha Jeshi letu linakuwa na sura ya kitaifa lenye uwakilishi wa kila kona ya Tanzania. Hili sio suala la ubaguzi, ni jitihada za makusudi za Serikali kwa maeneo ya pembezoni kama Wilaya ya Mafia vijana wake mnapata fursa ya kujiunga na Jeshi. Ni matarajio yangu Mheshimiwa Waziri ataweka miongozo kukabiliana na hali hii inayoharibu taswira ya Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja.