Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, na mimi niungane na Wabunge wenzangu wengi kuwapongeza Jeshi letu la Ulinzi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya. Lakini nilikuwa natoa ombi kwa Wabunge na hata Kanuni zetu inabidi tuzibadilishe, inapofika kipindi tunapojadili bajeti ya Jeshi, Wabunge wote tuwe kitu kimoja. Ukitaka ujue ubora na kazi kubwa wanayoifanya Jeshi angalia yaani ukiona majirani zetu wametulia ujue Jeshi wako kazini. Maana kuna kipindi fulani makelele makelele yalikuwa yanasikika huko lakini sasa hivi yametulia. Kwa hiyo, nikupongeze sana Ndugu Venance Mabeyo kwa kazi kubwa ambayo unaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nilikuwa napenda kupata majibu, hivi wanajeshi wanapokwenda kwenye makambi kule kuna vitu gani wanapewa, mbona wakija mtaani wanakuwaga na vurugu sana, kwa sababu mwanajeshi akimkuta mtu wa kawaida kavaa nguo inayofanana na Jeshi anamvua, mwanajeshi akiwa baa akifanyiwa kitu cha hovyo inakuja kambi nzima baa kuleta vurugu, hivi kuna kitu gani mnawapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la ulinzi wa mipaka. Jukumu la Jeshi letu ni kulinda mipaka ya nchi yetu, sina hofu sana naamini kazi nzuri wanayoifanya, lakini sasa hofu yangu inapokuja ninapoona kwenye makambi ya majeshi na maeneo ya majeshi yanapoingiliwa na wananchi wa kawaida. Wananchi wanalima, wanajenga, wanauziana yale maeneo, sasa najiuliza, hivi kwenye mipaka yetu kukoje? Sina hofu sana, lakini kuna umuhimu wa kufanya ukaguzi kwenye mipaka kwa sababu siku tunaweza tukakagua mipaka ya nchi tukakuta nchi iko nusu tayari watu wameshajigawia huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni jambo la matibabu, hili ndiyo jambo kubwa sana ambalo linalalamikiwa na wanajeshi wengi. Tunajua wanajeshi wengi wanaishi kwenye makambi na sina imani kama wake zao na wenyewe ni wanajeshi. Naamini wake zao wengi wanafanya kazi nyingine na wako maeneo ya nje ya makambi na watoto wao pia wanaishi nje ya makambi kwa sababu wengine ni wanafunzi. Sasa suala la matibabu limekuwa kizungumkuti, wengi wanatibiwa katika zahanati na hospitali za jeshi ambazo ziko kwenye kambi za Jeshi tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapata taabu sana wanapopata rufaa, matibabu ambayo hawawezi kutibiwa kwenye kambi zao, mpaka waende Lugalo. Lugalo kuna urasimu wa matibabu, wanajeshi wenye vyeo vya chini wanapokwenda pale wakiwa wanaugua wanawekwa pending mpaka watibiwe watu wakubwa. Hilo suala mimi nimeshakutana nalo na Waziri analifahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanashindwa kujiunga na mifuko mingine ambayo wafanyakazi wangine wanatibiwa, wanasema na hoja ya usiri. Hoja ya usiri ipi, kwenye matibabu hakuna usiri, wanasema wataanzisha mfuko wao wa wanajeshi kwa ajili ya matibabu. Kazi yao waliyonayo tu ya kulinda nchi ni ngumu, sasa wanataka kuanzisha kazi nyingine tena. Changamoto watakayopata, kwanza wana vituo vichache vya matibabu, pili mfumo wa malipo kuuandaa ni kazi, tatu kuandaa mfumo kwa ajili ya ukaguzi na kuhakiki madeni hiyo Jeshi hawataliweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa nawashauri, Jeshi wangejiunga katika mfumo wa matibabu ambao wanaupata majeshi yote ya ulinzi, kama Polisi, kama Jeshi la Magereza, kama Usalama wa Taifa, kama PCCB, kwa sababu hata wakistaafu wanajeshi hawathaminiwi tena. Kwa hiyo, mimi naunga mkono hoja lakini suala la matibabu ya wanajeshi ni muhimu sana wakajiunga na mfumo mwingine ambao wanatumia majeshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)