Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, Bismilah Ramahan Rahim, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nataka nianze leo makatibu angalieni dakika mnatukata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kupongeza na kuunga mkono Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri nilipongeze na Jeshi letu kwa kazi ngumu wanayoifanya na nawapa hongera sana siwapi pole kutokana na kazi ngumu na ugumu kwa sababu mwanajeshi hapewi pole akifanya kazi ngumu ndio kazi yake anapewa hongera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kile ambacho kinatukwaza sisi kama raia. Juzi nadhani ilikuwa siku ya Jumatatu kuna Msemaji wa Jeshi la Polisi sikupata jina lake, lakini alikuwa ni Luteni Kanali alikuwa anatoa taarifa juu ya clip inayoendelea katika mitandao ya jamii ikionesha jinsi wanajeshi walivyofyeka mazao ya mtu ambaye amevamia katika eneo la Jeshi. Akatoa maelezo, akatoa vielelezo na akathibitisha kwamba hilo ni eneo la jeshi ambalo limenunuliwa na wale raia wamelipwa, well hatuna tatizo katika hilo. Kinachotuumiza sisi kama eneo ni la kwenu wanajeshi kihalali maana yake nini, maana yake na kilichomo ndani ya eneo lile ni cha kwenu. Sasa ninyi mlikuwa mumuondoe yule yale mazao myaache kwa sababu mazao hayo ni ya kwenu, kwa kweli sisi wakulima na watu wa mazingira inatuumiza sana tunapoona Jeshi linatumia nguvu zake tunaita utemi kufyeka mazao ya kulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Amiri Jeshi Mkuu Awamu ya Pili wa nchi hii Mzee Ali Hassan Mwinyi ni mhamasishaji m kubwa wa kilimo cha papai. Leo akikuuliza Jeshi lako linatumika kufyeka mipapai utamjibu nini? Tunaliomba Jeshi letu kama eneo ni lenu tumieni taratibu na sheria kuhakikisha mnadhibiti maeneo yenu kwa sababu kiusalama ni maeneo yenu, lakini muwe waungwana kwa sababu mazao hayana kosa lolote, tumuogope Mwenyezi Mungu yale mazao ninyi mngeyatumia mapapai ni lishe bora kabisa kwa nini myafyeke, ile hamtoi picha nzuri tumeambiwa hapa na Kambi ya Upinzani kwamba Jeshi liwe-think tank ya Taifa hili, tunataka muwe mfano bora kwa wananchi na vijana wetu. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo labda limewaumiza sasa nawapeni asali kidogo hiyo ilikuwa shubiri kwenu. Wanajeshi wetu wanafanya kazi masaa 24 lakini katika hali ya kawaida minimum wanafanya kazi masaa 12 ondoa ule muda wa kusafiri. Sasa kama anafanya kazi masaa 12 kwa nini hawalipwi overtime lakini baya zaidi kinachoumiza kwa nini mishahara yao haiwi-specific ikawa hii ni tofauti na wafanyakazi wengine. Lakini kwa nini wanajeshi hawa kama halipwi over time, hawana mishahara ambayo ni tofauti na wafanyakazi wengine wanaofanya masaa tisa, lakini bado wanaendelea kukatwa kodi ndani ya mishahara yao hii si haki, kama Wabunge tunatakiwa kuisimamia Serikali kuhakikisha kwamba wanajeshi hawa wanalipwa kulingana na namna wanavyofanya kazi, ndio maana wanajeshi hawa anapostaafu anadhalilika sana muda mfupi tu.

Kwa hiyo, tunaiomba Serikali na Mheshimiwa Waziri ulisimamie hili kuona kwamba wanajeshi hawa wanapata stahiki kulingana na kazi ngumu wanayoifanya. Minimum 12 hours ukimwangalia mtu amesimama pale halafu anakatwa kodi kwenye mshahara wake hii siyo fair kabisa kabisa, lazima hili liangaliwe na marekebisho yafanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wanajeshi hawa wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, ameligusia Mheshimiwa Anatropia, limegusiwa hata katika hotuba zote hawana insurance, hawana bima ya afya, sasa hili nalo ni tatizo. Tatizo ni nini? Kwa hiyo, tunaiomba Serikali ihakikishe kuwapatia wanajeshi hawa bima za afya kwa faida yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ambalo nataka kulizungumzia hili ni lako kama Mwenyekiti wa Kamati hii lakini kama ambaye leo uko kwenye kiti tunaiambia Serikali, Jeshi nilisema hapa na leo naendelea kusema linaweza likawa chanzo kikubwa cha kuiletea mapato Taifa hili na kuingiza fedha nyingi katika pato la Taifa kulikoni Wizara nyingine yoyote. Inaweza ikashindana na Wizara ya Maliasili na Utalii kama Jeshi letu tutalitumia vizuri kuingiza fedha za kigeni katika nchi yetu.

Niiombe Serikali kwa nini tunanunua ndege hizi tunazonunua ambazo kwa mujibu wa taarifa toka ziliponunuliwa tunapata hasara kila mwaka kwa nini? Kwa nini fedha hii isitumike kununua ndege na vifaa vya kijeshi ambapo nchi yetu tumeingia katika US Missions vifaa hivi vikatumika kule ambako tunapata fedha moja kwa moja hakuna ujanja wa namna yoyote. Kwa nini isitumike hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna nchi kama Bangladesh, Pakistan, India, Rwanda, China, Nigeria, Uruguay na Ukraine zinaendesha nchi zao kwa sababu ya huyu UN Mission tu, sisi tunashindwa nini? Kwa mfano katika pale UN ukiingia tu unalipwa iwe ni dry lease, iwe ni wet lease unalipwa pesa yako kila baada ya miezi mitatu. Risasi inalipwa, bunduki inalipwa, hanga linalipwa, gari linalipwa, ndege inalipwa sasa kwa nini inashindikana hivyo? Kwa mfano gari moja ukiingiza katika US Mission inalipwa dola za Kimarekani 4000 kwa gari moja. Sasa kama tumeingiza gari 100 pale tutakuwa tunapata kiasi gani achalia mbali ndege na hivyo vifaa vingine, kwa hiyo huo ni mfano na US Mission wanalipa kila baada ya miezi mitatu hiyo fedha hakuna ujanja ujanja kwamba wamewaambia watu wapake rangi ndege wanakwambia milioni 200 kumbe ni milioni tano.

Kwa hiyo, tunaiomba Serikali badala ya kuelekeza fedha katika miradi ambayo inaleta hasara iwekeze katika Jeshi ili Jeshi litukusanyie hii fedha. Tulishasema kwamba Jeshi likitumika vizuri nithink tank na linaendelea Jeshi hili kutuzalishia fedha nyingi za kigeni kadri inavyowezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize leo tuna miaka zaidi ya 10 nchi yetu iko katika ulinzi huu wa amani kule Sudan, DRC lakini tumepata nini? Tumepata fedha kiasi gani labda Mheshimiwa Waziri kama unazo data unaweza ukatuambia ni fedha kiasi gani, lakini bado tunaishauri Serikali iangalie namna ambayo tutalitumia Jeshi letu kama kitega uchumi na ni kuliwezesha tu tukanunua vifaa hivi badala ya kuingia katika miradi ambayo ukweli haileti tija kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kukizungumzia katika Jeshi, wanajeshi hawa kuna malalamiko makubwa namna ambavyo wanakaa muda mrefu ndani ya Jeshi bila ya kupanda vyeo. Mtu anatumikia cheo kwa miaka 12 hajapanda cheo kingine hii kwa kweli inaumiza wanajeshi wetu, lakini si inawaumiza personally inaumiza mpaka na familia zao. Kwa hiyo tunaomba huo muda ambao wanajeshi wanakaa pale jeshini uangaliwe vizuri na isiwe mtu anakaa zaidi ya miaka 12 bila kupanda cheo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine wanapoenda katika mafunzo Serikali ihakikishe kwamba inawapatia stahiki na malipo yao mapema kabla ya kuingia katika mafunzo kwa sababu wanaziacha familia nyumbani, zinahitaji huduma yeye yupo kwenye mafunzo usipomlipa kwa wakati concentration yake itakuwa ni kuangalia familia na kuangalia mafunzo matokeo yake ikija ile akiwa katika mafunzo yale ya hatari ndio unakuta tunapata majeruhi katika mafunzo. Tuiombe Serikali kuhakikisha kwamba inawalipa wanajeshi wetu stahiki zao kwa wakati kabla ya kuanza kwa mafunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba Jeshi ni kioo katika jamii yetu, Jeshi linatakiwa liwe mfano bora la kufundisha wananchi wote tabia nzuri na mwendo mzuri. Jeshi letu linafanya kazi katika mazingira magumu liongezewe bajeti, lakini hata hii bajeti finyu itoke na itoke kwa wakati ili waweze kufanya kazi zao kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kupigiwa kengele kwa sababu nimeweka stop watch leo nimeona ni dakika yangu ya tisa namalizia kwa kusema kwamba nampongeza Mheshimiwa Waziri na wanajeshi kwa kazi ngumu na nawatakia kila la heri, ahsante. (Makofi)