Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kukupongeza kwa dhati wewe mwenyewe pamoja na Mheshimiwa Najma Giga ambaye alikuwa Mwenyekiti jana kwa jinsi mlivyotuongoza tangu nilipowasilisha hotuba yangu jana, mlivyosimamia mjadala na hadi kufikia muda huu nawapongeza sana na kuwashukuru sana.

Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge 40 ambao wamechangia kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge 37 ambao wamechangia kwa kusema moja kwa moja hapa Bungeni. Kwa ajili ya muda naomba majina ya Wabunge wote waliotoa ushauri, maoni, na mapendekezo yawe kwenye orodha ya hansard kwa ajili ya kumbukumbu, nawashukuru sana.

Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Naibu Mawaziri na Mawaziri waliopata nafasi ya kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali yaliyojadiliwa. Kwa namna ya kipekee namshukuru sana Naibu Waziri wangu Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya kwa jinsi alivyotoa ufafanuzi aliotoa hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nikiri kwamba Wabunge wote waliochangia kwenye hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara wameipatia Serikali ushauri na maoni mazuri ambayo mengi tutayafanyia kazi na kutoa taarifa kupitia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira ufafanuzi wangu ninaotoa ni kwa maeneo machache yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa upande wa Kamati ni maeneo mawili tu ya kuzungumza. La kwanza niahidi kwamba mapendekezo ya Kamati tutayafanyia kazi, ingawa kuna baadhi ya mapendekezo yanagusa mikataba, kwa hiyo baadhi ya mapendekezo ambayo yanagusa mikataba itabidi yaingizwe kwenye mfumo wa majadiliano yanayoendelea. Kamati itapewa taarifa rasmi kupitia utaratibu wa ratiba zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kutopendwa sokoni kwa bidhaa zinazozalishwa nchini na ushauri wa Kamati wa kuhamasisha Watanzania kupenda kununua na kutumia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya Tanzania. Tumeupokea ushauri huo kwa mikono miwili na moyo mkunjufu, kwa sababu mtu asiyependa chake ni sawa na kutojithamini mwenyewe. Viwanda vyetu vinazalisha vitenge vizuri sana, lakini vikiandikwa made in Tanzania baadhi ya Watanzania hawanunui mpaka baadhi ya viwanda vya nguo vinalazimika kuandika made in Nigeria ndiyo vipate soko. Sasa hii ni tatizo ambalo naomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane kuliondoa katika nyoyo za Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ushauri huo wa Kamati ya Bunge letu tuanzie na Bunge, lionyeshe mfano kwa kupendekeza manunuzi ya bidhaa za Tanzania kwenye ofisi zote za umma, Ofisi za Bunge na hata Bunge hili likubali kubadilisha kanuni za mavazi ya Wabunge hasa Wabunge wanaume ikiwezekana waruhusiwe kuingia Bungeni wakiwa wamevaa mashati nadhifu ya vitenge vikiwa vya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba ya Upinzani niseme tu kwamba, mwaka wa fedha 2018/2019 haujakwisha, randama aliyoinukuu Mheshimiwa Waziri Kivuli ilikuwa na takwimu za hadi mwezi wa Tatu 2019, bado miezi minne hadi mwezi wa Nne takwimu zimebadilika na hadi wiki ijayo ninazo taarifa kwamba takwimu hazitakuwa zile zilizonukuliwa. Kwa maana hiyo kwa ajili ya kuweka kumbukumbu sawa, siyo sahihi kabisa na haitokuwa sahihi kabisa kusema kwamba eti bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ilikuwa ni bajeti hewa, isipokuwa kilicho sahihi ni kusema kwamba Serikali huwa ina umakini mkubwa katika kutoa fedha za utekelezaji hadi pale inapojiridhisha kwamba hatua stahiki za maandalizi ya utekelezaji zitakuwa zimekamilika. Mfano, baadhi ya maeneo yanayoendelea na ratiba ya mapitio ya mikataba na baadhi ya maeneo yanahitaji tafiti kwanza zifanyike na kukamilika kabla ya utekelezaji kuanza lazima fedha zake zitasubiri kutolewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Viwanda na Biashara ina imani kwamba kwa maeneo na miradi ambayo taratibu za maandalizi zimekamilika mfano wa ulipaji wa fidia kwenye mradi wa Mchuchuma na Liganga fedha zitatolewa kabla ya kwisha kwa mwaka wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili katika hotuba ya Upinzani, ni lawama na kubeza utekelezaji wa miradi mikubwa ya ujenzi wa reli ya kati kwa viwango vya Kimataifa na mradi mkubwa wa kufufua umeme wa Stiegler’s. Napenda nisisitize pongezi zangu kwa Mheshimiwa Rais kwa maamuzi ya kihistoria aliyoyafanya kujenga miradi hiyo. Kwa mujibu wa Maazimio ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Dunia uliofanyika Rio de Janeiro, Brazil mwaka 1991, uchumi maana yake ni ardhi na anga kwa maana ya mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta za uchumi ambazo ni kilimo, mifugo, uvuvi, maji chini na juu ya ardhi, maliasili ikiwemo uoto wa asili na wanyamapori, madini na ujenzi kwa ujumla na sekta za uchumi anga ambazo ni pamoja na nguvu jua, mwanga, hewa na mvua ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yoyote ile ikiwemo Tanzania. Hata hivyo uzalishaji ghafi kwenye sekta hizo hauwezi kuwa na faida kubwa kiuchumi kama sekta ya viwanda haitachakata malighafi zinazozalishwa ili kupata bidhaa zenye thamani kubwa ambazo zitafikishwa kwenye maeneo mbalimbali zinakohitajika kwa matumizi ya binadamu na viumbe wengine kupitia mifumo wa biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili Sekta ya Viwanda na Biashara itimize jukumu lake hilo vizuri, inahitaji mazingira wezeshi yanayopunguza gharama za uzalishaji, gharama za hifadhi, gharama za usafiri na gharama za usafirishaji. Kwa maana rahisi mazingira wezeshi ni bandari inayofanya kazi vizuri, barabara nzuri za lami, madaraja makubwa, mfano, madaraja ya Mkapa, Kikwete na Magufuli, viwanja vya ndege, reli ya viwango vya Kimataifa, mradi mkubwa wa kufufua umeme wa uhakika kama Stiegler’s ambao utazalisha megawati 2,100 kuwa na uhakika wa kuhudumia viwanda. Miundombinu hiyo ndiyo chachu kubwa ya uwekezaji kwenye viwanda na biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii itakapokamilisha miradi hiyo na miradi mingine ukiwemo ule ambao utatekelezwa baadaye wa reli ya Mtwara hadi Mbambabay, ambao baadaye itajengwa reli kupita kwenye maeneo ya miradi ya chuma ya makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma itachochea kwa kasi ya aina yake maendeleo ya ujenzi wa viwanda na biashara nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili limezungumzwa sana ni eneo la software kwenye biashara. Hoja hii imejitokeza kwa kuchangiwa na Wabunge wengi sana na ilionekana kama ndiyo pekee ambayo pengine inakwamisha maendeleo ya viwanda na biashara nchini. Serikali imedhamiria kutekeleza mapendekezo yaliyomo kwenye mfumo wa kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara, uwekezaji na ufanyaji biashara nchini ambao utaboresha na kupunguza gharama za uwekezaji na ufanyaji biashara. Mfumo huo ambao ndiyo blue print utakaoanza kutekelezwa mwezi Julai ndiyo ambao utakuwa ni mwarobaini wa kuondoa malalamiko mengi sana ya sekta binafsi, sekta ya viwanda na sekta ya biashara hapa nchini. Tumejizatiti na naamini chini ya uratibu na usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo mengi yatakaa vizuri na kuanzia mwaka ujao wa fedha malalamiko yatakuwa yamepungua sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, yamezungumzwa mengi sana na Waheshimiwa Wabunge kuhusu miradi ya kimkakati. Labda nikianza na Mradi wa Mchuchuma na Liganga, niseme tu kwamba Serikali imedhamiria kuanza uchimbaji wa makaa ya mawe ya Mchuchuma na chuma cha Liganga. Uendelezaji wa mradi huu utaanza mara tu baada ya mambo kadhaa kukamilika ikiwemo mchakato wa kurekebisha vipengele katika hati ya makubaliano kulingana na sheria mpya ya ulinzi wa maliasili, kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi watakaopisha utekelezaji wa mradi, kujenga miundombinu wezeshi kwenye eneo la mradi, hasa barabara, reli na njia ya msongo wa umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la kurekebisha vipengele vya mkataba ni kulinda maslahi ya nchi kufuatia Sheria mpya za Madini za mwaka 2017 na Sheria za kulinda maliasili zetu. Kwa hiyo majadiliano ya kina ni lazima yafanyike upya kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, vivutio vingi vilivyoombwa na mwekezaji vinapingana na sheria za nchi hivyo kufanya utekelezaji wake kuwa mgumu. Pili, mkataba uliosainiwa baina ya mwekezaji na Serikali una vipengele vingi vinavyomnufaisha zaidi mwekezaji kuliko Serikali. Tatu, kufanya tathmini upya juu ya kiwango na ubora wa madini ya chuma titanium, vanadium na aluminium katika mgodi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakumbuka kwamba wakati wa mkataba ule wa awali kilichokuwa kinatajwa ilikuwa ni chuma na makaa ya mawe peke yake ilidhaniwa kwamba titanium, vanadium na aluminium kwamba hiyo itakuwa na viwango kidogo sana ambavyo havitakuwa na maana katika mapato, kumbe hiyo tulikuwa tunaingizwa katika mkenge ambao Taifa hili kama mkataba ule ungesainiwa kama ulivyokuwa, inawezekana aliyesaini angebatizwa jina la Mangungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya jitihada za dhati kupunguza muda wa majadiliano ili kuhakikisha kwamba tunamaliza majadiliano ndani ya muda mfupi. Aidha, katika mradi huo Serikali inaangalia uwezekano wa kutenganisha mradi wa makaa ya mawe na ule wa kuzalisha umeme ili kurahisisha utekelezaji wake. Lengo ni kuwa na vyanzo vingi vya kuzalisha umeme wa uhakika ukiwepo uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe utakaotumika viwandani.

Mheshimiwa Naibu Spika, klatika mradi wa Liganga madhumuni ni kuchenjua na kuzalisha bidhaa mbalimbali za chuma ikiwemo vanadium na titanium ili kukidhi soko la ndani na nje ya nchi badala ya kuuza chuma ghafi. Kwa hiyo, kuuza bidhaa za chuma cha Liganga kwa wenye viwanda nchini ndiyo nia ya Serikali ili kuongeza mnyororo wa thamani na hivyo kukuza sekta ya chuma nchini. Azma hiyo itatekelezwa mara tu Mradi wa Liganga utakapoanza uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mwelekeo wa Serikali ni kutenganisha Mradi wa Chuma cha Liganga na ule wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma. Hata hivyo suala hili linahitaji majadiliano na wadau mbalimbali kwa kuwa mkataba wa awali ulikuwa unganishi kwa lengo la kuzalisha chuma na umeme kwa kutegemeana ambapo umeme unaotokana na makaa ya mawe ungetumika kuyeyusha chuma cha Liganga ili kupata bidhaa mbalimbali zitokanazo na chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tungetekeleza nina takwimu hapa, ule mkataba wa awali kama ungesainiwa ulivyokuwa, Serikali ingepoteza dola za Kimarekani bilioni kumi na tisa laki nane na milioni mia nane sitini kwa chuma na vile vile tungepoteza dola 23,342,200,000 kwa aluminium na dola milioni 450 kwa titanium. Hii ingekuwa ni hasara kubwa kwa Taifa na mikataba ya aina hii iliwahi kusainiwa huko nyuma na Bunge liliwahi kutangaza kwamba mikataba ile ilikuwa mibovu. Kwa hiyo, kwa sasa hivi tuko makini kuhakikisha kwamba tunalinda maslahi ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Soda Ash Engaruka; madhumuni ya Serikali katika Mradi wa Magadi soda wa Engaruka ambao utazalisha magadi soda kama msingi wa viwanda vya kemikali nchini yako wazi. Kwa sasa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu ambao inaitwa tekno economic study kama nilivyosema kwenye hotuba. Lengo la study hiyo ni kubaini faida na namna bora ya kutekeleza mradi huu. Kwa hiyo, upembuzi huu yakinifu utakapokamilika ndiyo utakaotushauri tutekeleze vipi mradi huu. Namwomba sana Mheshimiwa Mbunge Kalanga tushirikiane katika hili kwa sababu huwezi kuanza kujenga barabara ya lami leo kwenda kwenye eneo la mradi wakati upembuzi yakinifu haujatushauri je, tutajenga mabomba au tutajenga barabara ya lami au tutajenga barabara ya changarawe. Kwa hiyo naomba tuwe na subira, wananchi wawe na subira mradi huu utatekelezwa na tutakuwa na faida kubwa sana kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kiwanda cha Matairi cha Arusha, napenda nirejee kama nilivyosema kwenye hotuba yangu Serikali imedhamiria kufufua kiwanda hiki, kile kiwanda cha Kenya wameshakifunga hakizalishi tena kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge walikuwa wanasema hapa tunazidiwa na Kenya. Kenya watategemea matairi kutoka kwenye Kiwanda cha Matairi cha Arusha tutakapoanza uzalishaji. Kwa hiyo, hiyo ni fursa ambayo tutaitumia na hii kampuni ambayo tunaendelea na majadiliano nayo, majadiliano haya tutayakamilisha kwa haraka iwezekanavyo kama ambavyo Wabunge wameonesha ili tuhakikishe kwamba kiwanda kinaanza uzalishaji wa matairi. Tunawatafutia eneo lingine ili kuongeza eneo maana yake eneo hilo la Arusha limeonekana ni dogo, kwa hiyo tutawatafutia eneo la hekta 100 nje ya Arusha na litakapopatikana tu tayari tutaingia kwenye makubaliano rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Kiwanda cha Tabotex cha Tabora ni kweli kwamba kiwanda hiki hakifanyi kazi tumeshamwonya mwekezaji mara nyingi, ameandika barua kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu tangu mwezi wa 12 akiomba muda wa kufikiriwa kwa sababu alikuwa anatafuta mkopo TIB. Sasa mkopo wa TIB wa shilingi bilioni tano sisi hatujajua kama ameupata, lakini muda wake alioomba umepita. Kwa hiyo itakapofika tarehe 31 sawasawa na ambavyo tumezungumza kwenye viwanda vingine, kiwanda hiki itabidi kirejeshwe Serikalini kama hatakuja na concrete plan ya kuendeleza kiwanda hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kuhusu miradi ya mikakati, ni miradi ya EPZA. Miradi ambayo ni ya kujivunia sana hapa nchini ni miradi ya EPZA ingawa kuna changamoto katika baadhi ya maeneo machache, eneo la Tanga na maeneo mengine kwa ajili ya fidia, lakini miradi ambayo tayari inafanya kazi, inafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Riziki Lulida alizungumzia mradi wa EPZA wa utengenezaji wa nguo pale Ubungo, akisema kwamba wafanyakazi pale ni kama vile wananyonywa, lakini nikwambie tu ukweli kwamba wafanyakazi walioajiriwa pale kiwandani kwenye kiwanda cha Took Garment Limited ni wafanyakazi 2,600 na idadi hii itaongezeka kufikia wafanyakazi 4,000 miezi michache ijayo. Wafanyakazi ukiwatembelea pale, nimetembelea pale nimeongea nao, wanaridhika na hali ya ajira kwenye kiwanda hicho na si kweli kwamba wanalipwa sh.100,000 au chini ya hapo, wafanyakazi wengi wanalipwa mishahara ambayo wamekubaliana. Kwa hiyo kazi inayoendelea pale inaendelea vizuri na kuna amani na utulivu na hakuna mgogoro wowote na endapo kutakuwa na mgogoro mimi nitakuwa wa kwanza kuusikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Indo Power nataka nirudie tena Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza, ile Kampuni ni Kampuni genuine kabisa iko Kenya imefanyiwa due diligence vizuri kabisa na Balozi wetu wa Tanzania nchini Kenya na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, tumepata taarifa za kutosha linafanya biashara hapo Kenya na ni Kampuni ambayo inastahili kufanya biashara ndani ya Kenya, Afrika Mashariki na Duniani kwa ujumla. Sasa mkataba ambao tuliingia na kampuni hiyo mkataba ule ulikuwa halali na ulikuwa na vipengele vya utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa bahati mbaya kampuni ile imechelewa kutekeleza baadhi ya vipengele, kiasi ambacho kikafikia tukaanza sasa kupata matatizo, baadhi ya watu wengine wa Tanzania hapa, kama benki inataka kulipa labda mtu fulani anataka kununua korosho Tanzania, wakaanza kupeleka taarifa kwamba mnalipa korosho, zimeshanunuliwa na kampuni fulani. Kwa hiyo ndiyo maana tumetangaza kwamba ile kampuni tumeamua kuachana nayo ili kusudi tuweze kuuza korosho na hizi korosho tutaziuza hivi karibuni tofauti na watu ambao wanafikiri kwamba hatutauza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kulinda viwanda vya ndani, naomba tushirikiane Bunge zima, Serikali nzima na wananchi tushirikiane kuhusu suala la kulinda viwanda vya ndani. Hatua ya kwanza ya kulinda viwanda vya ndani ni kuhakikisha kwamba wanapata raw materials kwenye viwanda. Kama kiwanda kinajengwa halafu hakipati raw materials kitakufa, kwa hiyo tusije kukamata koti la Mheshimiwa Kakunda, kwamba Kakunda hajasimamia vizuri viwanda vimekufa kama vimekosa raw materials itabidi wote tusimame tuulizane. Kwa hiyo jambo la kwanza ni kuhakikisha kwamba, viwanda vinapata raw materials.

Mheshimimiwa Naibu Spika, mimi na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo tumeshazungumza tumekubaliana viwanda, kwa mfano, viwanda vya korosho tumekubaliana vitapata raw materials. Hata wale wanaotaka ku-invest kwenye viwanda vya korosho Tanzania tunawapa mkataba maalum kuwahakikishia watapata raw materials ili viwanda visife wala kuhamishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ngozi Serikali haijazui kuuza ngozi ghafi nje. Hadi sasa ngozi zinauzwa kwa wingi katika nchi za Ghana na Nigeria na vibali vinaendelea kutolewa kwa wale wanaohitaji. Hadi kufikia mwezi Machi, 2019 kilo za ngozi ghafi 3,636,700 za ng’ombe zenye thamani ya shilingi trilioni 4.6 na kilo 274,000 za mbuzi zenye thamani ya shilingi 320 zilisafirishwa nchi ya nje. Kwa hiyo, siyo kweli kwamba tumezuia kusafirisha ngozi nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu miradi ya maendeleo kutumia vifaa vinavyopatikana nchini. Hili limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge, mambo mengine yanahusu mikataba, tunaendelea kuzungumza na Wizara ya Fedha na wadau wengine kuhakikisha kwamba sehemu kubwa ya matumizi kwenye miradi mikubwa ya maendeleo kwa mfano ujenzi wa barabara, reli na madaraja wanatumia vifaa ambavyo vinazalishwa ndani ya nchi ikiwemo bidhaa za chuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani nitakuwa nimegusa maeneo maeneo muhimu sana ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge na mengine yote ambayo yamezungumzwa tumeyachukua na tutayatolewa taarifa wakati utakapofika.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, ahsante sana.

WABUNGE FULANI: Toa hoja.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)