Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii. Naomba nianze kwa pongezi kwa Waziri, Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie machache sana katika Wizara hii, mambo mawili au matatu. La kwanza, nianze na alilolisema Mheshimiwa Dkt. Chegeni jana kwamba mimi Naibu Waziri wa Fedha mwaka jana nililidanganya Bunge kwa kutoa takwimu ambazo siyo sahihi kwa biashara zinazofungwa na zinazofunguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliambia Bunge lako Tukufu, sina sababu ya kudanganya kwa sababu niko field, mimi nafahamu kinachotokea, biashara zinazofungwa tunazijua, biashara zinazofunguliwa tunazijua. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Dkt. Chegeni kwamba kwa mwaka huu kuanzia Julai, 2018 hadi Aprili, 2019 biashara zilizofungwa nchi nzima ni 16,252 lakini biashara zilizofunguliwa ambazo ni mpya ni 147,818. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo ukweli, huo ndiyo uhalisia. Kama biashara zingekuwa zimefungwa bila kufunguliwa nyingine tungewezaje kukusanya kodi inayokusanya Mamlaka ya Mapato Tanzania?

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, hili lazima tulielewe, kwa sababu sehemu ambako biashara inafungwa tu hiyo wachumi tunaita it is a dormant economy, Tanzania is not a dormant economy na hatujawahi kufika huko, tunaendelea kusisitiza. Kwa hili, nimpongeze sana Dkt. John Pombe Magufuli, Watanzania halali wamemuelewa na wanaendelea kufanya biashara halali. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania wanaendelea kufanya biashara…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mtulie, kwani wakati mnaongea si tulikuwepo.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane na kuna wengine mkianza kutajwa majina huwa mnajisikia vibaya sana. Kwa hiyo, tusifanye fujo ambazo ukitajwa hapa mbele unaanza kujisikia vibaya, tumuache Mheshimiwa anachangia kama wewe ulivyopata fursa ya kuchangia, muache atoe ufafanuzi amalize.

Mheshimiwa Naibu Waziri, zungumza na mimi tu wala hawa wasikupe taabu.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niendelee kusema uchumi wetu uko imara na makini, tunaendelea kutenda kwa ajili ya Watanzania. Hili ni jambo la msingi sana na ndiyo maana hatujawahi kushuka kwenye makusanyo tangu ameingia Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli madarakani chini ya trilioni moja kukusanya kila mwezi. Huu ndiyo uhalisia na ndiyo tunayoyajua ambao tuko field.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la pili ambalo napenda kuchangia, nalo ni hili ambalo limesemwa hapa kwamba kwa nini waagizaji wa mizigo kutoka nje wanaombwa original documents. Sheria inasema nini? Kifungu cha 234 cha Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki kinamtaka mteja kuleta nyaraka halisi za uingizaji wa mizigo, sheria inatuelekeza hivyo. Kwa mujibu wa sheria hii mzigo wa kuthibitisha muamala wowote ule upo kwa muingizaji wa muamala huo hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria inatuambia a burden of proof of any import transaction rests on the shoulder of the importer or the authorities of the exporting country. Tunachokifanya kwa sasa, nimesema Watanzania halali wanafanya biashara halali wamemuelewa Dkt. John Pombe Magufuli na hii lazima tuelewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni mwaka jana tu kipindi kama hiki ombwe kama hili la mafuta lilitokea, tujiulize swali la kwanza, kwa nini huwa wana-target kipindi kama hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani? Lazima tuelewe scenario nzima kabla hatujasimama kuwatetea, kwa nini wana-target kipindi kama hiki? Sheria inasema hivyo, hiki ni chakula, unapotuletea tuoneshe umeitoa nchi gani kwa original document, hiki ni chakula. Sisi tuliopewa mamlaka haya ya kusimamia tunataka Watanzania walindwe kwa kila hali na lazima tulisimamie jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niyasemee mafuta haya. Mafuta yaliyopo bandarini yalikuja metric tons 14,400. Katika mafuta haya yapo ambayo hawajafanya declaration mpaka leo, yako bandarini lakini hawajafanya declaration, kipi kinafichwa kwenye hilo? Lazima tujiulize ndugu zangu Watanzania. Waheshimiwa Wabunge tuelewe dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni njema sana. Kwa hiyo, lazima kabla hatujabebwa tu tuelewe nini kilichopo kwenye mzigo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hawaja-declare mpaka leo, yapo mengine wame-declare ndiyo hayo ambayo hawajaleta original documents na sisi hatutotoa bila kuleta original documents…

MBUNGE FULANI: Sawasawa.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi kutoa mpaka tuweze kutekeleza sheria. Original documents ziletwe tujiridhishe ni crude oil au siyo crude oil kwa sababu crude oil inalipiwa kodi kutoka kwenye country of origin. Kama imelipiwa kule watuletee tujue thamani yake ili tuweze kuwapelekea Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mafuta hayohayo yapo mengine yameondolewa. Mwanzo walisema yanatumika ndani ya nchi lakini wameyaondoa wameyapeleka nchi jirani, lipi linafichwa hapo?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kijaji, muda umekwisha lakini inavyoonekana una hoja nyingi sana za kujibu hapo, maliza hoja zako ndani ya dakika moja ninayokuongezea.

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nimalizie kwa kusema tunaendelea kusisitiza Watanzania waendelee kumuelewa Dkt. John Pombe Magufuli, biashara halali ziendelee kufanyika na tunaendelea kulinda afya ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)