Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya Mkoa wa Kilimanjaro vilivyobinafsishwa bado havijaanza kufanya kazi kama ambavyo Serikali imekuwa ikiagiza. Mji wa Moshi katika miaka ya 70 hadi mwanzoni mwa miaka ya 90 ulikuwa una viwanda vikubwa zaidi ya 12 ikiwa ni pamoja na viwanda vya watu binafsi. Viwanda hivyo ni pamoja na viwanda vya magunia, ngozi, mbao, nguo, pipi, vibiriti, karatasi na kadhalika. Hali ilivyo sasa ni tofauti kabisa kwa vile viwanda vyote hivyo vimekufa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali ipitie upya kanzidata ya viwanda katika Mkoa wa Kilimanjaro ili ione ni namna gani inaweza kufufua viwanda vilivyokufa katika Mji wa Moshi na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla. Kufufuliwa kwa viwanda hivyo kutachochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Kilimanjaro na Taifa kwa ujumla. Pia, kutaongeza ajira na mambo mengine kama hayo. Aidha, ni vizuri Wizara ikawatafuta wawekezaji binafsi ambao viwanda vyao vimekufa ili kuona ni jinsi gani wanaweza kushirikishana namna bora ya kuvifufua.

Mheshimiwa Naibu Spika, uimarishaji wa soko la ndani. Dhamira ya Serikali ya kujenga Tanzania ya Viwanda itafikiwa iwapo tutaimarisha soko la ndani. Soko la ndani ndilo litakalohakikisha mauzo ya bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani. Wajibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara ni kutoa msukumo na motisha kwa wafanyabiashara wa Tanzania ili biashara zao ziimarike ambapo wataweza kuajiri wafanyakazi wengi sana, hivyo kuongeza kipato cha Watanzania na kwa maana hiyo kuongeza nguvu ya soko (purchasing power).

Mheshimiwa Naibu Spika, soko la ndani ndilo linaweza kufanya wawekezaji wa kiwango cha kati na cha chini kuimarika na baadaye kuwa wawekezaji wakubwa watakaouza nje. Soko la ndani ndilo linaweza kukuza kidogokidogo viwango vya bidhaa zetu zinazozalishwa na kuziingiza kwenye ushindani wa soko la nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kodi ya Huduma (Service Levy). Sheria ya Kodi hii ya Huduma lazima ibadilishwe ili iweze kulipika. Utaratibu wa sasa ambapo kodi hii inalipwa kwa kigezo cha mauzo ghafi siyo utaratibu wenye tija kwa wafanyabiashara na kwa Taifa kwa ujumla. Utaratibu huu unaweza ukafilisi wafanyabiashara kama ukitekelezwa kama ulivyo. Hivyo, ushauri wangu ni kwamba kodi hii itozwe katika faida na kama haifai kutozwa katika faida itozwe kwa viwango kulingana na madaraja ya biashara.