Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo hoja hii ya viwanda, biashara na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Waziri kwa namna alivyowasilisha ripoti yake na alivyoisoma kwa nguvu mpya na ari mpya. Nakuombea ndugu yangu, mdogo wangu, pambana bwana tunataka viwanda sisi. Tunataka 2025 iwe nchi ya viwanda, nchi ya kipato cha kati, kazi ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme Serikali ya Awamu ya Tano ilijipangia mambo kadhaa ya kufanya ili kuipeleka nchi hii kwenye viwanda. Jambo la kwanza ilisema ingeweza kuanzisha viwanda vya msingi ambavyo vinachochea viwanda vingine. Kwa mfano, viwanda vya chuma; Liganga na Mchuchuma, tumesema sana hiyo na tunaishukuru Serikali kwa kuliona kwamba hilo jambo lilikuwa la msingi. Viwanda vya magadi soda kwa mfano kule Engaruka tuliweka kama jambo la msingi. Viwanda hivi vikianzishwa, vingeweza kulipeleka Taifa mahali pazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali ya Awamu ya Tano iliendeleza shughuli ya gesi na mafuta. Jambo lingine ambalo Serikali ilijiwekea ni ujenzi wa miundombinu. Tunaipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa jambo hilo, ujenzi wa reli, barabara, bandari, viwanja vya ndege, ndege zenyewe, umeme, nishati na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine Serikali hii ililizungumza sana tangu iingie madarakani ni kilimo. Ilitengeneza mkakati unaoitwa Cotton to Clothes (C2C), lakini ilikuwa na mkakati wa ASDP I na mikakati ya Sekta ya Ngozi. Kwa maandishi, Serikali imekaa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni mazingira ya kufanya biashara iwe rahisi. Pamoja na hayo, Bunge liliendelea kuishauri Serikali, tangu mwaka 2015 nakumbuka mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Viwanda na Biashara, tumeishauri Serikali kama Bunge iyafanye haya mambo ambayo yameandikwa kwenye Mpango wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema, kwenye mazingira ya kufanyia biashara, tulitaja mambo kadhaa ambayo tunahitaji Serikali iyarekebishe ili biashara iwe sawa sawa. Kwa mfano, utitiri wa kodi, wingi wa mamlaka zinazosimamia, pia mtazamo kuhusu wafanyabiashara na wawekezaji, kuwatazama kama marafiki badala ya kuwatazama kama maadui, wezi na wanyang’anyi. Naipongeza tena Serikali, ilikubali na ilisikiliza ushauri. Natoa vithibitisho vya ushauri kusikilizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, iliandaliwa blue print, ukiisoma hiyo, mambo yote haya ya uwekezaji pamoja na biashara yamesemwa vizuri sana, tena sana. Changamoto iliyopo Mheshimiwa Waziri, ni utekelezaji. Leo ni mwaka wa pili tuna blue print ipo kwenye shelf na wale buibui wameanza kuitanda sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mkakati wa ASDP I nadhani umemaliza sijui miaka mingapi? Mitatu, minne hivi haujatekelezwa. Tunaanza kutengeneza mkakati mwingine, ASDP II. Changamoto kubwa tuliyonayo Mheshimiwa Waziri ni kutekeleza haya mambo ambayo tuliyakubali, tumeyaandika vizuri, mnataka wenzetu majirani wachukue hii mikakati wakatekeleze, sisi tunaangalia tu! Tukiweza kutekeleza hayo, Mheshimiwa Waziri, yaani hatuko mbali kabisa na mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme kwamba mchango wangu mkubwa ni kuishauri Serikali sasa, naomba nitoe ushauri ufuatao: La kwanza, Wizara hizi zifanye kazi kwa ushirikiano. Niliwahi kusema zifanye kazi kwa ushirikiano; kilimo, Wizara ya Viwanda na Biashara, Nishati na Ujenzi lazima mkutane. Narudia tena, nilisema mwaka 2016 mtengeneze mkakati wa pamoja wa kutekeleza jambo hili. Wizara ya Fedha nimeisahau, ndiyo inayotoa fedha. Msipofanya hivyo, tutakuwa na mikakati na mipango lakini hatuitekelezi kwa sababu kila mtu anakwenda vya kwake. Ni muhimu sana tukawa pamoja katika mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa hizi documents ambazo nimezitaja hapa; blue print, ASDP, C2C na mikakati mingine ipo mizuri mingi kabisa, imejibu hoja zote na matatizo yote ambayo tunayasema humu Bungeni, hebu itekelezeni. Nakumbuka kuna mkakati wa kuzalisha mbegu za mafuta nyingi hapa ili tusiwe na matatizo ya mafuta, tekelezeni. Tukiendelea kila mwaka tunakuja tunatoa story hapa, kwa kweli hatutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mwingine, tuangalie baadhi ya sheria. Kuna sheria nyingine tumezitengeneza nzuri kweli, lakini mle ndani kuna maneno ambayo yamefukuza wawekezaji. Naomba kila sekta angalieni sheria zenu, mbadilishe kidogo. Ngoja nitoe mfano, mnisamehe. Sheria za sovereignty tulizotengeneza ni nzuri kweli zinalinda rasilimali zetu, lakini kuna vipengele mle ndani akisoma tu mwekezaji anabwaga manyanga anaondoka. Naomba sana Waziri wa Sheria na Katiba, Waziri wa Madini na Waziri wa Nishati hebu tazameni, kuna vipengele vichache siwezi kuvitaja, ukivibadilisha tu kidogo unahamasisha uwekezaji wa ndani na wa nje, utakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa nne, tuongeze bidii katika kujenga miundombinu. Hapa tunafanya vizuri sana, tunajenga reli, barabara, viwanja vya ndege, tunatengeneza umeme, lakini tuongeze bidii. Kuna sehemu hatujaenda vizuri. Kwa mfano, tunajenga reli kwenda Mwanza, lakini financing inatupa shida kidogo na Wabunge kadhaa walisema, tuna-finance kidogo kidogo, tutatumia miaka 20 kufika Mwanza. Hebu tutafute mkakati mzuri zaidi tuharakishe jambo hili. Kwa kweli ni jambo zuri, lakini tulifanye kwa speed ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa tano, tujenge viwanda mama. Liganga na Mchuchuma jamani tungetumia chuma sasa hivi kujenga reli yetu, chuma cha ndani, lakini tumechelewa. Hebu tukazane kidogo hapo. Mheshimiwa Waziri wasiliana na Nishati na Madini hii rasilimali iweze kuchimbwa. Hizo changamoto zilizopo hapo tuzirekebishe, tutaenda vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa mwisho, tulifanya vizuri sana katika kuweka maeneo ya uwekezaji; EPZ pamoja na SEZ. Tume-identify maeneo mengi lakini kuya-develop imekuwa taabu. Moja ya changamoto ni Bandari ya Bagamoyo; ni kitu kizuri kweli na kina maelezo mazuri kweli, lakini tumeenda mpaka sasa hivi kuna kizungumkuti wanasema Waswahili. Kwa kweli Mheshimiwa Waziri hatuelewi kama tunaenda au hatuendi. Maeneo mengi kama Kurasini mpaka leo, yapo mengi tu, mpaka kule Igunga kuna maeneo ya uwekezaji ambayo hayajaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema, tunafanya vizuri sana katika kuandika projects na mikakati lakini hatufanyi vizuri katika kutekeleza. Tunaandika sheria, tunashindwa kuzitekeleza. Sheria ya PPP kwa mfano, tuliitunga mwaka 2018 lakini ina vikwaruzo vingi mle ndani. Nami nikiwa Mjumbe wa Kamati ya Bajeti, nilisema, nilimwambia Waziri wa Fedha kama anakumbuka, kwamba hii tulivyoipitisha kama ilivyo hivi hatutapata mwekezaji hata mmoja kwenye PPP kwa miaka 20 ijayo. Lazima tuirudishe hapa tuibadilishe, kuna mambo ambayo hayakusemwa vizuri humu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Dalaly Kafumu.

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana kwa kunisikiliza. Mungu awabariki. (Makofi)