Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Naungana na Waheshimiwa wenzangu wote waliochangia katika Wizara hii. Nataka tu kufahamu, kuna mazao matano ya kimkakati, lakini kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri hapa nimetezama sijaona sehemu yoyote ile. Sasa ndiyo utakuta unapata mkanganyiko wa kujua anayesimamia hiyo biashara ni nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuelewa mwenye dhamana ya biashara na mikokotoo yote tunayohangaika nayo humu ndani, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana hii anaweza akawa na mchango mkubwa sana kuisaidia Serikali na kujua tumekusanya kiasi gani na changamoto zilizoko kwa wafanyabiashara ni kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunalo zao la Pamba, Kahawa, Tumbaku, Korosho na Mbaazi, lakini Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ambaye ndiye kabeba jukumu la kibiashara na Waziri huyu anatakiwa afanye mazungumzo na wafanyabiashara kujua changamoto zao zote na kuzipeleka Serikalini ili zitatuliwe lakini tumekuwa na mkanganyiko mkubwa sana. Waziri wa Kilimo ndiye mwenye sera, lakini yule ni mzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa na malalamiko mengi, kila Bunge likikutana lazima wazungumze, lakini Waziri mwenye dhamana haonekani katika sekta nzima ya biashara. Kwa hiyo, ningeshauri Mheshimiwa Waziri aje atueleze, majukumu yake ni yapi? Labda ni Waziri wa Viwanda tu pekee bila biashara. Naamini kama ni Waziri wa Viwanda na Biashara anaweza akawa na mchango mkubwa na akasaidia nchi hii. Naye tu kwa uelewa wangu, Waziri wa Fedha anaweza akawa ndiyo Mhasibu wake, lakini yeye ndio anaweza akajua makadirio tunayoyakadiria haya tunaweza tukakusanya kodi zaidi kuliko mtu yeyote mwingine humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Waziri mwenye dhamana hajui biashara zinakwendaje hapa nchini, lakini kuna Wajumbe wenzangu wamezungumza vitu vingi. Kuna mambo yamezungumzwa ya OSHA, sijui WFP na kadhalika, yote haya Mheshimiwa Waziri yanakulenga wewe ili uwasaidie wafanyabiashara. Ili Serikali hii isiwe na malalamiko na wafanyabiashara wewe ni jukumu lako kuhakikisha unasimamia sera nzima ya biashara. Ukifanya hivyo, utakuwa umepunguza dhana nzima ya ulalamikaji katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi kuna Wajumbe wamegusia suala la General Tyre, lakini tunacho pale Kilombero mavuno ya Matairi. Watu wa Kenya (Firestone) wanachukua malighafi yetu, inakwenda Kenya halafu ndiyo tunaletewa matairi.

Mheshimiwa Waziri, ukiangalia tu ni magari mangapi yanayopita kwenye nchi yetu kuzunguka wanapohitaji matairi? Kwa hiyo, ni suala ambalo ukiliangalia linaweza likatusaidia na tukapiga hatua kubwa sana katika dhana nzima ya uwajibishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la TBS, wawekezaji wamekuwa wakifanya analysis za kwanza ana kiwanda chake labda cha Oil Mill linachukua muda mrefu zaidi ya miezi miwili, lakini katika dhana nzima ya uwekezaji inaleta changamoto katika maeneo husika. Ningeshauri Serikali iboreshe mfumo mzima wa TBS ili kusudi wafanyabiashara hao wanaowekeza katika nchi yetu, wanapowapeleka sample yao basi ichukue angalau hata siku 30 au 20 sio kwa mieizi miwili na hiyo miezi miwili inachukua muda mrefu. Wameboresha wakaweka TFDA sehemu ya kwanza na sehemu ya pili. Sasa nashauri watengeneze mfumo mzima wa kusaidia dhana nzima na waweke kikanda, isiwe tu Dar es Salaam peke yake wakiweka kila kanda itatusaidia kuhakikisha kwamba watu wanapiga hatua katika dhana nzima ya uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitazungumzia suala la masoko, nimeligusia. Serikali yetu kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi tulisema tutaboresha ushirika na tunavyo vyama vya ushirika na tunavyo vinu vinachombaua pamba katika maeneo mbalimbali. Nimeona kwenye ukurasa waa kitabu cha Mheshimiwa Waziri amezungumzia suala zima la kwamba amerudishiwa viwanda vilivyokuwa 156 na amebaki na vingapi na vingapi. Katika hali nzima ya kuhakikisha ananufaisha na kuboresha ushirika, Mheshimiwa Waziri anaweza akaniambia ni maeneo yapi ambayo ushirika umeimarika na unachakata mwenyewe bila kupitia fedha za wafanyabiashara. Naomba nalo hilo atusaidie katika majumuisho yake kwamba ameboresha hiki na amepiga hatua kufikia mahali hapa itatusaidia nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala zima lingine, wenzangu wamezungumza mchana hapa, kuna kiwanda cha BORA tena ni cha kizalendo cha Watanzania, Mheshimiwa Waziri atusaidie malalamiko haya watu wanayoyazungumza kulingana na uzalishaji uliopo hapa nchini, taasisi zote za kiserikali ziangalie namna gani ya kwenda kuunga jitihada hizi za wawekezaji walio kwenye maeneo yetu ili wasaidie kuongeza uchumi wa nchi na pato la Taifa, kuliko hivi sasa watu wanazalisha mali inakuwa nyingi, matokeo yake ngozi inakosa mahali pa kununuliwa ni kwa sababu mali haitoki. Mheshimiwa Waziri akitusaidi hilo atakuwa ameweka mfumo mzuri wa kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anao wataalam waliobobea kwenye eneo lake hilo la kibiashara, naamini akiyachukua haya mawazo na akitengeneza mfumo wa kufanya mazungumzo kama Waheshimiwa Mawaziri wengine wanavyofanya, trip ijayo hatutampigia kelele, lakini sasa hivi ni kukutana tu mitaani anakwenda huku na huku, lakini walenga hajakutana nao na wana mawazo mazuri, naamini akishirikiana nao mtu wa kilimo abakize kuzalisha, suala la biashara asimamie Mheshimiwa Waziri itatusaidia na ndio maana miaka ya nyuma Kilimo, Chakula, Ushirika na Masoko ilikuwa ni Wizara moja lakini wakaona watofautishe, sasa leo tunavutana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika hili akitufanyie utaratibu huu, biashara zitasonga mbele na shughuli zitakwenda mbele zaidi. Hilo litakuwa sehemu kubwa sana ya kuongeza uchumi katika maeneo yetu na nchi nzima kwa ujumla. Haya akiyachukua Mheshimiwa Waziri itatusaidia sana lakini tutakapokuwa tunaendelea kupiga kelele na Mheshimiwa Waziri wa Biashara anakuwa ni sehemu, leo ameomba bilioni 100, yeye ni sehemu kubwa ya kuwezesha shughuli hizi zisitembee mara moja, kwa sababu wafanyabiashara wote anao mwenyewe, sasa sielewi ni kigugumizi gani ambacho anakipata, anashindwa kukutana nao na kupata mawazo mazuri ya kuhakikisha nchi inapiga hatua na uwekezaji unakwenda kwa kasi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri asipofanya hivyo itakuwa kila siku watu tunalalamika lakini mwisho wa siku hakuna jibu lolote lile na mwisho wa siku kama walivyosema wenzangu mchana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)