Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Mwanne Ismail Mchemba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kwa siku hii ya leo nami niweze kuchangia Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nashukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uwezo wa kuamka leo salama na kunipa nafasi kama hii ya pekee kuweza kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na pongezi. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta Sera ya Viwanda nchini na kuisimamia yeye mwenyewe kikamilifu. Nampongeza sana kwa sababu siyo hilo tu ameyafanya Mheshimiwa Rais wetu, lakini ana mengi ameyafanya katika nchi hii kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015/2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Makamu wa Rais, anafanya kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, wamejipanga. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na timu yake, wanafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia. Nimeanza kwanza kwa pongezi, sasa nakwenda kwenye jukumu kubwa ambalo ninalo moyoni mwangu. Mheshimiwa Waziri naomba Mwenyekiti alipokee hili na alisikilize kwa makini. Nataka nizungumzie habari ya kiwanda cha Tabora cha Nyuzi (TABOTEX). Kiwanda hiki kimeanza muda mrefu, tangu mwaka 1978 kama sikosei au 1975. Baada ya kubinafsishwa, kiwanda hicho kimesuasua na mpaka leo hakifanyi kazi. Malighafi yote imeondolewa. Nilishamwomba hapa ndani Mheshimiwa Naibu Waziri twende mimi na yeye akaangalie hali halisi ilivyo kwa sababu hatuwezi kukubali kutafuta wawekezaji ambao ni wababaishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda hiki kilikuwa kinasaidia sana ajira kwa watu wa Mkoa wa Tabora, lakini mpaka sasa hakuna ajira, vijana wanahangaika, lakini mwekezaji hakuna chochote alichokifanya. Nilitegemea basi, kwamba angalau Mheshimiwa Waziri angeweza kuiweka mle TABOTEX. Nimeangalia ukurasa wa nane hamna kitu, nimeangalia ukurasa wa 20 hamna kitu, labda mimi sijui kusoma. Kama sijui kusoma leo Mheshimiwa Waziri ataniambia kwamba ameiweka wapi? Kiwanda cha Nyuzi ambacho ni tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hiki historia yake ni kwamba kulikuwa na Mbunge anaitwa Marehemu Mzee Misigalo. Miaka ya nyuma ili kuweza kufanikisha alimwomba Baba wa Taifa kwamba kiwanda hiki kiwepo Tabora baada ya kuonekana kwamba hakuna kiwanda chochote ambacho kinaweza kikawa kinatengeneza nyuzi kwa Kanda ile ambayo wanalima pamba. Kwa hiyo, akaitoa shilingi, nami leo naitoa kwako. Aliitoa Shilingi, Baba wa Taifa akampa hicho kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri mwaka uliofuata anaomba kura, wakampa tena akatawala vipindi viwili. Alivyotawala vipindi viwili, hakuna tena aliyevunja ile historia kwa sababu ya kile kiwanda. Sasa nami kwako Mheshimiwa Waziri shilingi hii nitaondoka nayo, naenda nayo Tabora mpaka wewe uje ujieleze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ujenzi wa Kiwanda cha Tumbaku. Ujenzi wa Kiwanda cha Tumbaku tulitegemea pia tungekiona humu kwenye kitabu hiki, hamna. Tumbaku inalimwa Tabora asilimia 60 na tuliomba kwamba kuwepo na kiwanda cha kutengeneza, kusindika Tumbaku Mkoa wa Tabora lakini hakimo. Mheshimiwa Waziri ana ajenda gani? Ana ajenda gani wakati Tumbaku tunailima sisi wenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda hiki gharama zake ni kubwa ambazo wanatoa tumbaku kupeleka Morogoro. Wakipeleka Morogoro, gharama yote inakwenda kwa mkulima na wakulima wa tumbaku wanalima katika mazingira magumu, hawana afya nzuri kutokana na usumbufu wa zao la tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu aliweka mazingira mazuri ya suala zima la bei ya tumbaku, lakini nilitegemea sasa leo Waziri mhusika mwenye dhamana angeweza pia akaliongelea hili suala la kiwanda cha tumbaku kwa ajili ya Mkoa wa Tabora na nchi nzima, kwa sababu Kanda ile yote Kigoma, wapi wanalima tumbaku, lakini hakuna kitu chochote alichoweza kuandika. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili kwa upana, ni jinsi gani atakavyojipanga aliweke hili jambo la kiwanda cha nyuzi aweke pia na suala zima la kiwanda cha tumbaku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la SIDO. SIDO ni mkombozi mkubwa sana, watu wanadharau; SIDO imeweza kulea wanawake, imewatoa wanawake na vijana kwenye ujasiriamali sasa wamekuwa wawekezaji wakubwa, lakini hakuna fedha yoyote ambayo inakwenda kwenye mikopo. Kwa hiyo, bado nina wasiwasi, tunawasaidiaje vijana na wanawake kwa kuidharau SIDO? SIDO ilitakiwa ipewe fedha nyingi ili waweze kukopesha wanawake na vijana na walemavu, watu wote ambao ni wajasiriamali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia vifungashio. SIDO imewaelimisha wananchi, wajasiriamali wote wamepita mafunzo ya SIDO na ndiyo maana wanajua maana ya vifungashio. Sasa hivi wanafnyakai nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Maonyesho ya Saba Saba. Wajasiriamali wanateuliwa wachache sana tena kwa kupitia vikao ambavyo havihusiki na SIDO. SIDO wanaleta tu mwelekeo, wanatoa waraka, lakini nani anayeweza kudhibiti wajasiriamali ili waende kwenye Masoko ya Maonyesho ya Kimataifa na Maonyesho ya Saba Saba? Ni lazima SIDO iingize mkono wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili SIDO iweze kufanya kazi nzuri, mimi siafiki kutokuwapa pesa SIDO. SIDO hawapati fedha zozote. Kwa hiyo, hata mimi ningeweza kuishauri Serikali, kama kuna fedha nyingine zozote ambazo wanaona ni rahisi kuwafikia walengwa, wananchi ambao ni wa chini, lazima ipitie SIDO. Tangu imeanza SIDO haina mgogoro wowote wa kazi kubwa ambayo inafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, ukiisoma kwenye taarifa ya SIDO, urejeshaji wa mikopo ni tofauti na asilimia 10 ambayo inatolewa na Manispaa au Halmashauri. Wao wameweza kukusanya marejesho asilimia 91.5. Hata ukitaka kusoma lile jedwali lake liko ukurasa namba 16. Ni watu ambao wanaweza wakasaidia nchi hii kuondokana na figisu figisu ya mikopo midogo midogo kwa sababu mikopo yao ni ya riba nafuu. Kwa hiyo, nilikuwa nataka nizingatie hayo ambayo ni ya muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho mimi sikutaka kuchangia mengi. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, sitaki kuichafua Serikali yangu, lakini utakapokuja hapa unipe majibu ya mambo mawili; la kwanza Kiwanda cha Nyuzi, kwa nini wanaondoa vifaa wanapeleka Manonga? Vingi wamepeleka Manonga. Kwa hiyo, nataka majibu hayo, kwa sababu sasa hivi asilimia 100 ya wakulima wa pamba wanatoka Igunga. Kwa hiyo, bila hilo, sitaki kukosana, nimesharudia mara tatu, mara nne; nitakosana na wewe kwa ajili ya Kiwanda cha TABOTEX, nitakosana na wewe bila kupata majibu. Sitaki kujua kama unatoka Tabora au unatoka wapi! Mimi sitambui. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mimi najua wewe ni Waziri, kwa hiyo, siitambui. Yeye ni Waziri lakini sitaki kujua huko nyuma kama anatoka Tabora. Mimi na wewe humu ndani ama kesho patakuwa hapatoshi. Nipate majibu mawili ya Kiwanda cha Nyuzi na Kiwanda cha Tumbaku, lini kitaanza mchakato? Hayo ndiyo ya kwangu ambayo nataka wewe Mheshimiwa Waziri sasa, nakuomba, nam-address yeye kwa sababu haijalishi kama anatoka wapi? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja asilimia mia kwa mia. Ahsante sana. (Makofi)