Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe J. Magufuli, Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Mhandisi Isack Kamwelwe, Naibu Waziri Mheshimiwa Kwandikwa, Naibu Waziri Mheshimiwa Mhandisi Nditiye, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara husika. Mheshimiwa Waziri ameacha historia Pwani kwenye maji, nina hakika na barabara atazitendea haki, hongera sana.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa usimamizi mzuri na kufuata ilani kwani miradi mingi imeweza kuvuka na kupiga hatua na kuleta sura nyingine nchini. Hii ni kwa sababu Mheshimiwa Rais Magufuli ameamua kuleta maendeleo nchini. Kwani tumeona ununuzi wa ndege, ukarabati vya viwanja vya ndege na hata Wilaya yetu ya Mafia imepata fedha kwa ajili ya matengenezo ya Mafia.

Mheshimiwa Spika, sambamba na ukarabati wa Bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga pia tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa Bandari ya Nyamisati na ukarabati, tunaomba ukarabati Gati la Kilindoni, Mafia uende sambamba kwani ndiyo itakuwa mwanzo/mwisho wa safari zote za wananchi wa Mafia na kuinua uchumi na kuendeleza Kisiwa cha Mafia na hata idadi ya watalii itaongezeka. Naomba kupata maelezo lini kazi hiyo itaanza.

Mheshimiwa Spika, jiografia ya Mkoa wa Pwani iko katika hali ya kutegemeana na mikoa mingine nchini na pia kiungo cha safari zote za mikoani. Napenda kujua ujenzi wa barabara ambazo ni kiungo kikuu kwa wilaya nyingine na hata mikoa utaanza lini. Mfano, barabara ya Kisarawe – Maneromango – Vikumburu - Mloka, hii barabara ni muhimu sana na hasa kwa sasa ambapo kuna ujenzi wa mradi wa umeme Rufiji.

Mheshimiwa Spika, mkoa una visiwa vidogo vidogo vingi katika Wilaya ya Kibiti, Mafia, Mkuranga na Rufiji, tunaomba bajeti zinazokuja wafikirie kupeleka boti za uhakika ili wananchi wa maeneo hayo nao wawe na uhakika wa safari na kupata huduma muhimu.

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa la mawasiliano kwenye Mkoa wa Pwani kwenye baadhi ya maeneo, kwingine mawasiliano ya simu na maeneo mengine mawasiliano ya redia hasa Radio TBC. Mfano, Wilaya ya Kisarawe ambako kuna minara yote/baadhi ya TV/Radio lakini bado kuna maeneo hawapati/kusikia chombo hicho cha Taifa, ikiwemo Wilaya ya Mafia na baadhi ya maeneo na hata mawasiliano ya simu. Hili suala linaeleweka kwenye ofisi ya Mheshimiwa Waziri, hivyo napenda kupata majibu ya ufumbuzi wa matatizo hayo.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kupata taarifa rasmi ya lini Kisiwa cha Mafia kitapata chombo/meli/boti/feri ya uhakika kwa ajili ya wananchi wa Mafia.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.