Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia kidogo Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nikushukuru na kumpongeza Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake. Kipekee niwapongeze Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu ya Ijumaa na leo.

Mheshimiwa Spika, itoshe mimi leo kuchangia kwamba safari yetu ni kwenda kwenye uchumi wa kati, ulio jumuishi na ili kufika hapo lazima tujenge uchumi wa viwanda, siyo viwanda. Kuweza kujenga uchumi wa viwanda ni lazima tuwe na miundombinu wezeshi na saidizi. Kwa hiyo, Wizara hii ndiyo inayojenga miundombinu wezeshi na saidizi. Twaweza tusione leo hayo tunayoyataka lakini tunapokwenda kwenye uchumi wa kati nina imani hayo tutayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo nalotaka kuzungumzia ni bandari. Watu wa bandari, sitazungumzia suala la Bagamoyo ila Mheshimiwa Ally Saleh, nikukosoe kidogo au nikupe taarifa, Bagamoyo Special Economic Zone itazalisha viwanda 1,000 na watu laki tano watapata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wa bandari, kuna kiwanda cha Hengia cha Tanga kinachotaka kuzalisha tani milioni saba, nawaomba tukubaliane na wazo la kiwanda kile cha kupata access. Alipokuja Dangote akazalisha tani milioni tatu nchi nzima bei ilishuka, akiingia wa tani milioni saba mambo yatakuwa mazuri. Kama walivyosema wenzangu, twende kasi kwenye maamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, watu wa TPA niwaeleze kuhusu kitu kinaitwa Port Community. Tunafanya vizuri sana ndani ya bandari lakini wale wanaotusaidia, kwa mfano TRA, TANROADS, hawafanyi kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, nimewaeleza kwa maandishi kwamba ya nini kuweka mzani wa TANROADS Kurasini wakati unaweza kuweka mzani huohuo bandarini na wote wako chini ya Wizara moja? Ndiyo maana kunakuwa na foleni. Niwaombe watu wa bandari tuongeze kasi, tunafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nirudie tena; sisi Nacala na Beira si washindani wetu katika bandari, Durban si mshindani, tunatengeneza washindani sisi wenyewe. Yaani ni kama mtu unatengeneza mke mwenza, unashindwa kumhudumia uliyenaye mpaka analazimika kwenda nje kutafuta ushindani. Wanaokwenda Beira na Durban wamelazimika kwenda kule. Tukisawazisha ease of doing business, Nchi za Maziwa Makuu wanapenda kuja hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa na rafiki yangu mmoja kwenye Serikali ya Kongo iliyomaliza muda, aliniambia wanaweza kutupa robo ya shehena waliyonayo, Bandari ya Dar es Salaam haitapokea mzigo wa Tanzania au nchi nyingine. Kama walivyozungumza tuitumie njia ya Kigoma tuweze kuvuta huu mzigo wa Mashariki ili uweze kuja lakini na Kigoma iweze kuchangamka ili hawa ndugu zangu waache mambo ya kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie ATCL, niwashauri watu wa Wizara hii tafadhali Uwanja wa Ndege wa Bukoba uangaliwe. Bukoba tunahitaji uwanja mkubwa, hatuhitaji ndege nyingi, sisi shida yetu ni kupakia bidhaa za kwenda kwenye masoko makubwa. Mkoa wa Kagera unamiliki sehemu kubwa ya Ziwa Victoria lakini viwanda vya samaki haviwezi kwenda pale kwa sababu ndege za mizigo haziwezi kuja pale Bukoba.

Mheshimiwa Spika, lakini niwapongeze ATCL hapo mlipofikia, mnachopaswa kufikia sasa ni kutengeneza soko kubwa, kuchangamsha soko na mimi nawaona Watanzania wanakwenda kule. Mnakumbuka kuanzia tarehe 19 Desemba mpaka Januari Bukoba mlikuwa mnapiga trip mbili kwa siku na ilikuwa inajaa. Sasa ninachowashauri ATCL, nimekuwa nikiwaambia muende kwenye utamaduni, mtu akipanda ndege unamkaribisha kwamba karibu kahawa, unampa kahawa, unampa senene ili watu wapande ndege waweze kuzoea ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi hatufanyi mambo ya profit and loss, hii siyo biashara ya maandazi, wazoeshe Watanzania ndege hata kwa kuwapa free ride, wapande ndege na wazipende ili tutengeneze soko kubwa. Haya mambo ya kuongeza destination watu wakishapanda ndege wakazizoea watapanda ndege.

Mheshimiwa Spika, kama alivyozungumza Mheshimiwa Kepteni Abbas, sitaki kuchangia, competitive advantage ya Air Tanzania ni soko la ndani.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa muda huo, mengine ntaleta kwa maandishi. (Makofi)