Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba nianze na barabara ya Kidatu – Ifakara; barabara hii ilizinduliwa tarehe 5/5/2018, tulizindua nikiwemo na mimi na Mheshimiwa Waziri na Wabunge wote wa Morogoro. Rais alizindua ujenzi na barabara ikaanza kujengwa, lakini baada ya muda mfupi mkandarasi akaondoa vitu site; mpaka sasa hivi ninavyoongea ni mwaka mmoja sasa barabara hii haijawekwa hata kilometa moja ya lami.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitoa mwongozo kwa Wizara ya Fedha na Wizara ya Ujenzi watatue tatizo la mgogoro wa kikodi wa VAT lakini mpaka leo hii Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Ujenzi wanaogopana kama mtu na baba mkwe wake. Mheshimiwa Rais ameshawaambia wakae watatue huu mgogoro lakini wanaogopana; kama wameoleana si wamwambie Mheshimiwa Rais awahamishe Wizara waje Mawaziri wengine watatue huo mgogoro kama wao wanashindwa? (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, la pili, ni barabara ya Ifakara – Mahenge. Barabara hii ina urefu wa kilometa 74. Sasa hivi Ulanga tuna deposit kubwa ya graphite na kuna kampuni kubwa tatu tayari zimeshaanza uwekezaji na kwa mwaka tutatoa tani zaidi ya laki tano.

Mheshimiwa Spika, kwa hali ya barabara ile hii biashara haiwezi ikafanyika. Endapo barabara hii itakuwa tayari Serikali ina uwezo wa kuingiza zaidi ya shilingi bilioni 400 kwa mwaka. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati ana- wind up atuambie mkakati uliofikiwa kwa ajili ya barabara hii.

Mheshimiwa Spika, barabara nyingine ni ya Liwale – Ulanga. Ukiacha ahadi ya Mheshimiwa Rais, ni mkakati wa Serikali kuunganisha barabara za mikoa na ni muhimu sana katika uchumi wa Wanaulanga. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atuambie amefikia wapi kuhusiana na ujenzi wa barabara hii umefikia.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni la viwanja vya ndege. Naipongeza Serikali kwa umaliziaji wa Terminal III lakini wasisahau na viwanja vingine kwa vifaa, maana tumeshuhudia ndege zikisukumwa na watu. Bahati mbaya ikatokea wafanyakazi wa airport wakawa na miili kama mimi watasukumaje hizo ndege? (Kicheko)

Suala lingine ni uhalifu wa mitandaoni, hii naongelea kuhusu TCRA. Uhalifu wa mitandaoni umegawanyika katika sehemu tatu: Udhalilishaji, wizi na upotoshaji.

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia udhalilishaji mkubwa na TCRA wamekuwa wakikaa kimya. Wameanzia kwa viongozi wa siasa sasa hivi wamekuwa wakitengeneza picha za ngoni za viongozi wa dini. Hali imekuwa mbaya na TCRA wamekaa kimya.

Mheshimiwa Sika, suala lingine ni la wizi wa mitandao. Wizi huu makampuni ya simu yanahusika. Tumeona meseji za tafadhali tuma pesa kwenye namba hii, waganga feki, unaweza ukatumiwa meseji ukaambiwa mtoto wako ameanguka shuleni, hizo meseji ni za uongo. Meseji nyingi zinatoka Kampuni ya Vodacom na baada ya uchunguzi wangu nikakuta wafanyakazi wanahusika. Kwa hiyo, makampuni ya simu walipeni vizuri wafanyakazi wenu na wekeni mfumo ambao mtaangalia hawa wafanyakazi wasiwe wanashiriki katika wizi wa mitandaoni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na taarifa nyingi za upotoshaji. Taarifa hizi nyingine zinatolewa na Wabunge wakiwa wanapotosha taarifa za Serikali katika mitandao na wanafahamika lakini TCRA wanashindwa kuwachukulia hatua. Naomba suala hili lishughulikiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la ATCL na nitaongelea kwenye nauli. Nauli za ATCL zimekuwa kubwa tofauti na matarajio ya Watanzania. Kwa mfano, kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam nauli hadi Sh.600,000. Sasa mimi nakuwa nimepanda nalipa nauli au nimekodisha ndege? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, napenda kuongelea usafiri wa Noah. Enzi zenu kipindi hicho kulikuwa na mabasi tu, sasa hivi kuna usafiri wa Noah ambao umesaidia kwa kiasi kikubwa. Sasa hivi kuna Noah zaidi ya 16,000 zinasafirisha Watanzania zaidi ya milioni 115 kwa mwaka. Hizo Noah 16,000 zimeajiri makondakta na madereva 32,000. Ukichukulia kila kondakta mmoja na dereva mmoja akiwa anahudumia watu wanne, kuna wananchi zaidi ya 128,000 wanahudumiwa na watu hawa. Bado wanalipa kodi, TRA, SUMATRA, bima na wanatumia mafuta lakini kumekuwa na sintofahamu ya hawa madereva wa Noah na huu usafiri wa Noah Serikali imekuwa ikiwasumbua hasa SUMATRA…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mlinga.

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, siungi mkono mpaka niambiwe suala la VAT linaishaje.