Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Hussein Nassor Amar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyang'hwale

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ameniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu. Pia napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu Mawaziri na watendaji wote kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya katika Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja ambalo natakiwa nianze kulisema, leo ni mwaka wa nane niko Bungeni, kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, aliahidi ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kahama – Bukwimba – Nyijundu – Busisi Sengerema na Rais wa Awamu ya Tano naye pia ameahidi. Hata hivyo, cha ajabu kwenye kitabu hiki nimejaribua kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho sijaona upembuzi yakinifu wa barabara hiyo. Kwa hiyo naomba nijue, ahadi za Marais hawa zimepuuzwa ama zitatekelezwa na kama zitatekelezwa ni lini? Kwa sababu barabara hii ina umuhimu sana, inaunganisha mikoa mitatu; inaunganisha Mikoa ya Shinyanga, Geita na Mwanza. Barabara hii ikifunguliwa uchumi wa Nyang’hwale utapanda. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aingize angalau basi niweze kuona kwamba upembuzi yakinifu umeanza tuwe na matumaini, leo miaka nane nazungumzia barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, nimejaribu kuangalia kwenye kitabu chake, ameweza kunitengea karibu milioni 900 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe kutoka Nyankumbu hadi Nyang’hwale, lakini kutoka Nyang’olongo mpaka Nyang’hwale. Barabara hii ina kiwango cha changarawe lakini imepangiwa kujengwa kwa kiwango cha lami kutoka Geita- Nyankumbu kuja Nyang’hwale. Cha ajabu, miaka nane imepita, lakini tumejengewa kilometa tano tu za lami na imesimama. Miaka miwili iliyopita hatukuweza kutengewa, je, 2019/2020 kwa nini tena haikutengewa ama imeondolewa kwenye utekelezaji? Naomba Mheshimiwa Waziri aiangalie barabara hiyo kwa sababu ilishaahidiwa kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Mheshimiwa Waziri, kuna barabara ambayo ameiweka, barabara hii kwa kweli ikifunguliwa itakuwa imefungua maendeleo makubwa sana katika Wilaya ya Nyang’hwale. Ameweza kututengea pesa kufungua barabara ya wilaya kwa wilaya kutoka Mbogwe kuja Nyang’hwale; kutoka Bwelwa – Bukoli – Nyijundu mpaka Bumanda na Makao Makuu Kharumwa, Makao Makuu ya Nyang’hwale, barabara hiyo ikifunguka naamini mambo yatakuwa mazuri. Nimpongeze sana kwa hilo, naomba tu utekelezaji ufanyike kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri anayehusika na masuala ya mawasiliano, kuna kata kama tano kwangu zina matatizo ya mawasiliano. Kata hizo zikiwa ni Shabaka, Nyamtukuza, Nundu, Nyabulanda na Nyugwa, mawasiliano sio mazuri, Mheshimiwa Waziri alitupa fomu tukajaza maeneo ambayo hayana mawasiliano mazuri, nami nilijaza ile fomu mwaka jana, lakini cha ajabu mpaka leo fomu hii haijafanyiwa kazi na wananchi wangu wanapata tatizo kubwa sana la mawasiliano. Namwomba Mheshimiwa Waziri atekeleze ahadi zake, aliahidi kwamba atashughulikia maeneo yote ambayo yana matatizo ya simu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kueleza hayo machache, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)