Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na barabara zangu za Jimboni lakini na zile zinazounganisha mkoa na mkoa. Barabara inayounganisha mkoa mmoja na mwingine hili ni suala la kisera ambapo sera inataka zitengenezwe kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa masikitiko makubwa sana na Mheshimiwa Silinde amezungumza lakini pia yuko Mbunge hapa wa Kwela amezungumza na nimekuwa nikizungumza mara kwa mara, kuna barabara hii ya kutoka pale Mloo - Kamsamba, Mloo kwa maana Jimbo la Mbozi, Mkoa wa Songwe kwenda Kamsamba, Wilaya ya Momba lakini pia kwenda Kwela, Mkoa wa Rukwa lakini pia kwenda sehemu moja hivi inaitwa Kasansa hadi Kibaoni kwa maana ya Mkoa wa Katavi. Barabara hii inaunganisha karibu mikoa mitatu ya Songwe, Rukwa na Katavi na ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti iliyopita walitenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu naona safari hii tena wametenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu, sasa huu upembuzi yakinifu hatujui mwisho ni lini kwa sababu miaka yote sasa wanatenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Barabara hii kwa sababu ya umuhimu wake, tulitegemea kwamba Serikali ingekuwa sasa imeshaanza kujenga hii barabara kwa kiwango cha lami kwa sababu tayari Daraja la Kamsamba lilishaisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili ambalo nalizungumza mazao yote yanayoingizia pato kubwa Taifa kama kahawa, mpunga, kwa maana ya mchele lakini pia ujumlishe mazao kama ufuta, alizeti na mazao mengine mengi sana ya misitu na kadhalika yanatoka kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami maana yake inaenda kuongeza kipato cha Mikoa ya Songwe, Rukwa, Katavi lakini pia pato la Taifa kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ili Mheshimiwa Waziri kuacha alama Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, nadhani ni kuhakikisha kwamba barabara hii inatengenezwa kwa kiwango cha lami. Hakuna namna nyingine unaweza ukafanya kuwaaminisha watu wa Kanda za Nyanda za Juu Kusini kwamba kuna kazi imefanyika kama hii barabara itabaki kama ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Pinda alijitahidi sana barabara kutoka pale Tunduma - Sumbawanga, nadhani anaweza akajivunia. Sasa Mheshimiwa Waziri wewe unatoka Katavi sijui utawaambia nini watu wa Katavi, Rukwa na Songwe kwa sababu barabara hii ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuna barabara inayotoka Jimbo la Songwe kule kwa Mheshimiwa Mulugo kuna Kata inaitwa Magamba kuja Magamba ya Mbozi, kwa sababu kuna Kata mbili za Magamba, Mbozi kuna Magamba lakini pia Songwe kuna Magamba, watu kutoka Jimbo la Mheshimiwa Mulugo wanalazimika kupita Mbalizi kwa maana Mkoa mwingine wa Mbeya wakati Makao Makuu yako Mbozi pale ndani ya mkoa mmoja hakuna barabara inayounganisha kati ya wilaya ya Mbozi na wilaya ya Songwe. Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo kwa kweli Waziri atakapokuja hapa atuambie wanafanya nini kushughulikia changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nizungumze kuhusu suala la Wakala wa Ndege za Serikali kuhamishiwa Ofisi ya Rais Ikulu, Fungu 20. Naomba hapa Serikali iweze kuwa makini kusikiliza vizuri sana. Wakala huyu wa Ndege za Serikali kuhamishiwa Vote 20, ukiangalia majukumu ya Wakala wa Ndege za Serikali, moja ni kusimamia mikataba ya ukodishwaji wa ndege kwa kampuni ya ndege ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbili, kufanya matengenezo na ununuzi wa vipuli vya ndege za Serikali. Leo Ikulu inaenda kusimamia ununuzi wa vipuli vya ndege halafu haitakaguliwa imenunua vipuli wapi na kwa gharama gani hamna atakayekagua kwa sababu Vote 20 haikaguliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kufanya matengenezo kwa maana kufanya ukarabati wa karakana ya ndege za Serikali. Yaani leo watafanya ukarabati wa karakana za Serikali maana yake hawatakaguliwa…

T A A R I F A

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, anaposema Fungu 20 linakaguliwa, Wabunge mara kadhaa hapa tumetaka watuambie, kwa mfano Vote 20 inahusu pia suala la bajeti yao ya Usalama wa Taifa, mbona Bungeni hapa hatujawahi kuambiwa kwamba Usalama wa Taifa wanakaguliwa kwa sababu nayo iko kwenye Vote 20. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Fungu 20 maana yake hata CAG mwenyewe hatakagua na hatutajua nini kinafanyika. Bunge lako Tukufu halitajua fedha za walipa kodi, za wavuja jasho, wauza michicha, wauza nyanya zinazoenda pale kwenye ndege hamna atakayejua kwamba ni shilingi ngapi zinaenda pale na zinafanya kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Waziri atuambie kwa sababu wanasema jukumu lingine la kitengo hicho ni kulipia gharama za bima za ndege, hakuna atakayejua kwa sababu ni kwenye Vote 20 ambayo haikaguliwi. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Serikali katika vitu ambavyo wamebugi, kwa mfano, tunasema Serikali hii inafanya kazi na inajali kweli kodi za Watanzania hii Wakala wa Ndege za Serikali wasiipeleke kwenye Vote 20 ili Wabunge tuwe na uwezo wa kuhoji, Watanzania wajue fedha zao zinafanya nini na mwisho wa siku tujue kwamba tunasonga vipi mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni kuhusu suala la TBA. TBA wanapewa miradi mingi sana.

T A A R I F A

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niseme tu kwamba suala hili la Fungu 20 tunapozungumza kwamba halikaguliwi kwa mfano nisaidie kitu kimoja umeshawahi kusikia matumizi kwa mfano fedha zinazonda TIC kwa maana usalama wa taifa zikajadiliwa hapa Bungeni.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kaboyoka ngoja tulinyoshe hili tunakupa fursa. Mheshimiwa Heche naomba unyamaze nazungumza. Mheshimiwa Heche naomba ukae nazungumza, nazungumza naomba unyamaze Mheshimiwa Heche, toka nje Mheshimiwa Heche naomba utoke nje Mheshimiwa Haonga ongea halafu nitampa yeye fursa ongea ulichokuwa unataka kuongea. Mheshimiwa Heche naomba utoke nje ukiwa umeshapewa hiyo taarifa ya kutoka nje usiende kuzungumza ukiwa humu ndani funga mlango nyuma yako ondoka. Mheshimiwa Haonga. (Makofi)

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kanuni zetu, kwa kanuni zetu tulizonazo Bungeni hapa mtu anayesema anapotosha Mbunge ndio anayomamlaka kwa maana ya nafasi yakuweza kuweza ukutuambia kwamba ushaidi ni huu kwa maana haikaguliwi. Ninajua kwamba hapa Bungeni haijawahi kuna kuba baadhi ya vifungu havijawahi kuletwa hapa Bungeni kwa mfano kama suala la taarifa hizi za TIC kwa maana ya usalama wa Taifa hazijawahi kujadiliwa Bungeni hapa.

NAIBU SPIKA: Basi Mheshimiwa Kaboyoka.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kama mwenyekiti wa PAC niweke taarifa vizuri, kwamba Fungu namba 20 linakaguliwa lakini hatujawahi kulikagua halijawahi kaguliwa.(Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimwa Wabunge tusikilizane Mheshimiwa Haonga ulikuwa unapewa taarifa na Mhehimiwa Kaboyoka unaipokea taarifa hiyo.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipokee taarifa ya Mheshimiwa Kaboyoka hapa na ninaomba niendelee baada ya kupokea.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Jenista naomba ukae kidogo, naomba ukae kidogo nakupa fursa. Mheshimiwa Haonga umesema unaipokea taarifa ya Mheshimiwa Kaboyoka?

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema kwamba baada ya Mheshimwa Kaboyoka kunipa taarifa nimeipokea na taarifa ya Waziri pia nimeipokea lakini kwamba haijawahi kuletwa hapa kwa maana ya haijakaguliwa muda mrefu.

NAIBU SPIKA: Sawa naomba ukae tusikie kanuni inayovunjwa. Mheshimiwa Jenista Mhagama.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu nikwenda kanuni ya 64(1) ambayo inaenda sambamba na kanuni hiyo ndogo ya (1)(a) inayokwenda sambamba na kanuni ya 63. Unapotaka kuzungumza Bungeni lazima uwe unasema ukweli na unakuwa na uhakika na kile unachokisema. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ametoa maelezo fasaha hapa, Vote 20 inakaguliwa, na Vote 20 sio Vote ya Usalama wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mbunge ameendelea kusisitiza kwamba wakala wa ndege za Serikali kuwekwa kwenye vote 20 tunakwenda kuficha jambo kwa sababu vote hiyo haikaguliwi. Jambo ambalo si kweli kwa maelekezo ambayo tumepewa na Waziri wa Fedha. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PAC anasema vote inakaguliwa halafu akasema wao hawajawahi kukagua lakini wao hawana mamlaka ya ukaguzi wa vote hizo kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Mheshimiwa Haonga Mbunge anayechangia hoja hii afute kauli yake, na kama hataki kufuta kauli yake tunaomba alithibitishie Bunge hili kama kweli ana ushahidi. Suala ukaguzi ni kazi ya CAG sio suala la Mbunge kuthibitisha kwama vote imekaguliwa au haijakaguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika naomba kutoa hoja. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge naomba tusikilizane, Mheshimiwa Jenista Mhagama amesimama kwa mujibu wa Kanuni 64 ambayo inazungumza kuhusu mambo yasiyoruhusiwa Bungeni. Mheshimiwa Jenista ametoa hoja yake akieleza kwamba mchango wa Mheshimiwa Haonga kuhusu ukaguzi wa vote namba 20 namna alivyozungumza kwenye hoja yake ametoa taarifa ambayo haina ukweli. Lakini pia amezungumza kuhusu matakwa ya kanuni ya 63 inayozungumza kuhusu kutokusema uwongo Bungeni.

Waheshimiwa Wabunge nadhani wote tumeona mjadala namna ulivyoenda kwanza Mheshimiwa Haonga alikuwa anasema wakala kuhamishiwa pale hataweza kukaguliwa na kwa hivyo Bunge halitaweza kupata taarifa yoyote kuhusu jambo hilo.

Mheshimiwa Waziri wa Fedha akasimama kumpa taarifa kwamba vote namba 20 inakaguliwa na yeye akaulizwa kama anaipokea na yote yaliyofutwa baada ya hapo nadhani sote tunafahamu alijibu vipi mwanzoni na baadaye akapewa tena taarifa na Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali. Baada ya mwenyekiti wa Kamati Hesabu za Serikali kumpa taarifa Mheshimiwa Haonga kwamba vote 20 inakaguliwa isipokuwa Bunge halijawahi kukagua ndio maneno Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali.

Mheshimiwa haonga akasema anaipokea alipoulizwa kwa mujibu wa kanuni zetu alisema anapokea taarifa hiyo ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa kamati ya PAC. Lakini wakati huo huo akiwa anatoa maelezo yake kabla sijampa fursa ya kuzungumza Mheshimiwa Jenista akasema pia anaipokea taarifa ya Mheshimiwa Waziri kuhusu kukaguliwa kwa vote 20.

Mheshimiwa Jenista amesimama kuomba ufafanuzi kwa sababu anaona kanuni ya 64 lakini pia kanuni ya 63 imetumika katika matumizi ya maneno ya kutokukaguliwa kwa vote 20 na kwa hiyo, Mheshimiwa Jenista anataka tutumie kanuni ya 64 na 63 tukimtaka Mheshimiwa Mbunge atumie uhuru wake uliyowekwa katika kanuni hizi mbili kufuta kauli yake kuhusu kutokukaguliwa kwa vote namba 20 na katika maelezo yake amesema kwamba kuhusu kukagua hiyo ni kazi ya Mkaguzi wetu wa Hesabu za Serikali na si Bunge. Kwa sababu Mbunge huletewa taarifa na CAG. Kwa muktadha huo na kwa kuwa Mheshimiwa Haonga alishaipokea taarifa ya Mheshimiwa Naghenjwa Kaboyoka kwamba Vote 20 hata kama mwanzo alisema hakaguliwa sasa kwa kuwa alipokea taarifa amekiri inakaguliwa na pia akakubali maelezo ya Mheshimiwa Waziri kuhusu kukaguliwa. Sasa kuhusu mambo yanayofuata baada ya hapa yale yanayoletwa huku Bungeni PAC na LAAC inafanya kazi baada CAG kuwaletea kinachokuwa kimeshakaguliwa. Kwa hiyo jambo lolote ambalo CAG hakulileta maana yake yeye ameona halipaswi kuletwa, kwa muktadha huo maneno aliyoyazungumza Mheshimiwa Haonga kuhusu kukaguliwa ama kutokukaguliwa kwa Vote namba 20 ameyanyosha hapa mwishoni kwamba anaikubali taarifa ya Mheshimiwa Waziri lakini pia Mheshimiwa Mwenyekiti wa kamati ya PAC. (Makofi)

Wakati huo huo nitamtaka sasa kwa mujibu wa kanuni zetu kuhusu hayo maelezo mengine ya taarifa kuweza kufika ama kutokufika yale sasa sio ya Bunge hili yale anatakiwa ayafute kwa sababu hayakuwa sehemu ya taarifa aliyokuwa akipewa. Nadhani utakuwa umeelewa vizuri Mheshimiwa Haonga. La kwanza la kuhusu ukaguzi ulilimaliza kwa maelezo yako ya mwisho, lakini lile la taarifa kufika hapa au kutokufika hilo ndio unatakiwa kuliondoa ili umalizie mchango wako.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kwanza nishukuru sana kwa kuweka vizuri nione kwamba umesimamia kanuni vizuri na umeenda vizuri. Niseme kwamba cha msingi ni kwamba hapa nilijaribu kuliweka sawasawa kwamba hii inakaguliwa lakini tangu nimekuwa Mbunge kwa miaka hii mingapi hii taarifa haijaletwa hapa Bungeni kuhusu Vote 20 nadhani haijaletwa hapa kukaguliwa. Lakini hili lingine ulivyoelekeza naona maagizo yako yachukuliwe kama yalivyo kwamba maagizo yako tumeshaweka sawasawa na ninaomba nichangie kitu kingine kwenye hilo tumeshamaliza na ninaomba unisaide muda wangu.

NAIBU SPIKA: Ngoja sasa nitakupa muda wako umalizie. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge kwa ajili ya kuliweka sawasawa hili la Mheshimiwa haonga hoja ya kwanza alishaikubali kwamba Vote namba 20 inakaguliwa ile sehemu ya pili kuhusu kuleta taarifa hapa au kutokuletwa taarifa huletwa na CAG, kama CAG hakuleta basi hakuona umuhimu ama hatakiwi kuleta hilo. Na yeye kwa ajili ya kupunguza matumizi ya muda amesema maelezo haya ndio ambayo yanachukuliwa. Kwa hiyo, sehemu hiyo ya mchango wake inakuwa imeondolewa Mheshimiwa Haonga malizia muda wako.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naomba niendelee kama ambavyo umetaka niendelee. Kuhusu suala la TBA, mheshimiwa TBA wana miradi mingi ambayo wanapewa, wanamiradi mingi karibu miradi 90 wanapewa. Lakini cha ajabu TBA wanaopewa mradi mingi ya ujenzi, miradi mingi haikamiliki kwa wakati. Na kama miradi haikamili kwa wakati tafsiri yake ni kwamba fedha za walipa kodi maana yake mwisho wa siku inakuwa zinatumika nyingi sana maana yake unapochelewesha mradi gharama za mradi zinaongezeka, gharama ya mradi ikiongezeka anayeingia hasara ni watanzania wanaolipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba niseme tu kwamba hata kule kwetu Mkoa wa Songwe tuna ofisi ya Mkoa wa Songwe zimeanza kujengwa muda mrefu sana ni kama miaka minne sasa hizo ofisi zinajengwa na TBA hazijawahi kukamilika na ni muda mrefu mno.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie ana mkakati gani wa kuwapunguzia TBA miradi. Kusudi hii miradi wapewa wengine na kuwe na ufanisi wa miradi wanapomrundikia mtu mmoja miradi hii miradi, miradi haiwezi kufanyika kwa ufanisi. Na wakati huohuo fedha za watanzani zitakuwa zinapotea kwa hiyo niombe Mheshimiwa Waziri utakapkuja hapa utuambie mna mikakati wa kuwapunguzia TBA miradi ili sasa na wengine waweze kupata miradi na mwisho wa siku iweze kufanyika kwa ufanisi na tuweze kupata ile value for money.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)