Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. Kwanza kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Manaibu Waziri wote wawili kwa ushirikiano ambao wanatupa wananchi wa Madaba kwenye masuala yote ya barabara na mawasiliano na nitoe salam za pekee kutoka kwa wananchi wa Ifinga ambao tangu nchi hii ipate uhuru hawakuwa na mawasiliano kabisa, walikuwa wanasafiri zaidi ya kilomita 30 kwenda kupiga simu, lakini sasa tatizo hilo limekwisha, tunawashukuru sana. Pia watu wa Madaba wanamkumbuka sana Mheshimiwa Waziri, alianza utumishi Madaba na leo ameshirikiria Wizara muhimu sana katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiifuatilia historia ya Madaba utagundua kwa nini ina matatizo makubwa ya barabara, Madaba ilikuwa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea miaka minne iliyopita. Katika kipindi hicho, barabara ambayo ilikuwa inahudumiwa na Serikali kwa kupitia fedha za halmashauri ilikuwa kilometa 48 tu na sasa Madaba ni Halmashauri ya Wilaya na ni Jimbo na kilometa zinazohitaji kuhudumiwa kwa maana ya mtandao wa barabara Madaba umefikia kilomita 642. Mpaka sasa bajeti tunayopata Madaba kwa kupitia TARURA ni ya kilometa 48 tu, haizidi shilingi milioni 400.16. Madhara yake barabara nyingi za Madaba ni mbovu hazifai na hazipitiki katika kipindi cha masika na hata kiangazi bado kuna makorongo mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo barabara za kimkakati ambazo naamini Mheshimiwa Waziri tumeanza kuzungumza kwenye vikao vyetu ambavyo siyo rasmi na yeye, lakini hapa naongea mbele ya Bunge hili Tukufu kumwomba akubali kupokea baadhi ya barabara zitoke TARURA ziende TANROADS. Moja katika barabara hizi ni hii barabara ya kutoka Wino kwenda Matumbi – Ifinga. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro na barabara hii ndiyo barabara ambayo itachangia sana kwenye kuipata Tanzania ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza hekta za ardhi zimewekeza kule kwa ajili ya kilimo cha miti na muda si mrefu kama Mheshimiwa Waziri atatusaidia, hawa watani zangu wa Iringa tutawapita kiuchumi. Uchumi wetu utafafana na uchumi unaouona Mafinga leo kwa kutokana na miti, lakini kinachotuangusha ni hii barabara. Hii ni barabara ya kimkakati, ni barabara yenye uchumi mkubwa sana. Barabara hii ina urefu wa kilomita 57, pia inaunganisha na mbuga ya Selou ambako tayari kuna vitalu ambavyo wawekezaji wamewekeza kwenye kuwinda na kwenye utalii. Kwa hiyo ina mchango mkubwa sana kwenye uchumi na hatuwezi wana Madaba kushiriki kwenye uchumi wa viwanda kama barabara hii Mheshimiwa Waziri hatakubali kuipokea. Namwomba sana kwa niaba ya wananchi wa Ifinga akubali kuichukua barabara hii iende TANROADS ili ijengwe kwenye viwango tunavyovitaka na matokeo yake ni uchumi ambao utatokana na kazi kumbwa inayofanyika katika maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ukiangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri aghalabu utakuta mahali pameandikwa Madaba, najua kwa sababu labda Madaba barabara zake ni fupi na ni barabara ambazo wanadhani TARURA itazikamilisha, lakini kiuhalisia sivyo hivyo, TARURA hawana fedha za kuweza kumaliza zile barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara nyingine ya kimkakati inayounganisha Madaba na Njombe kwa kupitia Kijiji cha Maweso na kama Mheshimiwa Waziri alifanya kazi Madaba wakati ule, ili uje Dar es Salaam ilikuwa unapita Maweso unaenda Mikongo unatokea Kifanya unakwenda Njombe, ile barabara ya zamani, barabara kubwa ya kutoka Dar es Salaam kwenda Madaba, kwa sasa unaweza kwenda mwisho Maweso, baada ya pale huwezi kuendelea na ile barabara. Namwomba Mheshimiwa Waziri barabara hii pia aichukuwe kwa maana ya Mfuko wa TANROADS aihudumie ili kukuza uchumi wa wananchi wa Madaba na wananchi wa Maweso, lakini wananchi wa Njombe kwa sababu hilo ndilo eneo kubwa ambalo lina ardhi kubwa ya uzalishaji, lakini pia lina matukio ya kihistoria. Barabara hii ina kumbukumbu za kudumu za mashujaa wa vita ya Uganda…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mhagama muda wako umekwisha.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)