Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Joyce Bitta Sokombi

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nami nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, hasa kwa manufaa ya wananchi wa Mkoa wa Mara na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti kwa miaka mitatu zimetengwa shilingi trilioni 13. Naitaka Serikali itueleze, tunapata ajira kiasi gani na return yake ni nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, fedha nyingi za maendeleo kila siku tunaambiwa zinafanya upembuzi yakinifu. Maana toka nimekuwa Mbunge, sasa hivi ni mwaka wa nne, kila ukiuliza swali unaambiwa ni upembuzi yakinifu, sasa sijui huo upembuzi yakinifu utaisha lini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo? Sasa hivi Wilaya ya Rorya, TARURA haijapata fedha za maendeleo ya barabara takribani miaka miwili mfululizo na ukiangalia Wizara hii imetengewa pesa nyingi sana. Naomba tafadhali Mheshimiwa Waziri asikilize kilio cha wananchi wa Mkoa wa Mara apeleke fedha zikamalize ujenzi wa barabara ambazo zinatakiwa kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Musoma – Busekela ina kilometa 42, lakini fedha zilizopelekwa ni za kilometa tano tu, kilometa 37 bado hazijajengwa. Sasa sijui Mheshimiwa Waziri atatuambia ni lini zile kilometa 37 zitaenda kumalizwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Wanyele – Kitario imekatika na kila siku nimekuwa nikiizungumzia hapa kwenye maswali; na majibu yamekuwa ni yale yale ya marudio. Ile barabara ya Wanyele – Kitario ni barabara ambayo inahitaji kuwekwa daraja na ilishasababisha maafa. Kuna takribani watoto 20 walishafariki na nilishasema katika hili Bunge lako tukufu, lakini mpaka sasa hakuna hatua yoyote ambayo imeshachukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tafadhali, hizi mvua zinazonyesha, wasije tena watoto wengine wakaendelea kufa tukaendelea kupata maafa katika Mkoa wetu wa Mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi viporo mingi tu. Kwa mfano, Bunda – Kisoria, Makutano – Sanzate, Mugumu – Tabora B, zinahitajika fedha kuweza kukamilisha miradi hii viporo. Mpaka leo hii hakuna pesa yoyote ambayo imeshapelekwa na barabara zile zimekaa tu, hatuelewi hatma ya hizi barabara. Tunaomba Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa kwenda kumalizia miradi hii viporo iweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilivile kuna round about Tarime. Ile round about ya Tarime Mjini mara nyingi imekuwa ikisababisha madhara. Imesababisha ajali nyingi sana. Naishauri tu Serikali ihakikishe eneo lile inaweka angalau zile taa za kuongoza wale watu wa magari, hata wale waenda kwa miguu. Kwa mfano, kama ile barabara ya pale Mwenge kwenda Mjini, Mwenge kwenda Mikocheni, Mwenge kwenda Kawe, Mwenge Kwenda Ubungo, ni taa ambazo zinaongoza vizuri sana. Naishauri sana Serikali ione umuhimu kwa sababu ile keep left pale ni ndogo na eneo lile ni dogo sana. Naomba na kuishauri Serikali ituwekee taa eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda Uwanja wa Ndege wa Musoma, ule uwanja ni mdogo. Sasa hivi wanataka kuutanua ule uwanja uwe mkubwa, lakini kuna wale watu ambao wamezunguka lile eneo la Uwanja wa Musoma na wale watu walishawekewa X toka mwaka na miezi mitano mmoja sasa hivi. Wale watu walishafanyiwa tathmini, lakini watu waliofanya tathmini walifanya bila kuwashirikisha wananchi husika. Mpaka sasa wale wananchi hawajui hatma yao kwa sababu wanatembea tu hati, hawawezi kwenda benki kukopesheka wala kufanya kitu chochote cha maendeleo yoyote katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na kuishauri Serikali wakarudie kufanya tathmini kwa kushirikiana na wananchi wa eneo husika ili mtu anapofanyiwa tathmini ajue nyumba yake inafanywa tathmini kwa kiasi gani? Kwa sababu mnapofanya tathmini tu na kuondoka bila kumwambia mhusika kwamba tathmini tumefanya nyumba yako ina thamani ya kiasi fulani kwa kweli inasikitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda upande wa TBA. Kwa kweli TBA hawafanyiwi ushindani na makampuni binafsi, ndiyo maana kazi zao zimekuwa ni substandard. Matokeo mengi tunaona kazi nyingi za Serikali zinafanywa na TBA na kazi zao nyingi zimekuwa za kiwango cha chini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naongea hivyo kwa sababu gani? Kuna zile nyumba za mradi wa Bunju. Ule mradi, yaani kwa ushauri wangu mdogo tu, sana sana wangeanza kuweka social services kwa kuanza kuweka zahanati, wakaweka shule, wakaweka barabara nzuri ili mtu anapokwenda kule kwa sababu zile nyumba ziko pembezoni sana, angalau hata ziwe ni nyumba za kufikika kwa urahisi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JOYCE B. SOKOMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, zile nyumba malengo ilikuwa ni kwa ajili ya wafanyakazi na wafanyakazi wengi wamehamishiwa Dodoma, kwa maana hiyo zile nyumba zinakaa tu hazina wapangaji. (Makofi)