Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata muda kuchangia Wizara hii ya Ujenzi. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai mpaka siku ya leo. Napenda kabisa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Engineer Kamwelwe, Naibu Mawaziri Mheshimiwa Engineer Nditiye na Mheshimiwa Kwandikwa, Katibu Mkuu TANROADS Engineer Mfugale na watendaji wote wa Wizara hii. Vilevile bila kumsahau Meneja wangu wa TANROADS Mkoa wa Rukwa na wasaidizi wake wanafanya kazi vizuri sana, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanza napenda kusema kwamba Mkoa wa Rukwa ni mkoa wenye mvua nyingi sana, kwa maana hiyo barabara zake za changarawe ni mara nyingi zinaharibika sana lakini fedha tunazopangiwa ni kidogo sana, hazikidhi mahitaji ya uharibifu wa barabara zile. Nishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja lile la Mto Momba kama wenzangu walivyoshukuru, sasa hivi tumeona urahisi hata malori yanayopita sasa hivi yaliyokuwa yanazunguka kule Kibaoni yamebeba nguzo, sasa hivi yanakatisha yanapita yanaingilia Songwe yanakuja kutokea Kamsamba na kuleta nguzo; tunashukuru sana kwa kweli Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, tunaishukuru Serikali kwa kilio cha wananchi wa Mji Mdogo wa Laela walikuwa wana kilio cha kivuko lakini kupitia TAMISEMI tumepata milioni 163 kujenga kivuko kile, tunashukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie barabara ya Kiliamatundu, Muze, Ntendo na Kasansa. Waziri aliyepo sasa hivi ni Waziri ambaye huwezi ukamwambia chochote juu ya barabara hii. Anaifahamu vizuri umuhimu wake na jinsi inavyounganisha mikoa hii mitatu; tunashukuru mmejenga daraja lakini tunaomba sasa muweke nguvu kuiwekea lami. Na mmetenga kiasi cha milioni 180 kwa ajili ya usanifu lakini naona fedha hii sidhani kama inaweza ikatosha kwa urefu wa ile barabara, ile barabara ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Eng. Kamwelwe wewe ni mwenyeji wa maeneo yale, tunaomba kabisa katika awamu yako hii weka nguvu ile barabara iweze kutengewa fedha ili kupata lami; kama tutakosa katika kipindi chako sidhani kama tunaweza tukapata tena. Ni kipindi muhimu kabisa na muafaka kwa sababu unajua umuhimu wa barabara ile kiuchumi, tunakuomba sana utilie maanani katika barabara hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kipande cha barabara cha Ntendo – Muze. Barabara hii ndiyo inayotumika katika kuingiza malighafi inayotoka ukanda wa Ziwa Rukwa, ni barabara ambayo ipo busy sana muda wote, malori ni muda wote. Nashukuru Serikali mwaka jana mlitupangia pesa tukaweza kutengeneza kilometa 2 za lami lakini nashangaa badala ya kuongeza, mwaka huu mmepunguza badala ya kutuongeza kilometa 5 mmetuwekea kilometa 0.8 badala ya kuongeza. Sasa nashindwa kuelewa ni kwa namna gani tena mnarudi nyuma badala ya kwenda mbele, tunaomba sana Mheshimiwa Engineer Kamwelwe utuongezee pesa hii barabara iweze kutanuliwa na kumalizika kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha hilo, barabara hiyo kilometa 8 za Mlima ambao wakati mwingine barabara ni finyu, kama lori lilikwama lingine haliwezi likapita. Nakumbuka mwaka juzi Waziri Mkuu alikwama, tukaanza sisi wote kutafuta namna gani Waziri Mkuu atapita lakini solution ilipatikana, alikuja Katibu Mkuu ambaye sasa hivi hayupo hapo akashauri tuipanue lakini nashangaa katika bajeti hii sijaona. Mheshimiwa Engineer Kamwelwe naomba hilo na lenyewe uweze kuliangalia, eneo la Mwilimani linahitaji kabisa kupanuliwa na kuwekwa zege sehemu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ni ya Kalambanzite – Ilemba kilometa 24; kilometa 12 zipo mlimani. Hii barabara tunashukuru TANROADS ilishaichukua, tunaomba na yenyewe basi iweze kujengwa kwa kiwango kizuri cha changarawe na mlima wote uwekwe zege lakini nimeona kwenye bajeti mmetenga pesa kidogo kama milioni 30, milioni 30 utatengeneza kitu gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, ningeomba sana Mheshimiwa Waziri uweze kuliona hili, tena ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano aliahidi kuiwekea lami, sasa nashangaa sasa hivi suala badala ya lami hata changarawe, hata kuweka zege mlima wa kilometa 12 tunashindwa kuweka fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nyingine ni barabara ya Miangalua – Chombe…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imegonga.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)