Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Hon. Capt. Abbas Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Fuoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema. Pia nichukue fursa hii kumpongeza Waziri Eng. Kamwelwe na Naibu wake wawili kwa kazi nzuri sana wanayoifanya ya kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwa asubuhi ya leo nitajikita katika taasisi mbalimbali ambazo ziko chini ya Wizara hii. Nitaanza na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji ambacho kwa siku za karibuni tulipata fursa kwenda kukitembelea na Kamati. Tumeona hatua ya maendeleo iliyofikiwa na chuo hicho lakini tatizo kubwa ni kwamba kitendea kazi kikuu hakijapatikana ambacho ni ndege. Kwa heshima na taadhima naomba Waziri atakapokuja kufanya wind-up, aje kutueleza lini hasa fedha ambazo zimeahidiwa na Serikali za shilingi bilioni 4.2 zitatolewa kwa chuo hicho kwa lengo la kununua ndege single engine aina Cessna 172 ambapo mpaka dakika ndege hizo hazijapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, tuna taarifa ya kwamba chuo hiki kitapata fedha kutoka Benki ya Dunia kiasi cha dola milioni 21.5. Fedha hizi pia zitatumika katika ununuzi wa ndege tatu, kwa hiyo, pamoja na zile mbili ambazo zimeahidiwa na Serikali zitafanya jumla kuwa tano. Mpaka ninavyozungumza hawana hata ndege moja katika kitengo hicho jambo ambalo kwa kweli linakifanya Kitengo hicho cha Usafiri wa Anga kudumaa, naomba Mheshimiwa Waziri aje kutueleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli wa hali halisi ilivyo sasa kuhusiana na uwiano wa marubani ambao wamepata leseni uko 60:40 yaani wageni wana asilimia 60 na wazawa wana asilimia 40 ya idadi ya marubani. Kwa hali hiyo basi, iwapo tutakisaidia chuo hiki, nafikiri uwiano huu utapungua kwa kiasi kikubwa. Itafika wakati sasa sisi kwa maana ya wazawa tutakuwa wengi zaidi kuliko idadi ya foreigners kama ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine nilikuwa nataka kugusia kuhusiana na Shirika letu pendwa la Air Tanzania ambapo kwa hali ilivyo hivi sasa linaendelea vizuri. Mengi ambayo nilikuwa nayakusudia kuyazungumza kwa siku ya leo wenzangu walionitangualia kama Mheshimiwa Kitwanga ameyazungumzia, kwa hiyo, sasa hivi nitazungumzia vile vipande ambavyo yeye hakuvigusia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli biashara ya ndege ni ngumu sana na gharama zake za uendeshaji hali hadhalika ni kubwa kupita kiasi. Napenda kukufahamisha tu kwamba, Rubani yeyote validity ya leseni yake ni miezi sita, ukimaliza miezi sita ina maana aidha ufanye revalidation course ambayo haifanyiki nchini bali ni nje ya nchi katika nchi za Canada, Uingereza au Ethiopia na watu gani wana-incur cost hizo ni shirika lenyewe. Kwa hiyo, wameelemewa na mambo mengi sana, cost ya vipuri halikadhalika iko juu sana. Tairi tu lile la Dreamliner linaweza kufika hata dola 10,000, tairi tu moja. Kwa hiyo, mnaweza kuona gharama za vipuri zilivyokuwa juu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda nishauri Serikali ni kwamba hatuwezi tukaendesha Shirika la Ndege kwa kutegemea fedha ambazo zinapatikana kutoka katika mauzo ya tiketi peke yake, haiwezekani lazima kuwe na mambo mengine, vyanzo vingine vya kupata mapato. Na vyanzo hivyo kwa upande wa Serikali wanaweza kutoa msahada hii Air Tanzania ikawa na Ground Handling Company yake yenyewe hiyo itafanya wapate fedha mbadala inaweza alikadhalika ikapate ile inflight catering service zile na hiyo ni chanzo kingine cha fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuwapatia sehemu ambayo kama godauni wale abiria ambao wanatoka nje ya nchi kuja kwetu wakija na mizigo yao na ile hasa ile ambayo iko sensitive kwa temperature inaweza ikahifadhiwa katika sehemu zile na baadaye sasa shirika likipata nafasi za kwenda kuzipeleka mizigo hiyo katika nchi za jirani kama Malawi na kadhalika na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jana Mheshimiwa Shangazi alizungumza ya kwamba kuna haja ya kupata Cargo Plane nakubaliana naye kwa hundred per cent, isipokuwa ushauri wangu si lazima iwe cargo plane hundred per cent per serve lakini kuna ndege ambayo inaitwa Comb Q4100 ambayo inachukua mizigo na abiria kwa wakati mmoja nafikiri aina hii ya ndege itakuwa inafaa zaidi kuliko kupata ile ambayo Mheshimiwa Shangazi ame-suggest. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nichukue tu fursa hii kumpongeza Mkurugenzi Mkuu na pamoja na Mwenyekiti wa Bodi kwa kazi nzuri sana ambayo wanaifanya na ninaomba nahisihi kwa kuwa shirika letu hili Air Tanzania halijaweza kusimama katika miguu yake miwili yenyewe limefufuliwa tu majuzi bado lina mahitaji mengi tungeweza kusamehe baadhi ya tozo na hilo si geni Ethiopia Airliner kwa mfano hawalipi landing fees, hawalipi parking fees, wala hawalipi navigation fees na sisi tungewasamahe hawa kwa fees kama hizo kwa sababu kwa mwezi tu kwa aina hiyo kwa calculation zangu ina maana fees hiyo ni zaidi ya milioni 400.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni mzigo sana hili shirika bado halijakua kiasi cha kutosha cha sisi kuanza sasa kuwanyonya. Kwa hiyo, kwa maana hiyo basi naomba Serikali iweze kufikiria jambo hili la kuweza kuwasamehe kodi za aina hiyo itapendeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nilitaka kulizungumzia leo ni kuhusiana na hifadhi ambayo ya Serengeti, asilimia yaani asilimia 90 ya hifadhi hii iko nchini kwetu Tanzania na asilimia 10 iko upande wa Kenya ambao wao wanaitwa Masai Mara. Sasa kwa ufupi katika sehemu Masai Mara peke yake wao wana airfields tatu za lami ambazo zina urefu zaidi wa kilometa 1.8, ambayo zinakuwa na uwezo sasa wa ndege aina ya Bombardier Q4100, kuweza kutua katika uwanja ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanachokifanya watalii wanapofika katika uwanja wa kimataifa wa Nairobi ambao wanachukuliwa nchi tofauti huko nje ya nchi. Sasa Kenya Airways wanakuwa na kampuni tanzu, nafikiri subsidiary company ambayo inaitwa Jambo Jet, inachukua watalii inawapeleka moja kwa moja Masai Mara. Sasa pale wale watalii hawawi inconvenient hata kidogo, wanakuwa wanafurahia safari yao kwa sababu ni rahisi. Lakini kwa mazingira hapa ya kwetu sehemu ambazo watalii wanaingia nchini ni Dar es Salaam, Kilimanjaro na Zanzibar, halafu wanakuja kwa makundi makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa maana hiyo basi tungeweza kutengeza uwanja wetu wa ambao uko katika sehemu ya Tanzania unaitwa Sereneira ambao uwanja wenyewe una kilometa 2.2 ni mrefu kiasi cha kutosha, lakini unataka maboresho ili wale watalii ambao wanatelemkia Kilimanjaro au Zanzibar wapate fursa au waweze kuchukuliwa moja kwa moja na Bombardier ya Air Tanzania na kupeleka katika uwanja huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeusaidia uwanja wenyewe kupata mapato, lakini kwa Taifa kwa ujumla siyo watalii wote ambao wanapenda kutelemka uwanja wa Kilimanjaro halafu wakachukua magari kuelekea katika sehemu husika, unakuwa unawasumbua kwa hali ya kutosha. Na hii ndiyo namna ambayo Air Tanzania ingeweza kushiriki moja kwa moja katika kukuza utalii kwa sababu unachukua watu unapeleka kule na wakimaliza shughuli zao wanapanda katika huo uwanja wa Sereneira wanarudi katika sehemu ya Airport kubwa ili waweze kuendelee na safari zao nchi ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ningeliomba hili sana upande wa Serikali uboreshwe uwanja ule na hautaki kazi kubwa, ni kuuweka tu control tower pale kwa sababu uwanja tayari upo mrefu ikiwa kama hali ya uchumi hairuhusu pengine si lazima lami kwa kipindi hichi unaweza ukaweka lami baadaYe ukauchonga katika namna ambayo ndege zinaweza kuteremka na kupaki kiurahisi. Hilo linawezekana kabisa nikuhakikishieni pato la Taifa litakuwa kabisa kwa kufanya hili jambo ambalo nail-suggest, halafu kingineā€¦ (Makofi)

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa ahsante sana, Mheshimiwa Abbas umeongezea dakika tatu za Mheshimiwa Mwita Getere, kwa hiyo, malizia hoja yako.(Makofi)

MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa la mwisho kuhusiana na hali ya Air Tanzania ambayo nilikuwa nataka kuizungumzia ni kwamba kwa ndege zetu, hazitumiki yani kuna underutilization na hizo hizo ndege hazitumiki ipasavyo naweza kusema kama vinatumika kama asilimia 60 underutilization ndiyo inavyofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hii inasababishwa na factors zingine kwa mfano viwanja vyetu vingi havina taa na kwa hali ya kawaida ndege haitakiwi kabisa isimame, wanaobadilishana ni Ma-crew lakini ndege inatakiwa ifanye wakati wote masaa 24 ikiwezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kutokana ukweli kwamba viwanja vyetu vichache tu vyenye huduma ya taa ndiyo maana sasa hatufikii ile kiwango cha matumizi ya ndege zilizokuwepo ya kutosha, lakini hii ni sababu moja. Nyingine ni sababu ya kibiashara ya kwanza unapowachukua watalii au watu wa nchi mbalimbali kwa maana ya wa hapa karibuni Malawi, au Lubumbashi kwa mfano ili kuwaleta Dar es Salaam lazima pengine wale wanasubiriwa sasa ndege nyingine ili waende nje, sasa kama hakuna ndege nyingine ambayo inawasubiri wale abiria ambao wanatoka katika nchi jirani inakuwa ni ngumu, hizo ndiyo sababu za kibiashara ndiyo maana ya kwanza tukawa asilimia 60 tu ya matumizi ya ile ndege ambayo tunayafanya ndiyo ambayo yanatokeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)