Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile kwa kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja. (Makofi)

Mhesimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza na kwa maandishi wakati wa hoja ambayo iko mbele ya Bunge lako Tukufu. Kipekee napenda kumshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba ambaye aliwasilisha maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge kuhusu utekelezaji wa maagizo ya Kamati pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yangu kwa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuwashukuru Kambi ya Upinzani ingawa mambo mengi yameandikwa kwa kukosa taarifa na takwimu sahihi ya hali ya Sekta ya Afya inavyokwenda mbele toka Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameingia madarakani. Kwa hiyo, nitawajibu hoja zao. Katika hatua hii tunawashukuru kwa kutoa hoja ambazo hazina mashiko ya takwimu sahihi na hali halisi ya utoaji wa huduma za afya nchini Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hotuba yangu kwa kuzungumza na kwa maandishi ambao ni Wabunge 112; kati yao Wabunge 44 wamechangia kwa kuzungumza na Wabunge 59 wamechangia kwa maandishi. Aidha, Waheshimiwa Wabunge tisa walichangia wakati wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge ni nyingi, kwa hiyo, nitashindwa. Haya makaratasi yote ni majibu ya hoja ambazo zimetolewa. Kwa hiyo, nitatoa tu ufafanuzi katika baadhi ya mambo makuu. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumepokea maoni na ushauri wenu na tutaufanyia kazi katika kuhakikisha kwamba tunaboresha huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawashukuru katika hatua hii ya awali kwa pongezi kubwa nyingi ambazo wametupatia mimi, Naibu Waziri pamoja na Watendaji wa Wizara na Katibu Mkuu. Naomba kupitia kwako niwaahidi Waheshimiwa Wabunge wote, pongezi hizi hazitatufanya sisi tukalewa sifa, bali ni chachu ya kufanya kazi vizuri zaidi ili tuweze kuhakikisha huduma bora za afya, maendeleo na ustawi wa jamii zinapatikana kwa Watanzania, lakini hasa wa kipato cha chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia Universal Health Coverage hatuzungumzii tu Bima ya Afya, maana yake kila Mtanzania wa hali yoyote masikini, kipato cha kati, tajiri wa kijijini, wa mjini aweze kupata huduma za afya bila ya kikwazo chochote ikiwemo kikwazo cha fedha. Kwa hiyo, niseme tu kwamba tumepokea ushauri na pongezi lakini tutaendelea kufanya kazi kuhakikisha tunatatua changamoto za Sekta ya Afya katika nchi yetu, kwani tunatambua bila afya hakuna elimu, bila afya hakuna maendeleo, bila afya bora hakuna uchumi na bila afya bora hakuna ulinzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijatoa ufafanuzi, natambua kwamba Kanuni za Bunge zilishatoa pole, lakini kabla sijaendelea, naomba nami kuungana na Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu kutoa pole kwa familia ya Dkt. Reginald Mengi ambaye amekuwa mdau mkubwa wa Sekta ya Afya. Kwa hiyo, tunawapa pole familia na tunawaombea Mwenyezi Mungu awape subira na ustahimilivu katika kipindi hiki kigumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wewe ni shahidi, Dkt. Mengi amekuwa akitupa nafasi katika vyombo vyake ITV, Radio One, East Africa Radio kutoa Elimu ya Afya kwa Umma kuhusu masuala mbalimbali. Pia ameweza kusaidia watu wenye ulemavu. Kubwa, tutamkumbuka na kum-miss katika Sekta ya Afya kwa sababu alianza kuwekeza kujenga Kiwanda cha Dawa M-Pharmaceuticals Bagamoyo, lakini Mwenyezi Mungu hakupenda ndoto yake iweze kutimia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa niruhusu nijibu baadhi ya hoja. Nikianza na hoja ambazo zimetolewa na Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii; tumepokea ushauri na maoni ya Kamati na kwa kweli yote tutayafanyia kazi. Jambo kubwa ambalo walilitolea maoni ni kwamba Serikali ihakikishe fedha zilizotengwa kwa Mwaka 2018/2019 zinatolewa zote na kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakubaliana na ushauri huu na niwaahidi Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango ili kuhakikisha kwamba fedha zote ambazo zimetengwa katika bajeti ambayo inaisha Juni zinatolewa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninazo habari njema. Mheshimiwa Dkt. Mpango na timu yako ninakushukuru sana. Katika mwezi wa Pili ambapo tulishatoka kwenye Kamati, tumepata shilingi bilioni 62 kutoka Hazina, shillingi bilioni 20 tumepata kwa ajili ya dawa; shilingi billioni 32 tumepewa baada ya kuwa tumeshawasilisha makadirio yetu kwenye Kamati ambazo zitatumika kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa ikiwemo upandikizaji wa kutumia chembe chembe za mwili tunaita bone marrow transplant.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumepata kutoka Hazina shilingi bilioni 10 kwa ajili ya kuboresha huduma katika Hospitali za Rufaa za Mikoa. Nje ya bajeti ambayo ilipitishwa na Bunge lako Tukufu Mheshimiwa Oscar Mukasa amesema hapa, sisi pia; mimi na Naibu Waziri na Katibu Mkuu, tunahangaika kutafuta vyanzo vingine vya fedha. Kwa hiyo, nje ya bajeti ambayo imetolewa, ndani ya mwezi wa Nne tumepata shilingi bilioni 58 kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya ambao tumepeleka katika zahanati, katika hospitali za wilaya, katika vituo vya afya kwa ajili ya fedha za uendeshaji. Kwa hiyo, tunapokea maoni na ushauri wa Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni Serikali ya kushughulikia na kutatua changamoto za watu hasa wanyonge na ndiyo maana fedha hizi zimeendelea kutoka kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo limeelezwa na Kamati ni kwamba Serikali ikamilishe mchakato wa kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya. Tunakubaliana na ushauri huu na tunaamini, kama tulivyoahidi katika hotuba yangu, mwezi wa Tisa tutakuja Bungeni kwa ajili ya kuleta mapendekezo ya Sheria ya Bima ya Afya ambayo itamlazimu kila Mtanzania sasa kuwa na Bima ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na hoja za Waheshimiwa Wabunge. Mtanzania masikini kama huna hela ni changamoto kupata matibabu. Tukiangalia takwimu ambazo nimezionesha katika kila Watanzania 100 ni Watanzania nane tu ndio wana Bima ya Afya ya NHIF. Sasa Mtanzania huyo awe na tatizo amezungumza kaka yangu Mheshimiwa Khatib kutoka Pemba, unatakiwa kufanya dialysis session moja ni shilingi 180,000/= mpaka shilingi 250,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, Daktari anaweza akakwambia ufanye dialysis, yaani kuchuja damu sijui kusafisha damu au kutakasa damu (sijui dialysis kwa Kiswahili), Kutakasa damu nadhani kwa Kiswahili kizuri. Anaweza akakuandikia ufanye mara tatu; minimum anaweza kukwambia ufanye mara mbili kwa wiki. Mara mbili Mtanzania gani anaweza ku-afford shilingi 400,000/= kila wiki kwa ajili ya huduma za dialysis?

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeoneshwa huduma za kupandikiza figo, kupandikiza vifaa vya kuweza kuwasaidia watoto kusikia, ni Bima ya Afya ndiyo zimefanya hii kazi ya kutoa huduma hizo ambazo zilikuwa zinapatikana kwa shilingi milioni 30 mpaka shilingi milioni 80. Kwa hiyo, tunakubaliana na Waheshimiwa Wabunge kwamba tutaleta Muswada wa Sheria, lakini pia kabla ya kuleta Muswada wa Sheria, tutaendelea pia kufanya uhamasishaji na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kujiunga na Bima ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kwamba Watanzania hawana pesa, kuna suala la willingness to pay na affordability to pay. Kwa hiyo, Watanzania wengi bado hawako tayari kulipa Bima ya Afya. Nitumie Bunge lako Tukufu kutoa rai kwa Watanzania. Ule utamadumi tuaojenga kuchangiana harusi, kuchangiana Kitchen Party, tuujenge katika kuchangiana kununua Bima za Afya kwa ajili ya Watanzania masikini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limeongelewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge, jambo la tatu, ni suala la kufanya uboreshaji wa huduma za uzazi katika maeneo mbalimbali. Tunakubaliana na ushauri wa Kamati. Waheshimiwa Wabunge wenyewe ni mashahidi, hata vituo vya afya vinavyoboreshwa na vilivyoboreshwa 352, asili yake ya andiko la vituo hivi ni kuboresha huduma za uzazi, mama na mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili tuliona, hivi sisi kama Mawaziri; nilikaa nikasema, hivi mimi Ummy Mwalimu, Waziri mwanamke, sina background ya Udaktari, lakini bado Mheshimiwa Rais ameniamini niongoze Wizara ya Afya, naacha legacy gani kwa Watanzania? Kwa hiyo, nawashukuru sana wataalam wa Wizara, tuliweza tukakaa tukaandika andiko na ndiyo maana sasa tunaboresha vituo vya afya takriban 350. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Jafo na timu yake kwa sababu walijiongeza na Dkt. Chaula. Sisi tungeweza tu tukatafuta fedha, lakini wao wakaja na wazo la Force Account ambalo limeleta mafanikio makubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya afya. Kwa hiyo, tunakubaliana na maoni ya Kamati. Tutaendelea kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nataka kusema mbele ya Bunge lako Tukufu, tunataka Watanzania hasa wanawake ambao ndio wapigakura wa chama changu Chama cha Mapinduzi kujionea kwamba huduma za afya ya mama na mtoto zimeboreka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na vituo vya afya, pia tumeanzisha kampeni mbalimbali za kuhamasisha uwajibikaji na matokeo chanya katika kupunguza vifo vya akina mama na mtoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa ndio mlezi wa kampeni hii. Tumeweza pia kuhakikisha tunaweka wataalam wakiwemo wataalam wa kutoa dawa ya ganzi na usingizi ambapo tumeweza kugharamia mafunzo takriban ya watu 200.

Mheshimiwa Naibu Spika, wifi yangu, sijui kama naruhusiwa kusema hivyo, Mheshimiwa Esther Matiko nitamjibu baadaye, lakini anaweza akasema labda tunasema. Ukitaka kupima, je, tunakwenda mbele katika eneo hili la afya ya mama na mtoto au hatuendi mbele? Tunaangalia viashiria vikuu ambavyo vimewekwa na Shirika la Afya Duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kiashiria cha kwanza: Je, huduma za uzazi wa mpango zinaendelea? Kwa mujibu wa takwimu zetu, tumeongeza kiwango cha watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango kutoka asilimia 32 hadi asilimia 38. Hizi ni takwimu za NBS. Tukiangalia program data tutakuwa tuko vizuri zaidi.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Huo ndiyo ukweli.

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, wakati wenu wa kuchangia Mheshimiwa Waziri alikuwa kimya akiwasikiliza na ninyi msikilizeni anapowajibu. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, huo ndiyo ukweli. Hata tukiangalia akina mama wanaojifungulia katika vituo vya kutoa huduma za afya, kabla Mheshimiwa Dkt. Magufuli hajaingia madarakani ilikuwa ni asilimia 65 lakini kwa sababu huduma za uzazi za mama na mtoto zimeboreka, tumeongeza idadi ya akina mama wanaojifungua katika vituo vya kutoa huduma za afya kufikia asilimia 32. Huu ndiyo ukweli, hata katika ngazi ya mikoa, inaonekana kwamba hali ya huduma za mama na mtoto zinaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ambalo ndiyo viashiria vikuu vya afya ya uzazi ya mama na mtoto, je, kuna ongezeko la akina mama wajawazito ambao wanahudhuria kliniki angalau mara nne katika kipindi cha ujauzito wao. Tumeonyesha pia kwamba lipo ongezeko la zaidi ya asilimia 30 la wanawake ambao wanahudhuria kiliniki angalau mara nne. Kwa hiyo, hivi ndiyo viashiria vikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakuja kwenye takwimu, je, vifo vimepungua au havijapungua. Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), ulikuwa ni utafiti wa mwaka 2015, kwa hiyo, sasa hivi hatuna takwimu zaidi ya hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu, NBS akifanya utafiti mwingine, sina shaka, vifo vya akina mama wajawazito vitakuwa vimepungua kwa zaidi ya asilimia 50. Tukikusanya takwimu ambazo tunazo katika mikoa, sipendi kuzitaja kwa sababu siyo takwimu rasmi, lakini hali inaonyesha kwamba tumepunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya akina mama wajawazito. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya nne ambayo imeelezwa na Kamati na ambayo tumeipokea ni suala la maambukizi ya UKIMWI na kwamba katika maambukizi mapya ya UKIMWI asilimia 44.6 ni vijana wakati sheria inakataza mtu mwenye umri wa miaka 18 kupima UKIMWI bila ya ridhaa ya wazazi lakini pia inakataza mtu kujipima UKIMWI mwenyewe isipokuwa apime katika vituo vya kutolea huduma za afya. Tumepokea ushauri na tayari tumeandaa marekebisho ya Sheria ya VVU na UKIMWI, Sura ya 431 ambayo tumependekeza turuhusu mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 18 kupima UKIMWI bila kuhitaji ridhaa ya mzazi au mlezi. Pia tunapendekeza kwamba tutafanya marekebisho ya sheria hiyo, kifungu 13(4) ili kuondoa ulazima wa watu kupima VVU katika vituo vya kutolea huduma za afya tu. Kwa hiyo, hayo tunategemea kuja katika Bunge lako Tukufu mwezi Septemba ili tuweze kufanya marekebisho haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Kamati kwamba hatuwezi kufikisha lengo la pili na la tatu la kuhakikisha tunatokomeza UKIMWI kama hatutatimiza lengo la kwanza ambalo sasa hivi takwimu rasmi za NBS zinaonyesha kwamba ni asilimia 51. Takwimu rasmi za programu data tunaonyesha kwamba watu ambao wanaishi na Virusi vya UKIMWI na wanajua hali yao ni asilimia 75. Kwa hiyo, sina shaka kwamba tukifanya haya marekebisho mawili ya kuruhusu watu kujipima UKIMWI na watoto kuruhusiwa kujipima bila ridhaa ya wazazi/walezi kwa sababu wanaolewa kwenye miaka 15 au 16 tutaweza kuongeza kasi ya kupambana na UKIMWI.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tano ambalo limeongelewa na Kamati ni suala la afya ya usafi na mazingira kwamba tushirikiane na Wizara ya Maji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Tumepokea yote haya na ni kweli nikiwa kama Waziri ambaye nasimamia sekta ya afya, tunaona mzigo mkubwa wa wagonjwa, takribani katika kila wagonjwa 100 wanaohudhuria OPD kwa maana ya wagonjwa wasio wa kulazwa asilimia 60 ni magonjwa haya yanayotokana na suala zima la usafi. Pia tuna taarifa ya Benki ya Dunia ambayo imeonesha kwamba Tanzania tunapoteza takriban shilingi bilioni 400 kila mwaka kutokana na hali duni ya usafi. Kwa hiyo, tumepokea ushauri kuhusiana na hali duni ya usafi na tutayafanyia kazi masuala haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la sita ambalo limezungumzwa na Kamati kwa upande wa Fungu 52 ni huduma za lishe. Tunalipokea na sisi tutaendelea kuhamasisha wananchi kuhakikisha kwamba wanazingatia lishe bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende katika hoja zilizoletwa na Kamati kwa upande wa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii na kubwa lilikuwa Serikali ihakikishe kwamba Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii inatengewa fedha kwa ajili ya kufanya kazi za maendeleo na ustawi wa jamii. Tumepokea ushauri huu na naamini Mheshimiwa Dkt. Mpango ananisikia kwamba Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii nao wana mchango mkubwa katika kuhakikisha tunajenga Tanzania ya Uchumi wa Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge, hata juzi nimeongea na Watendaji wa Wizara, Wizara hii ni moja, kwa hiyo, lazima sasa tuoneshe kwamba hakuna Vote ya Maendeleo ya Jamii ya Jamii au Vote ya Afya, bali ni Wizara moja. Kwa hiyo, tunaona Sekta ya Afya inapata rasilimali nyingi kutoka kwa wadau, kwa hiyo, tumeamua tutakuwa tunakata asimilia ya fedha za wadau ambazo tunazipata kwenye Sekta ya Afya, tutazipeleka kwenye Sekta ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala kubwa ambalo lilitolewa sasa na Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Kuna jambo moja naomba niliseme, hii hotuba ukisoma, kuna maneno mengine unasema, hivi huyu ni Mtanzania ambaye yuko Tanzania au yuko nje ya nchi, anazungumza mambo ambayo hajui nini kinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu anasema, anasema majigambo ya Serikali kwamba imeboresha sekta ya afya nchini ni kutafuta umaarufu wa kisiasa. Hivi unajiuliza hivi huyu, anajua analolisema au basi tu anataka kusema ili aweze kusikika anaposema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binadamu mwema ni yule mwenye kushukuru, lakini pia kazi kubwa imefanyika chini ya Utawala wa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko, shida iko wapi Mheshimiwa Esther Matiko tafadhali, hajakutaja wewe anaongea kwenye hotuba, kwa nini usimpe muda azungumze amalize, kwa nini usimpe nafasi azungumze? Tafadhali Mheshimiwa Esther Matiko, hii ni mara ya mwisho nakutaja jina humu ndani, tafadhali. Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposema huduma za afya zimeboreka hatutafuti umaarufu wa kisiasa, bali ndiyo ukweli. Naomba nitoe mifano kama minne, wakati Mheshimiwa Dkt. Magufuli anaingia madarakani, watoto waliokuwa wanapata chanjo ni chini ya asilimia 85, leo asilimia 99 ya watoto wote wenye umri wa chini ya mwaka mmoja wanapata chanjo na nieleze ni halmashauri gani imekosa chanjo za watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati naingia, wazazi wamejifungua watoto hawana chanjo za kuwazuia na kifaduro, kifua kikuu, leo chanjo zinapatikana za watoto katika kila watoto 100, watoto 99 wanapata chanjo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika huduma za matibabu ya kibingwa, Wabunge wameona, kabla Mheshimiwa Dkt. Magufuli hajaingia madarakani, niambieni kama kulikuwa na upandikizaji wa figo, niambieni kama kulikuwa na upandikizaji wa vifaa vya kuweza kusikia, lakini leo hadi ninaposema kuanzia mwaka 2017, Watanzania 38 wameweza kupandikiziwa figo katika Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili; Watanzania saba wameweza kupandikiziwa figo katika Hospitali yetu ya Benjamin Mkapa. Hawa Watanzania, hawawezi kusema ni umaarufu wa kisiasa, ila wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa sababu amewezesha huduma hizi kupatikana na zingekuwa zinapatikana nje ya nchi, wasingeweza kutoa milioni 100, milioni 120 kupata huduma hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cochlear implant, upandikizaji watoto wa vifaa vya kuwasaidia kusikia, havijawahi kufanyika, vimefanyika wakati wa Mheshimiwa Dkt. Magufuli, watoto 21 wamefanyiwa. Sasa unajiuliza, hivi huyu anaposema ni umaarufu wa kisiasa, nadhani tumsamehe bure. Hivi anaposema ni umaarufu wa kisiasa, anaandika kwenye speech, umaarufu wa kisiasa, watoto 21 wamepandikizwa vifaa vya kuwasaidia kusikia! cochlear

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kutoa mifano, health centers, vituo vya afya 352 vinaboreshwa na vimekamilika, tuna Hospitali za Wilaya 67 zinaendelea kujengwa, lakini pamoja na msomaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, ana Kituo cha Afya kinaitwa Magena kimepata milioni 400. Halafu atasema ni umaarufu wa kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kusema, yapo mambo makubwa ambayo yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano na kwa kiasi kikubwa huduma za afya zimeboreshwa. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kukiri kwamba, changamoto za afya bado ni nyingi na tutaendelea kuzifanyia kazi, lakini lazima tushukuru mambo makubwa na mazuri ambayo yamefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tena nimalize, suala la pili, ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani imehoji, kwamba bajeti ya afya imepungua kutoka shilingi trilioni moja hadi shilingi bilioni 866, lakini pia tunategemea fedha za wazungu. Kwa hiyo, hawa hawa Wabunge ndiyo wamekuwa wakituambia tupunguze utegemezi wa wahisani! Kwa hiyo, kilichopungua, Mheshimiwa Dkt. Mpango ni shahidi, tumepunguza fedha zilizotoka kwa wahisani, lakini fedha za ndani ya nchi, fedha za walipa kodi wa Tanzania, zimeendelea kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia bajeti ya mwaka 2017/18 ilikuwa bilioni 628, lakini mwaka 2018/2019 bilioni 681; mwaka 2019/2020 bilioni 686.6, kwa hiyo, unaziona fedha za ndani zinaendelea kukua, lakini ni kweli fedha za nje tumepunguza! Tulianza mwaka 2017/2018 ilikuwa ni bilioni 449, tumepunguza mpaka bilioni 184 na mwaka huu tunaomba fedha za nje bilioni 272. Kwa hiyo, inategemea unaliangalia kwa perspective gani, lakini kama ni kuongeza fedha za ndani, hakuna fedha ya afya ambayo imepungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna swali pia limezungumzwa na Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu suala la PPP, hilo sisi niseme tulishaanza kulifanyia kazi na kwa mfano katika kufunga mashine za kupima maambukizi ya damu, tumeweza pia kuingia mikataba na mdau ambaye amefunga mashine hatutumii fedha za Serikali, lakini pia tumetangaza tenda ya kuweza kuhakikisha tunafunga vifaatiba bila kutumia fedha za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limeelezwa na Kambi Rasmi ya Upinzani ni suala la huduma ya afya bila malipo kwa wanawake, lakini pia tumewasikia, suala la Wakunga wa Jadi kwamba wamezuiliwa. Tulichokitaka, siyo kuwazuia Wakunga wa Jadi, tunaendelea kutambua na kuthamini mchango wa Wakunga wa Jadi kama wadau wakubwa wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto. Sasa tunachokifanya, tunataka hawa watu wawe kama ni daraja letu kati ya vituo vya kutoa huduma za afya pamoja na Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunasema kwamba Wizara itaendelea kuwaelimisha Wakunga wa Jadi kuhusu umuhimu wa kuwashauri wajawazito kwenda katika vituo vya kutolea huduma mapema ili kupata huduma bora na salama za kujifungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hayo ndiyo makubwa ambayo ningetaka kuyajibu kutoka kwenye Kambi Rasmi ya Upinzani, lakini mengine yote tunakubaliana na wao, ikiwemo kuendelea, kuhakikisha tunatumia Community Health Workers, amezungumza Mheshimiwa Kandege kwamba changamoto ambayo tunaipata na kuna baadhi ya Wabunge wametoa mfano, kuna vituo vya afya vinaongozwa na Medical Attendant (Mhudumu wa Afya), lakini kuna vituo vya afya unakuta vinaongozwa na Wauguzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo sasa ndiyo tunajaribu kuweka balance, uwiano. Je, tujaze watumishi wa kwenye facilities au twende kwenye Community Health Worker, lakini as a matter of sera, ikiwa ni suala la kimsingi, tunakubaliana nalo na especially mimi katika ajenda yetu ya kuhakikisha tunaongeza hali ya lishe kwa akinamama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, lakini pia tunaongeza watu ambao wanajua maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na katika mapambano ya kifua kikuu tunaamini kwamba wahudumu wa afya ngazi ya jamii watato mchango mkubwa. Tunategemea kuajiri takriban 600 kupitia fedha ya Mfuko wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja zilizoelezwa ni nyingi, ikiwemo uboreshaji wa huduma katika ngazi zote tumepokea na lengo letu kwa kweli tunataka kutoka kwenye bora huduma twende huduma bora na ndiyo maana Wizara ya Afya tunayo idara ya kusimamia uhakiki wa ubora wa huduma za afya. Kwa hiyo, tutahakikisha kinafanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunakusudia kutoa usajili wa vituo vya kutoa huduma za afya vya Serikali na binafsi. Lengo letu tukiona, hata cha Serikali tukikiona hakina ubora, tunataka kukifungia kama vile tunavyofungia vituo vya afya vya binafsi. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo tumekubaliana kwamba tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la vifaa na vifaatiba kwa ajili ya vituo vya afya vilivyoboresha, Mheshimiwa Naibu Waziri ameongea kwamba tumeanza kununua lakini tutahakikisha kwamba, kwa sababu hata zoezi hili la kukarabati vituo vya afya, lilienda kwa awamu, kwa hiyo niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutahakikisha tunanunua vifaatiba na kuvifunga katika vituo vya afya vilivyoboreshwa ili viweze kutoa huduma bora zilizokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lilikuwa wazo, hoja ambazo pia zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge ni suala la X-Ray machines; wengi wameeleza kwamba hazifanyi kazi au ni za zamani. Naendelea kuwathibitishia Waheshimiwa Wabunge kwamba tumeshaagiza x-rays takriban 70 za kisasa, kwa hiyo, tutazisambaza katika Hosptali za Rufaa za Mikoa, lakini pia katika Vituo vya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mzee wangu Deo Sanga, nimemsikia kuhusu Makambako, nakubaliana na yeye, hata kama ni kituo cha afya, kwa kweli tutahakikisha kwamba anapata x-ray ili kuweza kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumezungumzwa suala la ambulance, Waheshimiwa Wabunge tumewasikia sana na tulikuwa tunaongea na Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa, mahitaji ya ambulance ni mengi, lakini kama nilivyoeleza katika hotuba yangu, tayari tumeagiza ambulances 50, kwa hiyo tutazigawa katika maeneo yenye uhitaji, lakini tutaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kugawa ambulance.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamaliza, nizungumzie suala ambalo pia limeongelewa na Waheshimiwa Wabunge, kwamba maiti anachajiwa, anadaiwa sijui. Kwa kweli, tunapata changamoto, lakini naomba Waheshimiwa Wabunge watuelewe, angalau katika Tanzania na hasa Hospitali yetu ya Taifa Muhimbili, kipaumbele wanakiweka kwa mgonjwa kupata huduma. Maana bora mtu angekufa kwamba kakosa huduma, lakini mtu kwanza anapata huduma, akishapata huduma ndiyo linakuja suala la deni. Nilikuwa naongea na Profesa Museru, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali yetu ya Taifa, Muhimbili, amenieleza, Mheshimiwa Waziri ambao wanakuja kwako pia, saa nyingine hawafuati taratibu. Kwa hiyo, nitoe rai kwa Watanzania, kwanza kuhakikisha tunawekeza kwenye afya zetu kwa kukata bima ya afya, lakini pale ambapo hatuna uwezo wa kulipia, basi tufuate utaratibu wa kupata matibabu bila malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninazo takwimu hapa, tukiangalia Hospitali ya Taifa Muhimbili, kuanzia Julai mpaka Disemba, iliweza kutoa msamaha kwa wagonjwa wenye thamani ya shilingi bilioni 2.7, kwa hiyo, watu wanasamehewa. Vile vile tukiangalia Hospitali ya MOI, Julai hadi Desemba, ilitoa msamaha kwa wagonjwa wenye thamani ya shilingi milioni 347. Tukiangalia Mloganzila Julai hadi Desemba, 2018 walitoa msamaha kwa wagonjwa wenye thamani ya shilingi milioni 178.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninazo takwimu mpaka za Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tunaomba watuelewe, hapo hapo tunahitaji kuboresha huduma, sasa tukisema tu jamani kila kitu bure bure bure, jamani bure, bure ni gharama, bure ni gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena bure ni gharama, kwa hiyo muhimu tuendelee kuhakikisha kwamba, kwanza tunawekeza kwenye afya zetu, lakini pili pia tunafuata taratibu katika kupata huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumze suala moja ambalo limeongelewa na Mheshimiwa dada yangu Taska Mbogo, kuhusu Customary Declaration Order, ni ya zamani na kandamizi na inabagua wanawake. Nakubaliana sana na Mheshimiwa Mbogo, kwamba sheria hii ni ya zamani, lakini kuna maamuzi ya Mahakama Kuu kwenye Kesi Na. 82 ya mwaka 2005 ambayo inatambulikana kama Elizabeth Stephen na mwenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambayo ilitolewa maamuzi tarehe 8 Mwezi wa Tisa mwaka 2006, mbele ya Majaji watatu wa Mahakama Kuu kuwa, Serikali imeweka kifungu cha 12 cha Sheria ya Judicature and Application of Laws Act, ambacho kinamtaka mtu yeyote atakayeona kuna mila kandamizi inayomzuia kupata haki yake, kufuata utaratibu uliowekwa katika kifungu hicho kwa kuwasilisha maombi ya kubatilisha mila hiyo kupitia Waziri wa TAMISEMI.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba kusema hii ni changamoto. Dada yangu Mheshimiwa Taska Mbogo, naomba nilichukue, tutakwenda kulifanyia kazi ili kuhakikisha ikiwezekana tunafuta sheria hii. Kwa sababu hoja ambayo ipo ni kwamba kuna baadhi ya mila zetu ambazo zimo ndani ya sheria hii siyo mbaya, za kutunza wazee na watoto wa ndugu. Kwa hiyo, tutaangalie yale ambayo yanamkandamiza mwanamke tutaweza kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mdogo wangu Mheshimiwa Amina Mollel amezungumzia suala la unyanyasaji wa wasichana hasa wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu. Sera ya Usawa wa Jinsia na Maendeleo ya Wanawake inahimiza kuanzishwa kwa Madawati ya Jinsia katika Taasisi, Wizara na Idara za Serikali. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kuvitaka vyuo vya elimu ya juu nchini kuanzisha Madawati ya Jinsia ili kuweza kushughulikia changamoto mbalimbali za jinsia ikiwemo vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanafunzi katika vyuo vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipongeze sana jitihada za Kamishna Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambaye ameanzisha Dawati la Jinsia ndani ya TAKUKURU ili kuweza kupambana na rushwa ya ngono. Kwa hiyo, nitoe pia wito kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu juu ambao wananyanyaswa au wanakumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kuhakikisha kwamba wanatoa taarifa katika Dawati hili la Jinsia ambalo limeanzishwa mwaka huu chini ya TAKUKURU.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, hoja ambazo zimeongelewa ni nyingi lakini kipekee niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge wa kutoka Mikoa mipya ya Katavi, Songwe, Njombe, Simiyu na Geita kwamba kipaumbele chetu kama Wizara tumekubaliana mwaka huu ni kukamilisha Hospitali za Rufaa za Mikoa ili ziweze kutoa huduma za rufaa katika mikoa hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika Mkoa wa Singida na Shinyanga, mdogo wangu Mheshimiwa Aisharose Matembe na ndugu yangu Mheshimiwa Azza Hillal, kama Wizara tumejipanga kuhakikisha tunakamilisha ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mikoa. Lengo ni ili sasa tuweze kukabidhi Hospitali ya Shinyanga kwa Manispaa ya Shinyanga, pia tukabidhi Hospitali ya Singida kwa Manispaa ya Singida. Kwa hiyo, mdogo wangu Mheshimiwa Aisharose na ndugu yangu Mheshimiwa Azza Hillal tunataka kuwathibitishia kwamba jambo hili pia tutalikamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hospitali nyingine za Rufaa za Mikoa kama tulivyosema tumezipokea kuanzia tarehe 1 Julai 2018. Tunachokifanya, tumeamua kuwekeza katika maeneo makubwa manne. Eneo la kwanza ni kuhakikisha tunakuwa na miundombinu ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura na ajali (emergence medicine) na tayari tumeanza kupata fedha kutoka Global Fund tutaanza kuweka vitengo vya dharura katika hospitali saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni kuweka huduma za ICU, huduma kwa wagonjwa wanaotaka uangalizi maalum. Huduma hii tutafanya pia katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa. Eneo la tatu ni kuboresha huduma za uzazi. Eneo la nne tunataka kuhakikisha tunaweka Madaktari Bingwa katika Hospitali za Rufaa za Mikoa yote. Tumebainisha maeneo nane ya kipaumbele, tunataka kuhakikisha tuna Madaktari Bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake angalau wawili, magonjwa ya watoto angalau wawili, upasuaji angalau wawili, upasuaji wa mifupa angalau wawili, usingizi na radiolojia na magonjwa ya ndani (internal medicine).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hayo ni maeneo ambayo tumeyabainisha na tutahakikisha kwamba kila Hospitali za Rufaa za Mikoa zinakuwa na wataalam hawa. Kama alivyosema Naibu Waziri tayari tumeanza kusomesha madaktari na ili tuweze kukupa ufadhili wa kusoma masters ya udaktari tutawafungisha mkataba ili wakimaliza waweze kufanya kazi katika Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema mambo ni mengi lakini kwa kweli kipee nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, asiye na macho haambiwi tazama, kazi kubwa na nzuri imefanyika katika utoaji wahuduma za afya. Mimi niseme tutaendelea kuhakikisha tunatimiza ndoto yake ya kuifanya Tanzania ya viwanda kwa kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na afya bora badala ya kusubiri kwenye mambo ya tiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge tumewasikia, Mzee wangu Mheshimiwa Lubeleje tumekusikia, tunataka na sisi tuondoke kwenye taifa la kulilia dawa, dawa, lakini liwe ni taifa la kulilia afya na lishe bora. Kwa hiyo, jambo hili pia tutalifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, mama Samia Suluhu Hassan ambaye kwa kweli amekuwa akinipa msaada mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yangu. Namshukuru sana mama Samia katika kuimarisha afya ya uzazi ya mama na mtoto. Mheshimiwa dada yangu Mariam Kisangi ameonesha, watu wanaosema hakuna mabadiliko, Hospitali ya Mkoa wa Rufaa ya Temeke hakuna kifo kimetokea mwezi Machi, mama Kisangi ni shahidi na watu wanaona. Halafu watu wanasema hakuna kazi imefanyika, kazi imeonekana ndiyo maana hakuna vifo vya akina mama wajawazito.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa uongozi wake mahiri na nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri wote. Kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Naibu Waziri kwa mchango mkubwa sana ambao ananipatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi niliambiwa unajua hawa madaktari wanaweza wakadharau lakini Naibu Waziri amekuwa akinipa mchango na heshima kubwa katika utendaji wa kazi zangu. Mheshimiwa Naibu Waziri nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru pia Katibu Mkuu (Afya), Dkt. Zainabu Chaula. Kwa kweli tunafurahi sana kama Wizara ya Afya tumepata mama ambaye anajua kusukuma mambo na anajua kusimamia utendaji katika Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana Dkt. John Jingu ambaye naye ni Katibu Mkuu, Maendeleo ya Jamiii kwa kazi kubwa na nzuri ambayo amefanya katika kusimamia Sekta ya Maendeleo ya Jamii. Tunamshukuru sana pia Mganga Mkuu wa Serikali na madaktari wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili tunawashukuru madaktari, wauguzi na watoa huduma za afya nchini. Hapa naongea kama Waziri wa Afya, nitoe maelekezo na maagizo kwa viongozi wenzangu, tuache kuingilia fani za kitaaluma. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna daktari au muuguzi amekosea ashughulikiwe kwa mujibu wa taratibu za Utumishi wa Umma. Narudia tena, kama kuna daktari amekosea tuleteeni kwenye Baraza la Madaktari, tutafuta usajili wake. Kama kuna muuguzi amekosa tuleteeni kwenye Baraza la Wauuguzi na Wakunga tutafuta usajili wake. Kama kuna mfamasia amekosea tuleteeni kwenye Baraza la Wafamasia ambalo ndiyo limeanzishwa kisheria kushughulikia changamoto kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka mitatu ambayo nimekaa katika sekta ya afya, Naibu Waziri ameongea, kazi ya wauguzi watano inafanywa na muuguzi mmoja halafu bado huwezi ku-appreciate (kuthamini)? Madaktari hawa wanajituma sana, kwa kweli lazima tutambue mchango wao na tuheshimu kazi kazi yao nzuri. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi na Naibu Waziri tutaendelea kuwatetea madaktari na wauguzi wetu kwa sababu mwisho wa siku wanaopata matatizo ni Watanzania wanyonge. Mwenye hela zake haendi kwenye hospitali ya Serikali au kituo cha afya cha Serikali. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli inatia uchungu, sisi ambao tuko kwenye sekta hii tunaelewa changamoto ambazo watoa huduma za afya wanapata. Kwa hiyo, sisemi kwamba wote ni malaika au ni wazuri, hapana, wapo wabaya lakini tufuate taratibu za kuwawajibisha watumishi watoa huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mkubwa na mzuri ambao wamekuwa wakinipatia katika kutekeleza majukumu yangu. Kipekee, nawashukuru wadau wetu wa maendeleo hususani wanaochangia Mfuko wa Afya wa Pamoja ambao ni Denmark, Canada, KOICA, UNICEF na World Bank, nadhani nimewamaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawashukuru na wadau wengine ambao hawachangii kwenye Mfuko wa Afya lakini mchango wao ni mkubwa ikiwemo Global Fund, Mfuko wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI pamoja na watu wa GAVI, Abbott Fund wote hao wanatusaidia, pamoja mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya dini. Nawashukuru sana Wakuu wa Taasisi na Idara za Serikali, Hospitali zetu za Taifa Muhimbili, Bugando, Jakaya Kikwete, Ocean Road, MOI, Benjamini Mkapa na hospitali nyingine zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu niwaambie Waheshimiwa Wabunge tutajibu hoja zenu zote kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.