Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Hasna Sudi Katunda Mwilima

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo, nianze sasa kuchangia Wizara hii. Kwanza nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Waziri kwa kunipatia ambulance mbili Kata ya Buhingu, kwenye kituo cha afya na ya pili Kituo cha Afya Kata ya Uvinza. Sambamba na shukrani hizi bado tuna changamoto kubwa kwenye Kituo cha Afya Kalya, kina umbali wa kilometa 250. Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara alituahidi ambulance ya Kituo cha Kalya, tunaomba tuletewe hiyo ambulance.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunavyo vituo vya afya vinne vinavyojengwa ndani ya Jimbo langu. Vituo vitatu Ukanda wa Ziwa Tanganyika na kituo kimoja ukanda wa reli. Vituo hivyo ni hivi vifuatavyo: Kituo cha Afya Kabeba, Kituo cha Afya Kazuramimba na Kituo cha Afya Igalula (Rukoma). Tunazo pia zahanati mbalimbali zinazojengwa kwa jitihada za wananchi na kupitia Mfuko wa Jimbo. Mheshimiwa Waziri akiona inampendeza atusaidie fedha kwa ajili ya kumalizia maboma haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaishukuru Serikali kwa kutupatia shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Ujenzi umeshaanza, tunaendelea. Tunaomba kwenye bajeti hii tutengewe fedha nyingine kwa ajili ya kuendeleza hospitali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, majengo hayawezi kwisha bila vifaa na watumishi. Hivyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri kwenye mgao wa watumishi, Uvinza iangaliwe kwa jicho la huruma, kwani jimbo ni kubwa na watumishi ni wachache sana. Sambamba na watumishi, tunaomba pia vitendeakazi, kwa mfano Ukanda wa Ziwa Tanganyika na Kituo cha Nguruka wapate vifaatiba kama X-Ray, Ultrasound na vifaa vingine, kwani wagonjwa ni wengi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua fika Halmashauri ya Uvinza ilianzishwa tarehe 18 Mei, 2012 lakini hakuna idara hata moja iliyo na gari. Hii inasababisha Wakuu wa Idara kupata taabu sana kwenye kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa fedha zinazopelekwa huko chini kwenye kata, vijiji na vitongoji. Namuomba Mheshimiwa Ummy atupatie gari moja, Land Cruiser ya watumishi kufuatilia miradi na utendaji kazi wa watumishi kwani malalamiko ya wananchi ni mengi, ni vyema gari ikapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimkumbushe Mheshimiwa Ummy Mwalimu ahadi yake ya kumpongeza Nesi Zainabu, anayefanya kazi kwenye Zahanati ya Mwakizega kwa kazi nzuri hadi wananchi wakaandamana kumlilia Nesi Zainabu. Maana tangu mwaka 2017 hakuna motisha yoyote aliyopewa kwenye Halmashauri ya Uvinza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, niendelee kumpongeza mdogo wangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kwani ataacha kumbukumbu muhimu sana kwenye hii Wizara. Sote ni mashahidi, anafanya kazi yenye tija na kuridhisha sana. Baada ya pongezi naomba kuunga mkono hoja hii asilimia mia moja.