Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Ni ushauri wangu Serikali ione namna ya kuchukua ushauri wa hotuba hiyo ili kuboresha maendeleo ya Wizara nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, afya ni kitu muhimu sana kwa binadamu yeyote. Bila kuwa na afya bora, hakuna kazi au maendeleo hapa duniani au Tanzania. Hivyo basi, pamoja na mambo mengi yanayofanyika, bila afya bora ni mzigo mkubwa kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii inashughulika na wazee, watoto na wanawake ambaPo wanawake hao ni kiwanda namba moja cha kuleta watoto duniani. Nianze na kuzungumzia afya ya mama na mtoto ndani ya Jimbo la Mlimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwepo na Kituo cha Afya Kata ya Mlimba ambacho kinahudumia takribani wakazi wa kata 10 na watu wasiopungua laki moja na zaidi, inasababisha kituo hicho kuzidiwa na wagonjwa kwa upungufu wa madaktari ambapo wapo wanne tu na kufanya tatizo kubwa katika kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia dawa zinazopelekwa mara kadhaa hazikidhi haja kutokana na hadhi ya kituo kuhudumia watu wa kata 10. Hivyo tunaomba tufikiriwe kuongeza vituo vya afya ili kupunguza mzigo mkubwa katika Kituo cha Afya Mlimba. Naomba angalau tupate vituo vya afya vitatu ambapo kila kata tatu zitahudumiwa na kituo kimoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Jimbo la Mlimba liko kilometa 220 hadi kufika Hospitali ya Rufaa St. Francis na miundombinu ya barabara ni mbaya sana kwa barabara kutopitika kwa mwaka mzima, hivyo kuhatarisha maisha ya mama wajawazito na wagonjwa wanaopata rufaa, naomba tupate bajeti ya kutosha ili tujenge Hospitali ya Halmashauri ambapo kwa bajeti hii. Tumetengewa shilingi milioni 500 tu, ambayo itachukua muda mrefu ujenzi kwisha. Naomba tuongezewe hela ili tujenge haraka na kuokoa jamii ya Mlimba. Pia tunaomba gari la wagonjwa kwani gari lililopo ni chakavu na linaharibika mara kwa mara. Pia ahsante kwa kupeleka hela ya kuboresha Kituo cha Afya cha Mchombe.

Mheshimiwa Naibu Spika, wazee waishio vijijini wanashindwa kupata huduma kutokana na ukosefu wa vituo vya afya na kushindwa kupata huduma kwa sababu ya umbali wa kufikia kituo cha afya Mlimba.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alipotembelea Wilaya ya Kilombero, pamoja na mambo mengine, aliamuru watumishi/wauguzi na madaktari wote waliokuwa wanalipwa na Serikali katika Hospitali ya Rufaa ya St. Francis waondolewe na wapelekwe kwenye vituo au zahanati za Serikali. Uamuzi huo ingawa umefanywa kwa nia njema, lakini umesababisha upungufu mkubwa wa madaktari na wauguzi kwenye Hospitali hiyo ya Rufaa ambapo ni tegemeo kubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Kilombero, Malinyi na Ulanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nashauri uangaliwe upya uamuzi huo kwani Mheshimiwa Waziri alipoagiza waangalie upya gharama ya matibabu, waliitekeleza kwa kuwashirikisha wadau na kupunguza gharama za matibabu. Hivyo, tatizo lililopo ni upungufu mkubwa wa madaktari na wauguzi. Ni matumaini yangu kuwa atalichukulia hilo kwa umuhimu.