Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na kuwapongeza Mawaziri wote, Mawaziri wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya, wasitishwe na watu wanaowaambia wanavamia vamia. Wafanye kazi kwa kujiamini, ni Serikali yao, wawatumikie
Watanzania kama Mheshimiwa Rais John Pombe alivyowaaamini kuwapa Uwaziri huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kidogo kuhusu uchaguzi wa Zanzibar tarehe imetangazwa. Niwaombe Wazanzibari wote wasubiri siku ya uchaguzi iliyotangazwa wakapige kura. Acheni kuwatisha Watanzania, acheni kuwatisha wananchi na kuwajaza jazba ambazo hazina msingi wowote na baadaye mtatuhatarishia amani ya nchi yetu, tunaomba sana.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwa kweli hotuba ya Mheshimiwa Rais imesheheni mikakati ya kuijenga Tanzania mpya, imesheheni mikakati ya kuijenga Serikali ya Awamu ya Tano. Nampongeza sana Rais John Pombe Magufuli kwa hotuba yake nzuri kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisisite kusema tu, kwa kweli Mheshimiwa Magufuli amewashangaza Watanzania, kwa muda mfupi tu ameanza kutekeleza ahadi zake alizozitoa Novemba hapa Bungeni. Ni vyepesi sana kukosoa na kulaumu, lakini kwa muda alioanza kutekeleza ahadi, ahadi zenyewe ni kubwa sana, zinahitaji utaalamu, zinahitaji pesa, ameanza kuzitekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mtu amesema kwamba, mambo elimu bure ni double standard, siyo kweli, mwanzo ni mgumu. Mheshimiwa Simbachawene ametuambia, wamepata hesabu vibaya ya wanafunzi, lakini wanaamini watakwenda vizuri huko mbele. Tuwatakie kila la heri kwenye mipango yenu, tuwatie moyo, tumsaidie Rais wetu, tuwasaidie Mawaziri kuhakikisha Watanzania wanapata huduma alizozisema Rais wetu. Tunawatakieni kila la heri na Mwenyezi Mungu atawasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, niongee kidogo kuhusu maji. Niipongeze Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, ilituahidi maji ya Ziwa Victoria watu wa Tabora, iko kazini inafanya kazi vizuri na imeahidi kuanzia mwezi wa sita itaanza kukarabati maji kutoka Ziwa Victoria kuleta Tabora, tutafaidika sana. Nzega mpaka Tabora Manispaa vijiji 86 vitapitiwa, vitapata maji ya Ziwa Victoria. Niiombe Serikali yangu, iende na action plan yake isije katikati ikakatiza.
Tunaambiwa kufika 2019, Tabora tutapata maji ya Ziwa Victoria. Naiomba sana Serikali ya Awamu ya Tano ambayo tunaiamini, Serikali ya hapa kazi tu, 2019 itupatie maji ya Ziwa Victoria.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pale Tabora kwenye maji ya Igombe, tulikuwa na shida ya pampu, tulikuwa na shida ya machujio, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshatuletea sasa na tunategemea kupata lita milioni 30 za maji badala ya lita milioni ishirini nne ambazo
tunazihitaji. Tunaipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya na tunaomba wananchi wa Mkoa wa Tabora mwendelee kutuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, juzi kati hapa maji yalikatika tulipigiwa simu kama Wabunge, lakini tatizo kubwa ni umeme, umeme kwa kweli Tabora umekuwa na mgao mkubwa sana, lakini niwaombe wananchi wa Tabora mtulie. Tumepata mwarobaini wa umeme ambae ni Profesa Muhongo. Profesa Muhongo yuko kazini, ameingia juzi, atafanya kazi, tunamwamini sana na tunaamini baada ya muda mgao huu utapotea. Tunamwamini na tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu afanye kazi yake kama tulivyomzoea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara, kuna kilometa 80 ambazo tunaziombea lami, Mheshimiwa Rais ametuahidi kutuwekea lami. Tunamwomba Waziri husika aiwekee lami hiyo katika hizo kilometa 80. Sasa hivi barabara ya Itigi-Tabora hakuna mawasiliano, imekatika,
tunaomba pesa za dharura, magari yamekwama pale, watu wanazunguka Singida, hali ni mbaya, nauli ni kubwa, watu wanashindwa kusafiri kupeleka wagonjwa wao na kuwahudumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba sana Serikali, namwomba Waziri wa Ujenzi, tunaomba pesa ya dharura, tutengeneze madaraja hayo yaliyokatika Itigi-Tabora na pia tunaomba ufuatilie hiyo lami ya kilometa 80. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naongelea sasa suala la zima la reli. Hakuna Mtanzania wala Mbunge asiyejua reli ni uchumi, reli inaleta maendeleo, reli inapunguza bei ya bidhaa.
Tunashangaa kwa nini kila tukipanga masuala ya reli yanaishia njiani. Nashindwa kuelewa, naiomba sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, ihakikishe tunaboresha reli, ihakikishe reli hii inakuwa kama ni kitega uchumi cha Tanzania. Tukiboresha reli tutasafirisha mizigo ya Congo, Rwanda na Burundi. Nashangaa tatizo ni nini? Tunapata habari za mitaani kwamba kuna watu wenye malori wanatufanyia vitu fulani kiasi kwamba reli yetu isiendelee. Naomba sana kama hilo suala lipo basi liangaliwe na lichukuliwe hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vitu vinavyoudhi sana kwenye suala zima la reli. Reli ni mbovu kwa muda mrefu, matengenezo yaliyofanyika ni Dodoma mpaka Igalula tu, lakini Kaliua-Mpanda haijatengenezwa, Tabora-Mwanza, Tabora-Kigoma, Igalula-Tabora reli hii haijatengenezwa. Kuna kilometa 35 kutoka Igalula kwenda Tabora Manispaa, hali ni mbaya sana, tunaiomba sana Serikali iangalie suala zima la reli.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye reli kuna majipu ya kutumbuliwa, hii ndiyo kazi ya Mheshimiwa Magufuli na Mawaziri wake. Tunaomba sana, kuna watu wamepewa miradi ya kukarabati reli. Kwa mfano, kuna mradi wa kukarabati reli kuanzia Kaliua-Mpanda, kuna watu
wapo pale wanaikarabati hii reli, lakini reli hii toka imeanza kurabatiwa na watu wanaojiita ni Wahandisi waliostaafu, wana Kampuni yao inaitwa ARN, wanaikarabati bila kokoto bila chochote na mabehewa yanaendelea kuanguka na hakuna chochote kinachokarabatika.
Tunaomba sana hili ni jipu na Serikali yangu sasa hivi ina mpango mzima wa kutatua matatizo haya basi ikafanye.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mradi wa kukarabati reli ya Godegode. Godegode pale kuna watu wanakarabati reli kila mwaka, lakini ndiyo kuna ajali kila mwaka za treni, kwa hiyo, nashindwa kuelewa watu wanalipwa pesa za nini wakati ajali zinaendelea. Kuna Wamalaysia
walikuja kututengenezea injini zetu, injini zetu za muda mrefu zilikuwa mbovu, wametutengenezea injini, ni jambo jema, tunawashukuru kwa kututengenezea injini zetu, lakini kinachonishangaza, tuna mafundi wa railway, lakini bado hawaa Wamalaysia wanakuja kila mwezi eti kufanya service za zile injini. Kwa nini service hizi zisifanywe na mafundi wetu wa railway ambao wanalipwa mishahara na Serikali ya Chama cha Mapinduzi? Leo Wamalaysia wanakuja kufanya service kila mwezi, hili ni j pu Mheshimiwa Waziri tunakuomba sana uliangalie.
Kuna Injini 9010 mpya imenunuliwa kwa mamilioni ya shilingi. Juzi tu imeanguka Zuzu kwa sababu reli ni mbovu. Naumia sana kukwambia kwamba katika mabehewa mapya yaliyonunuliwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa gharama kubwa, mabehewa 70
yameshaanguka katika mapya na yako porini mpaka leo hayajanyanyuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri afuatilie mabehewa haya mapya yaliyoanguka huko porini na yarudishwe, yakarabatiwe ili yaendelee kufanya kazi. Mheshimiwa Naibu Spika, naongelea suala zima la wafanyakazi, wafanyakazi hawa
wanakatwa mishahara yao ya kwenda kwenye Mifuko ya Jamii mfano NSSF, lakini wanakatwa kupelekwa kwenye SACCOS zao, wanakatwa wale waliokopa NMB. Hata hivyo, makato haya hayapelekwi NSSF, hayapelekwi kwenye SACCOS zao, tunashindwa kuelewa pesa hizi
zimekatwa kwenye mishahara yao zinakwenda wapi. Naomba sana Serikali ifuatilie suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna afisa amezuka anaitwa afisa wa kumsindikiza dereva, afisa huyu anapanda pamoja na dereva wa treni, analipwa laki moja na nusu kwa trip, dereva halipwi hata senti tano, eti yeye anaangalia treni isikimbie. Treni isikimbie wakati tuna vituo?
Mheshimiwa Naibu Spika, inajulikana kutoka Dodoma mpaka Zuzu ni dakika fulani, akiwahi ataulizwa? Kwa nini awekwe mtu ambaye analipiwa pesa nyingi? Kwa hiyo, huu ni mpango wa wakubwa, tunaomba ukomeshwe mara moja na pesa hizi walipwe madereva.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumezuka utaratibu ambao siuungi mkono, anayekwenda kukata tiketi ya kuondokea treni anaambiwa aende na kitambulisho. Sisi wote hapa asilimia kubwa tumetoka vijijini, tunajua ndugu zetu wa vijijini hawana utaratibu wa kutembea na vitambulisho. Unakuta mtu amemleta stesheni moja ya Kintinku siku moja, anaumwa, wanamkatalia kumpa tiketi eti hana kitambulisho au anaambiwa aende na picha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine nitaandika kwa maandishi.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Munde, muda wako umekwisha.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Ahsante sana. (Makofi)