Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia kuweza kusimama hapa, na niwatakie heri na baraka katika mfungo wa mwezi wa Ramadhani wananchi wote wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kutoa shukrani na pongezi za dhati kabisa kwa namna Mheshimiwa Waziri, Naibu wake na Watendaji wake wanavyoisimamia Wizara hii, Wizara ambayo ni uhai wa Taifa la Tanzania, ni uhai wetu sote. Mimi binafsi hata kama sitasema hadhara, lakini kwa kusema kweli naikubali sana Wizara hii na Watendaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nianze kuhusu suala la wagonjwa wa figo, Mheshimiwa Waziri, binafsi anafahamu, mimi nimewahi kuugua ugonjwa huo, nimepitia mazito ambayo kwa kweli kati ya magonjwa mazito na magumu sana ni ugonjwa wa figo. Kwa hivyo ninapozungumza hapa nazungumza kitu ambacho nimekipitia, nakijua na naendelea nacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka Mheshimiwa Waziri, kuna jambo moja linatatiza sana wagonjwa wa figo, jambo hili ni upatikanaji wa dawa za wagonjwa wa figo, wagonjwa wa figo ambao wako kwenye bima, Watanzania wengi hali zao za kiuchumi ni za chini sana, wale walioko kwenye bima, hizo bima hata ukikata lakini kuna masharti ya kufikia kupata dawa za figo, yako masharti, mtu kawaida ukikata ile bima unaambiwa lazima ikae muda fulani iwe ndiyo inakuwa matured ya kuweza kupatiwa dawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna binadamu yeyote anayejiombea ugonjwa kumfika, kama imewezekana kwa wagonjwa wa UKIMWI kupewa dawa hizi pasipo na masharti na wagonjwa wa figo waangaliwe urahisi wa kuzipata dawa hizi. Kwa kweli, hili jambo ni la kuliangalia sana, pamoja na hilo Mheshimiwa Waziri anajua mgonjwa wa figo anapopata tu ugonjwa huu, akithibitika kuna hatua za kupitia wakati anasubiri upasuaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya uchujaji wa damu, huduma za uchuchaji wa damu, kwa mtu asiye na bima ya afya sasa hivi ni 180,000. Watanzania wa hali ya chini kwenda kupatiwa huduma hii kwa 180,000 kila siku anayokwenda kwenye huduma hii ni jambo zito na ambalo Watanzania wengi hawawezi kulimudu. Hili linapelekea vifo vyao kabla hata hawajafikia kwenye kufanyiwa transplant. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri, aliangalie hili sana, kwa sababu Watanzania wengi wasio na uwezo wanafikia, hawafikii hatua ya kutafuta ndugu kuwasaidia upandikizaji tayari wamekuwa wamekufa katika hatua ya kufanyiwa uchujaji wa damu dialysis, kwa hivyo naomba suala hili liangaliwe nalo kwa umakini sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo mimi ni mmoja wa wanachama wa Chama cha Wagonjwa wa Figo na wanachama wenzangu wamenituma hapa nilisemee hilo, kwa hivyo Mheshimiwa Waziri, naomba alichukue kwa uzito stahiki. Naongea kama Khatib na naongea kama mwakilishi wa wagonjwa wenzangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ninalotaka kulizungumzia, Mheshimiwa Ummy katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo lipo tatizo, lipo tatizo ambalo sasa ni karibu miaka mitano, tatizo la lift katika wodi ya Galanosi ambayo wazazi wanakaa kwenye ghorofa ya tatu, theatre room iko chini. Kinachotokea sasa hivi anapofanyiwa operation, akipelekwa kule juu lazima abebwe mzega mzega. Tanzania ya leo mgonjwa kubebwa kwenye machela akapandishwa kwenye ngazi hilo ni jambo ambalo halikubaliki. Akinamama hao, ambao wanajifungua kwa operation wako chini, akinamama hao Mheshimiwa Waziri ajue ndiyo wengine wanajifungua Marais, wengine watajifungua Mawaziri Wakuu, wengine watajifungua Waziri wa Afya kama yeye, wengine watajifungua wachungaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni vizuri sana Mheshimiwa Waziri jambo hili aliangalie na nataka nimpe rai, kwa sababu mimi ni mdau wa Tanga, mimi ni mpiga kura ambaye natokea Zanzibar lakini mimi ni mkazi wa Tanga na familia yangu yote. Namwomba sasa, kama hili jambo limekuwa zito na mwaka wa tano limeshindikana, tuna bahati sana Mkoa wa Tanga na Jimbo la Tanga Mheshimiwa Waziri wa Afya ni mtu wa Tanga; Katibu Mkuu wa Wizara hii ni mtu wa Tanga, Dkt. Chaula; yupo Mbunge wa Jimbo la Tanga Mheshimiwa Mussa Mbarouk na nipo Mbunge mimi kutoka Zanzibar, lakini ni mdau mkubwa wa Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri ahitishe harambee mimi na wenzangu niliowataja tuwashirikishe matajiri wa Tanga wapo pale wa kina RATCO, yupo pale Raha Leo, yupo Simba Mtoto, tuitishe na harambee kubwa ambayo itasaidia kuitengeneza lift ile ili wagonjwa wetu, akinamama wetu wa Tanga waepukane na adhabu ile. Namwomba sana Mheshimiwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)