Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii muhimu ya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na kutuwezesha kufikia mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani. Niwatakie Waislam wote kheri ya Mfungo wa Ramadhani hususani wananchi wa Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya chama changu chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwatumikia wananchi wa Tanzania. Uzalendo uchapakazi wake maono amejipambanua ni kiongozi makini na ni mfano wa kuigwa Mheshimiwa Rais endelea kuchapa kazi sisi Watanzania tuko nyuma yako na tunakuombea sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Afya dada yangu Ummy Mwalimu, Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndungulile, Katibu Mkuu bi. Zainab Chaula pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Afya hakika wanafanyakazi nzuri sana. Nimekisoma kitabu hiki cha hotuba ya afya kwa namna kilivyopangwa na kilivyochapishwa, inaonyesha viongozi wa Wizara hii wako makini sana nawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika afya ndiyo utajiri na afya ndiyo mtaji wa kila mwanadamu. Niipongeze sana Serikali kwa juhudi kubwa inazochukua za kuboresha huduma za afya nchini kote. Kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Singida ninaomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutupa zaidi ya shilingi bilioni 5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 11, katika wilaya zangu zote za Mkoa wa Singida tumepata Kituo cha Afya Mkalama, Iramba, Singida Manispaa, Singida Vijijini pamoja na Wilaya ya Manyoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Namshukuru sana Mheshimiwa Rais hakika uwepo wa vituo hivi vya afya umeokoa sana vifo vya akinamama na watoto. Lakini Sera ya afya inasema kwamba kila kata iwe na Kituo cha Afya, basi niombe pamoja na uwepo wa vituo hivi vya afya jiografia ya Mkoa wangu wa Singida ni ngumu sana niombe vituo vya afya viongezwe ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naishukuru sana Serikali kwa kutupa bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya, hospitali ya Mkalama na hospitali ya Singida DC. Sasa hivi ziko katika hatua ya ujenzi na mwaka huu pia katika bajeti hii tumepata hospitali kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ikungi naishukuru sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na pongezi hizi na shukrani hizi mkoa wangu wa Singida una changamoto lukuki katika sekta ya afya. Nikianza na hospitali ya Wilaya ya Manyoni, hospitali hii ilijengwa kama kituo cha afya mwaka 1971 na ni ya muda mrefu. Kwa hiyo, majengo ya OPD limeshakuwa ni finyu na dogo, wodi ya akinababa, wodi ya watoto, wodi ya majeruhi haiendani kabisa na idadi ya watu katika wilaya hii ya Manyoni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ifahamike kwamba wilaya ya Manyoni ipo katika barabara kuu ya Mkoa wa Singida na Dodoma na ajali nyingi zimekuwa zikitokea kwa hiyo inakuwa ni changamoto sana kuwahudumia wagonjwa au majeruhi inapokuwa majeruhi hawa ni wengi ninaiomba sana Serikali itupatie fedha ili tuweze kujenga hospitali mpya ya Manyoni itakayoendana sambamba na idadi ya watu kwa wilaya yangu ya Manyoni lakini pia vilevile iweze kutoa huduma bora zaidi za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia ni kuhusu hospitali yangu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, hospitali hii ina changamoto nyingi na hospitali hii ilianza kujengwa mwaka 2009 ni takriban sasa miaka tisa imepita hospitali hii haijakamilika lakini jambo kubwa la kusikitisha hospitali hii ya rufaa kwa mwaka wa fedha uliopita haijatengewa fedha zozote na inatoa huduma katika maeneo mawili ipo hospitali ya rufaa ambayo ni ya zamani, ipo katika Kata ya Ipembe, lakini pia hospitali ya rufaa ambayo ni mpya iliyoko katika Kata ya Mandewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa jambo hili linapelekea kwa kweli ugumu katika uendeshaji wa hospitali hizi mbili kwa wakati mmoja. Nimuombe Mheshimiwa Waziri najua ni msikivu na ananisikia ifike wakati sasa zitengwe fedha za kutosha ili kumalizia ujenzi wa hospitali hii.

Mheshimiwa dada yangu Ummy ninakuomba sana kwa kuwa sasa imepelekea bajeti ndogo ambayo tunaipata kulipia bili za maji, umeme, ulinzi na usafiā€¦(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili ilishagonga. Asante sana.

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nauunga mkono hoja. (Makofi)