Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia katika Wizara ya Afya ambayo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza kwa dhati Waziri wa Afya, Naibu Waziri, Katibu Mkuu kwa kazi kubwa anayofanya na hakuna mtu yeyote ambaye ana mashaka na uchapakazi wao. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka miwili iliyopita, nilisimama hapa Bungeni nikalalamika sana kuhusu ubovu wa X-Ray katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega ambapo kuna wakati fulani ilikuwa inachukua mpaka miezi sita X-Ray haifanyi kazi. Leo hii nasimama hapa kutoa pongezi za dhati kwa niaba ya wananchi wote wa Wilaya ya Nzega kwamba Serikali sasa imesikia kilio hicho na imetupatia X-Ray mpya kabisa ya kidigitali ambayo inafanya kazi kwa ufanisi na inatoa picha za ubora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya aananchi wa Nzega lazima niishukuru Serikali kwa kutupatia X-Ray hiyo mpya kabisa. Kwa hiyo, sasa hivi uchunguzi wa magonjwa unafanyika kwa usahihi na maana yake ni kwamba tiba itapatikana kwa usahihi. Ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Serikali. Nimeangalia ukurasa wa 54, kwa kweli kuna mambo makubwa ambayo sisi kama wawakilishi wa wananchi ni lazima tuipongeze. Kabla ya mwaka 2017, kuna matibabu makubwa ya kibingwa yalikuwa hayawezi kufanyika hapa nchini, lakini sasa yanafanyika. Kwa mfano, kupandikiza figo, jambo hili limeokoa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa kipindi hiki tu ambapo wagonjwa 38 wameweza kupandikizwa figo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna mambo makubwa yamefanyika. Kwa mfano, kabla ya mwaka 2017, hatukuwa na uwezo wa kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto wadogo. Hili ni jambo kubwa ambalo sisi wawakilishi wa wananchi tunatakiwa kutoa pongezi za dhati. Fikiria mtoto anazaliwa hawezi kusikia, lakini anafanyiwa operesheni, anawekewa vifaa vya usikivu, anaweza kusikia. Kwa hiyo, anaweza kufanya mambo yote ya kupata elimu na haki nyingine zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni jambo ambalo siyo dogo, ni kubwa na ninachukua fursa hii kuipongeza Serikali kwa kufanikisha jambo kama hili. Pia jambo kama hili linaokoa fedha nyingi ambazo zinatumika katika mambo mengine muhimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaungana na mapendekezo ya Kamati ya Huduma za Jamii. Ukiangalia ukurasa wa 20 mpaka 21, Kamati imeitaka Wizara ya Afya kuwaangalia kwa makini wahudumu wa afya katika ngazi ya jamii kwa sababu hawa wanasaidia sana katika kuhakikisha kwamba tunapata kinga na kila mmoja anajua kwamba kinga ni bora kuliko tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mapendekezo yote ya Kamati ya Huduma za Jamii yaliyo katika ukurasa wa 20 mpaka 21 ninakubaliana nayo kwamba Wizara ya Afya iangalie namna ambavyo itaweza kuwa-accommodate hawa wahudumu wa afya ngazi ya jamii ili tuweze kuhamasisha akina mama wakajifungulie kwenye zahanati, tuweze kuhamasisha matumizi bora ya vyoo, tuhamasishe unywaji wa majisafi na salama ili kuepuka magonjwa ambayo yanaweza yakasumbua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kuongelea ni uhaba wa watumishi hasa Waganga katika zahanati zetu. Ningependa Wizara ingetoa mwongozo wa kuhakikisha kwamba angalau katika kila zahanati kunakuwa na Mganga.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali ilivyo sasa hivi, kwa mfano katika Halmashauri yangu ya Nzega Vijijini, katika zahanati 39 tulizonazo, zahanati 12 hazina kabisa Waganga, zinaendeshwa na Ma-nurse. Jambo hili siyo jema kwa sababu tunapaswa tuwe na Waganga ambao mgonjwa akifika anahudumiwa, anakuwa prescribed na Mganga halafu ndiyo wanahudumiwa na Nurse.

Mheshimiwa Naibu Spika. Zahanati 12; Zahanati ya Mboga, Zahanati ya Semembela, Zahanati ya Nkindu, Ikindwa, Lakui, Mwangoye, Mwasala, Malilita, Uhemeli, Mirambo Itobo, Magengati na Shila; hizi zahanati hazina kabisa Waganga. Kwa hiyo, ombi na ushauri wangu kwa Wizara ni kwamba tuhakikishe kwamba zahanati hizi ambazo tayari zipo angalau zinakuwa na Waganga ili wagonjwa wakifika pale waweze kupata huduma za tiba za uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili litakwenda sambamba na Ilani yetu ya uchaguzi ambayo tunahimiza kwamba kila Kijiji kiwe na zahanati. Kwa hiyo, maana yake ni kwamba tunakwenda kujenga zahanati za kutosha nyingi. Sasa zahanati ili ziweze kufanya kazi, ni lazima ziwe na Waganga na Ma-nurse. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nawapongeza Wizara kwa kazi kubwa wanayofanya kuimarisha afya katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsanteni sana. (Makofi)