Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi na mimi pia niweze kuchangia Wizara hii ya Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Wabunge wenzangu kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri na kubwa ambayo anaifanya ya kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora katika eneo hili la afya ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze kiupekee sana Waziri wa Afya, dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu akisaidiana na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa kazi nzuri na kubwa ambayo wanaendelea kuifanya ya kuhakikisha sekta ya afya inaendelea kutoa huduma kama ambavyo imeahidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mtovu wa fadhila kama sitasimama hapa na kutoa neno la pongezi kwa Serikali hii kutokana na kazi kubwa ambayo wameifanya. Wananchi wa Jimbo la Nachingwea kwa sehemu kubwa wamekuwa wanapata huduma za afya katika hospitali kubwa ya Wilaya ambayo Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu mmetembelea mara kadhaa. Kwa kweli naomba nitoe neno la shukrani kutoka kwa wananchi wale kwa namna ambavyo mmejali kwa kuja kukagua mazingira, lakini pia kwa kusikiliza maombi mbalimbali ambayo tumeyatoa kwenu kama Wizara na kwa kweli mmetuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niliona nitumie nafasi hii kuwashukuru sana lakini bado tunaendelea kuwaomba yale ambayo tumeyaleta mezani kwenu basi muendelee kutuunga mkono ili wananchi wale waweze kupata huduma kama ambavyo tumeahidi. Hapa ninapozungumza sasa hivi, uko ujenzi wa Jengo la OPD kupitia shilingi milioni 400 ambazo zimetoka katika Serikali yetu. Lengo kubwa ni kuhakikisha huduma za afya kwa wananchi zinaendelea kuimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nishukuru wananchi wetu wamekuwa wanapata huduma pia katika Hospitali ya Rufaa pale Sokoine, Lindi. Hospitali ya Sokoine, Lindi sasa hivi ni kubwa na inatoa huduma katika maeneo mengi sana. Uboreshaji mkubwa umefanyika katika upatikanaji wa maji lakini pia uboreshaji wa mazingira yale ya hospitali ambayo wananchi wetu wengi wanaotoka katika Wilaya za Mkoa wamekuwa wanaenda pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu ambalo ningependa kuliwasilisha kwenu ni kutuongezea wataalam hasa madaktari bingwa katika hospitali. Madaktari hawa watakwenda kuhakikisha wananchi wanaotoka katika maeneo ya Nachingwea, Liwale na maeneo mengine hawaendi sasa Muhimbili badala yake huduma zote wanazipata katika hospitali ile ya Rufaa ya Sokoine ambayo Serikali imefanya kazi kubwa sana kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka nijaribu pia kutoa ushauri na kuomba watu wa Wizara, Mheshimiwa Ummy utakumbuka tulifanya ziara Naipanga. Naipanga ni sehemu ya Tarafa lakini idadi ya wananchi pale ni zaidi ya watu 14,000, umuhimu wa kujenga kituo cha afya na kwa ahadi ya Serikali nafikiri pia utakumbuka na Naibu wako Waziri Mheshimiwa Dkt. Ndugulile tulifanya ziara pale. Nawaomba sana hebu tufanye yale ambayo tuliwaahidi wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama wananchi wa eneo lile tayari tumeshaanza kufanya jitihada za kuhakikisha tunatenga eneo. Hata hivyo, kwa sababu lengo ni kupandisha hadhi ile zahanati iliyoko basi, naamini ahadi ile wakati mnaenda kuhitimisha basi hamtatusahau ili wananchi waweze kupata huduma pale wasitembee umbali mrefu wa kwenda Hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenda Hospitali ya Wilaya maana yake tunaweka wingi wa watu usiokuwa na ulazima. Kwa hiyo, ili kuepuka umbali lakini pia kuwasogezea wale wananchi huduma, naomba niwakumbushe kwa sababu ni eneo ambalo tayari wenyewe mmeshaona mazingira halisi ya pale na namna ambavyo wananchi wamekuwa wanapata shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kiko kituo kingine cha Marambo. Kituo hiki kiko ndani ya Tarafa pia ya Ruponda, idadi kubwa ya wananchi wanatembea umbali mrefu kwenda Hospitali ya Wilaya. Naomba kupitia bajeti hii na mikakati mingine ambayo mnaendelea nayo kama Wizara, basi muone umuhimu pia wa kutuunga mkono ili tuweze kupandisha na kuboresha kituo kile cha afya kiweze kutoa huduma kwa wananchi wote wanaotoka Ukanda wa Marambo. Kule watahudumia wananchi wanaotoka Mkoka, Marambo yenyewe, Chilola pamoja na maeneo ya jirani ambayo wananchi wamekuwa wanategemea kituo kile kwa ajili ya kupata huduma zote muhimu ikiwemo upasuaji pamoja na kupata tiba nyingine muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo niliona pia nilizungumze, ndani ya Wilaya ya Nachingwea tuna kituo cha Mission cha Mnero. Kituo hiki ni cha zamani kidogo na kinahudumia wananchi wanaotoka Tarafa ya Ruponda. Kwa muda mrefu kituo hiki huduma zake zimekuwa za kusuasua. Tunashukuru Serikali kwa sababu imekuwa inapekeleka Busket Fund ingawaje siyo fedha ya kutosha sana lakini jitihada zozote zitakazofanyika za kuhakikisha kituo kile kinapatiwa fedha za kutosha naamini kitaenda kuondoa uwingi wa watu wanahitaji huduma katika Hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri, pamoja na watalam wako hebu nawaomba sana pamoja na mikakati mingine mnayoendele a kuifanya, hebu tukiangalie kituo hiki ambacho kwakweli kinatusaidia sana sambamba na kituo kile cha Ndanda ambacho nacho pia kinafanywa kwa mtindo huo kwa sababu kiko chini ya Mission lakini bado mkitoa fedha za kuhakikisha huduma zinapatikana katika maeneo haya basi wananchi wetu wengi wataenda kunufaika na huduma bora ambazo zitaenda kutusaidia kuondokana na kero za wananchi kukosa huduma bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nikuombe Mheshimiwa Waziri, bado tunachangamoto ya huduma ya magari kwa ajili ya kusafirishia wagonjwa. Kwanza katiak hospitali ya wilaya bado ambulance tuliyonayo ni moja, haitoshelezi mahitaji hivyo tunalazimika kuchukua magari mengine nje ya ambulance kwa ajili ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunacho kituo cha afya cha Kilimarondo ambacho ninaishukuru Serikali imetupatia milioni 400 kituo kimekamilika lakini bado tuna changamoto ya kupata gari ya wagonjwa na ni umbali wa zaidi ya kilometa 120 ambayo wananchi wale kwa kukosa gari wamekuwa wanapata changamoto kubwa kwa muda mrefu. Kwa hiyo, ninaomba pamoja na kazi nzuri iliyofanyika, bado nilete maombi kwenu watu wa Wizara muweze kutusaidia katika mgao wa magari basi maeneo haya mawili yapate magari ya wagonjwa ili wananchi waweze kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)