Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Janeth Maurice Massaburi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuweza kuchangia katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai ambayo amenijalia na kuniruhusu leo hii kusimama na kutoa mchango wangu kwa maslahi ya taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Ummy, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Watendaji wote wa Wizara na madaktari na wauguzi wote nchini kwa kazi nzuri na njema na takatifu wanayoifanya kuhakikisha afya za Watanzania zinaimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu aliumba mbingu na nchi, naomba ninukuu Biblia, Kitabu cha Mwanzo, kinasema: “Mungu akasema, iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza”. Mwisho wa kunukuu. Maana yake ni nini? Mwenyezi Mungu alifanya tathmini ya uumbaji wake hatua kwa hatua. Hata alipomuumba mwanadamu, alimuumba mwanaume kisha akatathmini akamuumba mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Watanzania wenzangu tufanye tathmini ya kazi kubwa inayoifanywa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimwa Dkt. John Pombe Magufuli akisaidiwa na Mawaziri, Makatibu Wakuu, watendaji na madaktari na wauguzi hapa nchini. Mabadiliko makubwa yamefanyika kusema ukweli, mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini asilimia kubwa hata na ndugu zetu hapa wanaamini na wanatambua amefanya kazi kubwa lakini haya huwa wanafanya tathmini wakiwa wamejifungia kwenye vyumba vyao. Hapa ni kawaida kwa sababu hata kwa Mungu pia kuna viumbe ambao hawamuungi mkono Mwenyezi Mungu, ni kawaida hiyo.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JANETH M. MASABURI: Hebu nyamazeni pale.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JANETH M. MASABURI: Mmeipata hiyo, katika kipindi hiki cha uongozi Awamu ya Tano chini ya jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ameidhihirishia ulimwengu na hata mataifa yanapongeza juhudi na kazi kubwa anayofanya, ni lazima tuseme. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Taasisi ya Jakaya Kikwete imefanya kazi kubwa sana chini ya uongozi wa Dkt. Janab, Dkt. Kisenge na madaktari wengine ambapo kwa sasa kwa asilimia 85 huduma za moyo zinafanyika nchini. Mtakumbuka siku za nyuma Watanzania wengi walikuwa wanachangiwa kwenda kupata matibabu nchini India, sasa hivi hiyo ni historia ni lazima tupongeze Serikali hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali ya Muhimbili inaendelea kufanya kazi vizuri na wameboresha maeneo mengi hata kule ndani ukienda utatambua ni hospitali ya taifa. Taasisi ya Mifupa (MOI), inafanya vizuri. Taasisi ya Ocean Road inafanya vizuri. Hospitali ya Mlonganzila inafanya vizuri. Hospitali ya Benjamin Mkapa inafanya vizuri na hasa katika magonjwa ya figo. Hivi karibuni tumeambiwa kwamba hata viongozi na baadhi ya Mabalozi wamekuja kutibiwa katika hospitali zetu, haijapata kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nauliza ni lini tutawapa tuzo madaktari wetu, tuwatambue kwa kazi njema wanayofanya. Tusingoje mtu akifaa ndiyo tunaanza kusema maneno mengi. Tuwatambue kwa kazi njema wanazofanya za kuokoa uhai na hasa madaktari bingwa, tuna madaktari wengi sana wanaofanya vizuri. Nitatoa mfano, tuna Profesa Janab, Profesa Mseru na madaktari bingwa wengine, Dkt. Magandi, tuna wataalam wengi sana hapa tunaomba tuwatambue hata kwa kuwapa tuzo. Mheshimiwa Ummy nakuomba Wizara ifanye mchakato wa kuwatambua madaktari na wauguzi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha hospitali za Wilaya. Hivi karibuni tumepata taarifa wamejenga vituo vya afya 352 katika kipindi kifupi sana, haijawahi kutokea na itaendelea kuwauma sana. Hospitali mpya za Wilaya 67 zimejengwa katika Mikoa ya Simiyu, Geita, kazi nzuri imefanyika katika sekta ya afya. Kwa sababu inauma na mnatambua kwamba kazi njema imefanyika na majibu tunayo, Chama cha Mapinduzi kimeendelea kuielekeza Serikali kutimiza haja ya Watanzania na hasa walio wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kutambua kwamba kinga ni bora kuliko tiba. Taasisi ya Chakula na Lishe kama itawezekana iundiwe Wizara yake au itengewe fedha za kutosha ili kuweza kuhamasisha wananchi wajue jinsi ya kula chakula bora, kufanya mazoezi ili kuzuia magonjwa mengi ambayo siyo ya lazima. Magonjwa haya yanailazimu Serikali kutumia fedha nyingi sana. Kwa hiyo, kinga ni bora kuliko tiba, nakuomba Mheshimiwa Waziri hili ni jambo la muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati fulani nilibahatika kwenda China katika Mji wa Shanghai, nilikuta kuna wazee wanakaribia miaka 80 mpaka 90 lakini wako mtaani wanafanya kazi na wana nguvu. Hiyo yote inatokana na ulaji wenye kuzingatia ubora wa chakula na mazoezi. Hiyo inasaidia hata kupunguza gharama za matibabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwaambia Waheshimiwa Wabunge tufanye mazoezi na wenye Gym wengine hapa wanapiga debe. Pia tuzingatie kula kwa wakati chakula bora na kulala mapema, yote ni katika kuzuia maradhi mengine yasiyokuwa na lazima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kuwapongeza madaktari wote nchini. Kusema ukweli wanafanya kazi njema na kazi ya Mungu, wanafanya kazi ya wito. Mimi nasema daktari hana tofauti na Mchungaji, Askofu au Shekhe, wanafanya kazi ya kumsaidia Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, naiomba Serikali iwaangalie, kuwaheshimu, kuwajali na kuwathamini madaktari wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nikupongeza Mheshimiwa Waziri na timu yako, Mwenyezi Mungu azidi kukulinda. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kukuteua mwanamke hodari na Naibu wako mmefanya kazi nzuri ya kutuongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)