Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini pia niungane na Wabunge wenzangu kwamba sasa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya. Pia, nampongeza kaka yangu Katibu Mkuu wa Wizara hii, Profesa Kitila Mkumbo na watendaji wake wote kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza mazingira bila kutaja uhifadhi wa vyanzo vya maji, maana yake mazingira yatakuwa hayajatimia. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge na ni ukweli usiopingika kwamba wameongea kwa hisia kubwa sana juu ya uhitaji wa maji na hili ni jambo jema sana. Mjadala huu unatuonesha picha ni nini ambacho Serikali tunapaswa kukifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna vita itatokea duniani leo itakuwa ni vita ya kugombania maji. Kwa bahati mbaya sana Tanzania inaweza ikawa nchi ya kwanza ya kuathirika na vita hii. Kwa nini? Asilimia 35 ya maji safi na salama duniani yanapatikana Tanzania. Tunayo maziwa makubwa, tunalo Ziwa Viktoria, Ziwa Tanganyika na maziwa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa inayojitokeza hapa ni namna ya kuhifadhi vyanzo vya maji na hili ndiyo jukumu letu. Hata kwenye mjadala ukiusikiliza, wote tunazungumzia water supply. Sasa una-supply water wakati unajua kabisa hujahifadhi vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niliseme hili kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kwamba jukumu la kuhifadhi vyanzo vya maji ni jukumu la kila Mtanzania, siyo jukumu la Serikali peke yake. Eneo hili linahitaji tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunahifadhi vyanzo vya maji ili tuweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imejitahidi sana kupeleka fedha za kutosha, inapeleka fedha za mradi, lakini mradi kwenye maeneo mengine hata kwangu kule Singida wanaenda kluchimba wanakosa maji na geological physical survey imefanyika inaonesha kwamba hapa kuna maji. Watakapochimba tu wakaenda hata mita 200 wanakosa maji. Hapo ndiyo kwenye changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayojitokeza hapa ni uhifadhi wa vyanzo vya maji ambalo hili ni jukumu letu kuwaelimisha watu wetu, tukirudi kuitaka Serikali itupatie fedha za miradi, tuwe tumetoa elimu ya kuhakikisha watu wetu wanajua namna ya kuhifadhi vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirudi nyuma mwaka 1961 Watanzania walikuwa takribani milioni 10, ukiweza kugawa unapata mita za mraba kama 7,862, lakini leo milioni 55 Watanzania mita za mraba unapata kama 2,300. Vyanzo vya maji ni vilevile na vingine toka mwaka 1961 vimeshakufa na leo vyanzo vinaendela kufa. Maana yake tunakoelekea ni kwenye vita kubwa ambayo tutashindwa kukabiliananayo. Vita hii inatuhitaji sisi wote Watanzania tuungane kwa pamoja, tusiiachie Serikali peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya ziara kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuangalia vyanzo vya maji vya mito mikuu mitatu; Mto Luengo nimeenda kule Namtumbo, nimepanda ile milima zaidi ya kilometa 10, nimeenda kuona chanzo cha maji. Kwenye chanzo cha maji pale hakuna tatizo, lakini inapoanzia pale kwenda maeneo mengine, maji kote njiani Watanzania wanafanya shughuli za kibinadamu na eneo hilo lote wame-tap maji wanayatumia kwa wingi kiasi kwamba maji yale kule yanakotoka mpaka yanakofika, yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Mto Ruaha Mkuu kuna shida kubwa sana. Watu wamevamia kwa kiwango kikubwa. Hili ni eneo ambalo tunahitaji sisi Watanzania tushirikiane kwa pamoja kulisimamia. Hivi vyanzo vya maji tusipovisimamia hapa tutakuja kudanganyana. Tukizungumza lugha ya water supply peke yake na Serikali kweli ikawa na fedha ikapeleka, unapeleka fedha unaenda kuchimba maji wakati hayapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mazingira nilitaka niwaombe Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kwa pamoja. Tunayo fursa na tunayo nafasi kwenye mikutano yetu ya Majimbo ya kuwaeleza Watanzania kwamba tunahitaji kutunza vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado kuna fedha ya miradi mbalimbali inayopelekwa na Serikali kwenye Halmashauri zetu. Tusiposimamia kuanzia hatua ya kwanza mpaka ya mwisho na baadaye tunaenda; hapa umesikiliza mjadala wa Waheshimiwa Wabunge, mijadala mingi inasema mradi umeenda umeisha, shilingi milioni 500 zimeenda, lakini hakuna maji. Jukumu ni la nani? Wizara imepeleka fedha. Fedha tunatakiwa tuzisimamie sisi, ndiyo wajibu wetu na kuwaelimisha watu wetu. Kamati za Maji zishirikishwe kuanzia initial stage. Hili ni jukumu letu kule chini. Hili eneo nilitaka niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tusibaki tu kulalamika na tukaiachia Serikali ikasimamia mpaka kule chini. Huu ni wajibu wetu na hatuwezi kurudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine Serikali imeweka mkakati mzuri sana. Yako maeneo iko miradi ya nyuma ambayo tayari miradi ile ime-collapse kwa uzembe wa watendaji na kwa uzembe wa kutokushirikisha jamii. Mkakati huu uliowekwa uwe mkakati ambao unahitaji na sisi kushiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo la mita 60, mita 500 limezungumzwa; eneo hili sisi kwenye Sheria yetu ya Mazingira mwaka 2004 kifungu cha 57(1) kimezungumza mita 60, lakini kifungu cha 57(2) kimeeleza ufafanuzi kwamba Waziri anayo dhamana ya kutengeneza kanuni za mita 60 itumikeje. Nataka niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba kanuni tayari zipo na hazielekezi moja kwa moja, kila mazingira yana tofauti yake; kuna eneo ambalo halihitaji mita 60, mengine yanahitaji mita 10 tu, tukapanda miti mita 10 kuhifadhi kile chanzo cha maji lakini mita zingine wakaweza kuzitumia ama mita 20. Kanuni tumeziweka wazi na hatuna muda mrefu kanuni hizi zitafika mpaka kwenye Local Government kuhakikisha kwamba suala hili linaweza kusimamiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo mengi tunaweza kuzungumza juu ya uhifadhi wa maji, maeneo haya yote hasa visima ukizingatia visima hivi ambavyo vimechimbwa na wadau mbalimbali; mdau akishachimba kisima watu wanaamua kuacha kiendelee. Jukumu la kutunza visima na jukumu la kutunza vyanzo vya maji ni jukumu letu sote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na haya ya kuweza kushauri/kuwashauri wenzangu na kuunga mkono bajeti. Nampongeza sana Mheshimiwa Profesa na Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)