Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja hii ya asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mungu kwa nafasi hii, lakini nawapongeza Wizara ya Maji. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa Mbarawa, nampongeza Naibu wake kwa kazi nzuri wanayofanya, pia nawapongeza watendaji wote wakiongozwa na Katibu Mkuu, Profesa Kitila Mkumbo kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Kwa kweli, maji ni uhai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu sisi katika Wizara ya Ujenzi tunapokuwa na miradi ya ujenzi wa barabara, tunahitaji kutumia maji kwa wingi. Kwanza sisi wenyewe kama sehemu ya kukamilisha miradi tunatumia maji, tunahitaji maji ya kutosha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapojenga barabara, madaraja makubwa, madaraja madogo, ma-calavat; pia tunapotengeneza madaraja haya ili kuweza kupitisha maji, maana iko mito midogo, mikubwa na iko mito ya msimu na ambayo inapitisha maji muda wote, tunahitaji maji katika kazi ya ujenzi kwa wingi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ili kushindilia barabara zetu zikae vizuri, maji yanatumika; ili kuweka zege katika maeneo mbalimbali, maji yanatumika; ili kuhakikisha kwamba barabara inakuwa stable, tunafanya curing kwa maana kwamba tunamwagilia maji na maji yanatumika kwa wingi sana. Kwa hiyo, upatikanaji wa maji huwa ni kigezo cha kupunguza au ku-control gharama za ujenzi wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukifanya shughuli za ujenzi wa barabara huwa tunawaelekeza makandarasi waweze kutengeneza au kujenga mabwawa ya kuhifadhi maji ili kukidhi mahitaji ya shughuli za ujenzi. Kazi hii ikikamilika, mabwawa haya hubaki na maeneo mengi tunatumia mabwawa haya yaliyobaki baada ya shughuli za ujenzi kwa shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi. Kwa hiyo, muda wote tunahitaji ku-manage maji ili tuweze pia kupunguza shida kubwa ya maji ambayo tunayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo ambayo pia tunachimba vifusi, tunachimba udongo ili kuweza kukamilisha shughuli za ujenzi wa barabara na baada ya ujenzi kukamilika na sisi kama Wizara hutoa mchango mkubwa wa kuhakikisha kwamba maeneo haya, hizi ball pits tunazifanyia marekebisho makubwa, tunazichonga vizuri ili ziweze kutumika kwa maeneo ambayo mahitaji ya maji ni makubwa sana. Kwa hiyo, huu utaratibu tunaufanya ili na sisi kutoa mchango katika kuhakikisha kwamba maji haya na hizi pits zinazobakia zinaweza kutumika kwa ajili ya kutoa huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme mbele ya Bunge lako hili kwamba uko uwezekano mkubwa wa kwamba sisi kama Wizara pale tunapotambua kuna mahitaji ya maji kwa wingi kiasi gani katika maeneo miradi ya barabara inapita tunazingatia kuanzia kwenye hatua ile ya usanifu tunaweka provision ili nasi tuweze kutoa mchango kwenye maeneo ambayo miradi ya barabara inapita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba sehemu ambayo tutakuwa na miradi kuanzia kwenye hatua ya usanifu watoe ushirikiano, watupe taarifa, lakini ninajua pia wako wadau wengine katika maeneo yetu, wakurugenzi na wananchi wenyewe wakitupa taarifa ili na hii fursa tuweze kuitumia na sisi kuendelea kupunguza adha ya maji ambayo yanahitajika kwa ajili ya shughuli za kibinadamu mbalimbali, shughuli za kilimo na pia kwa ajili ya kunyweshea wanyama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mifano ya miradi ambayo kwa ufupi tu niitaje. Baada ya miradi ya barabara kukamilika tumeacha huduma za maji kwa ajili ya kumbukumbu. Ukiangalia barabara ya kutoka Tabora – Puge kwenda Nzega yako maeneo mengi ambayo tumeacha mabwawa na sehemu nyingine tumeweka huduma ya maji. Barabara hii kutoka Nzega – Tinde kwenda Shinyanga kadhalika tunayo mabwawa ambayo yamebakia kandokando ya barabara, tunaendelea kuhudumia maji; barabara hii kutoka Nzega – Igunga – Shelui na penyewe yako maeneo ambayo tumeweka huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa maeneo pia ambayo yanazunguka kwenye Mji huu wa Dodoma kwa Barabara ya Dodoma – Manyoni – Singida, yako maeneo ambayo yanahudumia wakazi wa Dodoma na wakazi wengine wa Singida, tumeacha mabwawa ya maji. Ukiangalia pia, hata barabara kuu kutoka hapa Dodoma kwenda Morogoro, Dodoma – Kondoa – Babati, Dodoma – Iringa yako maeneo ambayo tumeweka huduma za maji. Kwa hiyo, nilitaka niseme tu kwamba fursa zipo kila wakati tupate hizi taarifa kuhusu mahitaji sahihi ya watu na sisi tutaendelea kutoa msaada wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunachimba visima kama sehemu ya social responsibility. Uko mfano, ukienda Kaliua kule kuna visima vitano tumechimba. Pia viko visima vingi kwa sababu, miradi ya barabara ni mingi, yako maeneo mbalimbali ambayo kama sehemu ya social responsibility tunatoa huduma kupitia wakandarasi wanaofanya shughuli hizi ili kuweza kutoa mchango mkubwa kwenye huduma za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja zilitolewa hapa kwamba maji yanapotea katika maeneo mbalimbali. Hii ni kweli, tunapokuwa tumetengeneza ma-calavat na madaraja madogo, madaraja makubwa na pia kwenye hizi ball pit kuna maji yanapotea, kwa sababu, hatujajipanga vizuri kuhakikisha kwamba tunayatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kutumia maji haya, siyo kazi ya Serikali peke yake, ni kazi yetu sisi wote. Wote tunao wajibu wa kushirikiana kuhakikisha kwamba tunayazuia maji haya yanayopotea kwa kiasi kikubwa kuliko maji yapotee halafu wananchi wana shida ya maji. Tukishirikiana kwa pamoja tutawahudumia vizuri wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwasihi na kuwaomba Waheshimiwa Wabunge na kwa sababu pia, ziko mamlaka, TANROADS inajenga barabara, TARURA tunajenga barabara, lakini pia iko fursa ambayo tumepewa kupitia Bodi zetu za Barabara katika mikoa ambapo Waheshimiwa Wabunge ni Wajumbe; Wakuu wa Wilaya ni Wajumbe; wako pia Wenyeviti wa Halmashauri zetu za Manispaa na Majiji nao ni Wajumbe kwenye bodi hizi za barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Waheshimiwa Wabunge tunapokuwa tunashiriki kwenye vikao hivi, basi mahitaji yetu, mipango yetu tuiweke kwenye bodi hizi ili nasi tuwe na sehemu nzuri ya kuchukua mahitaji haya. Kwa sababu kama nilivyosema, fursa ya kuendelea kutengeneza mabwawa haya yawe makubwa kulingana na mahitaji, nasi kama Wizara, uwezekano wa kutoa huduma hii ya maji upo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane ili sasa tukishatambua mahitaji yetu, kuliko kuyaacha maji yapotee, tunaweza sasa tukayatumia haya maji ili kuweza kuwahudumua wananchi sehemu mbalimbali. Kwa sababu tukiacha maji yakaenda, kwanza yanapotea bure, lakini tusipoya-manage pia yanaharibu makazi ya watu, yanaharibu mashamba na hata barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukiona kama kuna vitu ambavyo vinahitaji na sisi tuvijue tuweze kuyatumia vizuri haya maji, nawaomba wote tushirikiane na wananchi, Waheshimiwa Wabunge na viongozi mbalimbali kwenye maeneo yetu tuweze kupata taarifa hizi ili sasa maji haya yaweze kutusaidia kuendesha shughuli mbalimbali za kibinadamu, yatumike kwa ajili ya mifugo na shughuli nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa na hayo kwa ufupi. Naomba sana katika hatua zote, kuanzia hatua za usanifu, pale tunaposanifu barabara huwa tuna-involve watu walio kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo, hata tukiona kuna mradi wa usanifu unaendelea na kama tuna mahitaji ya maji, ni hapo naomba sasa tushirikiane ili mtuletee sasa mahitaji haya kwa pamoja tuyaingize kuanzia kwenye hatua za mwanzo ili saa hizi facility za mabwawa na sehemu ambazo maji yanapita na sisi mchango wetu uwe mkubwa kuhakikisha kwamba tatizo hili kubwa ambalo Mheshimiwa Profesa Mbarawa hapa anapambana nalo kupunguza shida ya maji, nasi kama Wizara ya Ujenzi tuko tayari kushirikiana na Wizara ya Maji ili kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge ili maeneo yetu ambayo yana-demand kubwa ya maji na sisi kama Wizara ya Ujenzi tuendelee kutoa mchango wetu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja iliyo mbele yetu asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)