Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi nami siku ya leo nichangie hoja hii. Kwanza naomba uniruhusu niwapongeze kwa kweli Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Watendaji Wakuu kama Katibu Mkuu wanavyofanya kazi kwenye Wizara hii ya Maji, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mdogo naomba tu nijielekeze moja kwa moja kwenye maeneo ya wakandarasi. Jimboni kwangu kwa kweli kuna miradi mitano, miradi hii yote kwa kweli mpaka sasa haifanyi kazi mmoja walau una afadhali. Kwanza nimshukuru Naibu Waziri amefika kwenye Jimbo langu na ametembelea miradi hii ameona mwenyewe kwa macho yake. Kwa hiyo ninapozungumza nina hakika anajua nazungumzia nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Harsha, umesanifiwa 2012, hadi leo haujakamilika, wamejenga matenki, wameweka maeneo ya kujichotea maji lakini kwa kweli wananchi sasa wameduwaa, wanazidi kusubiri, hakuna maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mradi wa Tumati - Mongahay uko palepale. Nimesoma bajeti ya Mheshimiwa Waziri aliyoiandika humu na nimesoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hakika nachelea kusema tuna hali mbaya kweli kweli. Nimeleta maswali si chini ya 13 humu ndani ya Bunge, nimepata majibu, lakini miradi hii bado haifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe kwa sababu kinachoonekana hapa tunalo tatizo kubwa la fedha na ukiangalia sasa kwa muda huu ambao mkandarasi amefanya kazi na hakulipwa, tumeshavunja mkataba maana yake mkandarasi huyu amekwishaondoka site, hayuko tena site. Nimwombe Mheshimiwa Waziri pamoja na Wakuu wake wa vitengo waangalie jinsi ambavyo wakandarasi hawa wamepewa hizi tender na hawa wanaopewa tender waangalie basi, nakumbuka kwenye hotuba ya mwaka jana alituahidi hapa kwamba wataunda tume ambayo wao wenyewe kama wataalm watakwenda kuhakiki na kuangalia miradi nchi nzima na nilitegemea basi watakuwa wamefika Jimboni kwangu Mbulu Vijijini, lakini hilo sidhani kama limetokea na kama limetokea basi Waziri atakuja kuniambia wakati anahitimisha bajeti yake hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ukiangalia tatizo lilloko katika maeneo yetu pamoja na wakandarsi kuwa na matatizo lakini shida ya ulipwaji wa certificate ambazo kimsingi zinakaa sana Wizarani, kama kuna Wizara nimetembea, nimeenda ofisini, nimetembea mno, nimeonana na wataalam wote, nimejitahidi kweli kweli, mara nyingi pia nimejaribu kwenda na Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri, lakini pamoja na kusumbuka kote huku miradi hiyo bado haina namna ya kumsaidia mwananchi. Kwa hali hii katika jimbo langu lazima niseme ukweli, ni ngumu kusema kwamba unaweza kumtua mama ndoo kichwani, kwa kweli hili halipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe ndugu yangu Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba amekuja na ameona pale Haidom, ameagiza kisima kichimbwe na juzi tarehe ya 25 nimeuliza swali la nyongeza hapa na akaagiza DDCA wachimbe visima, hali ni mbaya naomba kabisa waone namna ya Wizara watakavyosaidia Jimbo la Mbulu Vijijini kutokana miradi hii ambayo imekuwa viporo, wameshaacha certificate, zimeshakaa kwenye Wizara, lakini kubwa zaidi miradi mingine miwili wakandarasi wameshatengua mikataba, kwa hiyo hawafanyi kazi tena na tumetangaza tender. Naomba basi katika bajeti ya mwaka huu apeleke fedha ili hawa wakandarasi wanaoomba tena miradi hii waweze kuendelea kwa sababu bila fedha hakuna kinachotendeka. Kubwa zaidi niombe pia hawa Wahandisi Washauri wanaokuja katika miradi hii, nishauri tu watumie tena utaalam wao ili waweze kushauri miradi hii iishe vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo hali hii ya hao Wahandisi Washauri inawezekana huenda taaluma zao siyo sawa, waangalie kwa wana-design miradi ambayo haiishi na shida ni nini? Tujue, lakini kubwa zaidi nashauri kwa mfano Mradi wetu wa Haydom umekaribia kumalizika, tumepeleka maombi Wizarani tuumalizie sisi kama halmashauri kwa kutumia Force Account kwa sababu sheria inaruhusu na inasema mradi unaweza kutumia Force Account yaani bei ya soko na sisi tukajenga tukaumalizia kuliko kuweka tena mkandarasi kwa sababu tuna uwezo wa kufanya hivyo. Mabomba yako tayari, maeneo mengi yamekwishamalizika, watuache sisi tumalizie, tumepeleka Hadidu Rejea na iko Wizarani kwa Waziri aangalie namna yoyote, nafikiri wananisikiliza, ni hela kidogo tu ni milioni isiyopungua 70, tunaweza kumaliza sisi wenyewe watuachie na mimi nina Injinia ambaye kimsingi amekuja, watuachie tumalize kwa kutumia Force Account…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKIITI: Ahsante sana.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba tu niunge hoja mkono, lakini kwa masikitiko makubwa sana. (Makofi)