Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Edwin Mgante Sannda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kondoa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. EDWIN M. SANNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii ya kuchangia Wizara ya Maji, Wizara muhimu kabisa. Kwanza niwapongeze Wizara, Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wengine wote kwenye Wizara hii kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya na ukiona kama kilio ni kikubwa hapa si kwamba kazi hawafanyi, kazi wanafanya lakini bado uhitaji ni mkubwa kweli kweli, tunawashukuru sana na tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambazo anaendelea nazo na usimamizi mkubwa wa hata Wizara hii iliyo chini yake na Wizara nyingine zote, mambo mazuri yanaendelea na nchi naona kabisa kwamba sasa mwelekeo tunaokwenda ni mwelekeo umenyooka, mwanga unaonekana kule mbele kwamba Tanzania mpya sasa inaonekana. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye Wizara yetu hii ya Maji na mahitaji na changamoto ambazo tunazipata pale Jimbo letu la Kondoa Mjini. Toka nimeanza 2015 au tuzungumzie 2016 mwanzoni mpaka leo tunavyozungumza tulikwishaidhinishiwa fedha kiasi cha bilioni 3.7 na mpaka sasa ambazo zimekwishaingia, zimelipwa kabisa ni bilioni 2.5, hizo tayari kabisa zilishapokelewa, bado kuna kiasi kidogo cha kuwalipa makandarasi. Hapa tumechimba visima 10 ambavyo kati ya hivyo vingine vilikwenda Kata za Mjini ambazo ziko kama tatu, kata ambazo ziko pembezoni ni kama nane hivi na kwenyewe tumesambaza kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katikati Mji kwenye kata tatu, mwanzo tulikuwa tunategema maji ya chemchem ya asili, kulikuwa na tatizo kubwa sana, tukaamini na fedha hizi zote ambazo zimeingia kule kwetu basi tatizo la maji litapungua kweli kweli kwa sababu pale katika kwenye hizi kata tatu tumechimba visima vitano ambavyo vimeenda kuongezea upatikanaji wa maji ambavyo vinaenda ku- compliment ile chemchem. Hata hivyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri, leo tunavyozungumza bado kilio ni kikubwa kweli kweli cha tatizo la maji pamoja na kwamba tuna visima vipya vitano na vimesambazwa pale Kwapakacha, Kilimani, Tura, Tumbelo na maji yamesambazwa Wisikwantisi lakini bado huu mzigo wote tulitegemea sasa ule mzigo uliokuwa ukienda chemchem ungepunguza uhitaji basi hii mitaa mingine ibaki ina maji ya kutosha lakini sivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni nini? Inaonekana liko tatizo la wazi kabisa katika utekelezaji wa hii miradi kwamba labda zile design zinazofanywa za usambazaji, idadi ya matenki, urefu wa mabomba , idadi ya vizimba, huenda kuna tatizo wakati wa design, wasanifu wetu wanapofanya kazi inabidi Wizara isimamie kwa karibu sana kuona design hizi ni efficient na zitakuwa effective, sasa hebu fikiria bilioni 2.7 imeingia na bado kilio cha maji kipo kikubwa Mitaa ya Mnarani, Miningani, Ubembeni, Maji ya Shamba ambapo ndio mjini katikati, kilio ni kikubwa kweli kweli. Hapa nimwombe Mheshimiwa Waziri hebu tufanye utaratibu, turudi tufanye kazi na timu labda Mainjinia wa Mkoa lakini na kule halmashauri kwetu tuone tatizo liko wapi? Kwa nini tulishatoa hela nyingi halafu tatizo la maji bado ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuongezea, tulikuwa tumeomba pia fedha kiasi cha shilingi bilioni nne kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya maji pale mjini katikati, ilifanywa design nzuri tu sijui sasa kama Wizara na yenyewe imeihakiki ile design, tumepeleka andiko pale Wizarani, mpaka dakika hii niki-compliment yale niliyokuwa nikiongea mwanzo, inawezekana hata haya maji ambayo tayari tumeshakuwa tukiyasambaza kupitia hivi visima vipya na ile chemchem, chanzo cha maji cha chemchem inawezekana yasiweze kukidhi au kusambaa vizuri kama fedha hizi za ukarabati wa miundombinu zisipopatikana. Tunaomba, tutakuwa tumefanya kazi kubwa sana huku nyuma kama tumekula ng’ombe mzima tumebakiza mkia, hela imeshalipwa lakini wananchi hawanywi maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize kwenye hili kwamba kuna umuhimu mkubwa kupata zile fedha za ukarabati wa miundombinu ya maji. Miundombinu hii ilijengwa mwaka 1972, wakati Mji wetu wa Kondoa una population ambayo ilikuwa labda haizidi watu 20,000, leo hii tuna population ya watu 50,000, haiwezekani ikawa inatosha, lakini pili imeshakuwa chakavu… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Edwin Sannda.

MHE. EDWIN M. SANNDA: … kwa kiwango hiki hela ile tuipate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)