Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Khadija Hassan Aboud

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru kwanza naanza kwa kuunga mkono hoja hii, pili nachukua nafasi hiI kuipongeza sana Serikali kwa juhudi na dhamira yake ya dhati kabisa katika kuwapatia watanzania maji safi na salama, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa wanavyojitoa kwao kuhakikisha wananchi wa watanzania wanapata maji na kufuatilia miradi ya maji vijijini huko iliko pamoja na Mijini, nawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wetu na watendaji wote kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuhakikisha watanzania tunapata maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, maji ni uhai, maji ni afya, maji ni uchumi na kwa maana hiyo maji yakiwa ni uchumi kilimo kinahitaji maji, ufugaji unahitaji maji, mimea, miti na sisi binadamu tunahitaji maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi nashauri Serikali iongeze fedha za maendeleo katika kuhakikisha miradi hii ya maji inafanikiwa, na katika kuongeza fedha hizo za maendeleo naungana na Wabunge wenzangu waliosema kwamba katika mfuko wa maji tunahitaji kuongeza fedha ili
tutekeleze miradi ya maji, Serikali itafute vyanzo vya mapato kuhakikisha mfuko huu unakuwa mkubwa ili kuhakikisha miradi ya maji inatekelezeka ili kufikia malengo yetu tuliyojiwekea ifikapo mwaka 2020. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchelewa au kusuasua kwa miradi hii ya maji baadhi ya miradi ya maji imekwama kutokana na ucheleshaji ulioko bandarini kukosekana kwa misamaha ya kodi kwa vifaa vya maji. Ucheleweshaji huo unakwamisha pia utekelezeji wa miradi mbalimbali ya maji, pamoja na hilo ucheleweshaji pia unakuwa kwenye utoaji wa vibali vya kazi kwa wataalam wa maji ambao wanatoka nje ya nchi, wanachelewa kupata vibali vya kazi kwa hivyo miradi hii inachelewa kuanza kutoka na kukosekana kwa wataalam hao. Hili ni la kufanyia kazi kwa Wizara zinazohukia ikiwemo TRA pamoja Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuhakikisha masuala haya tunayafanyia kazi kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa miradi kuna changamoto nyingi zinakwamisha utekelezaji wa miradi, ikiwemo upungufu wa wataalam wa maji, Wizara inahitaji wataalam wa maji wapatao 3,910. Hili ni pengo kubwa sana kwa sababu kukosekana kwa wataalam hawa 3,910 wa kusimamia miradi katika maeneo yetu mbalimbali ya Tanzania inachangia sana kukwamisha utekelezaji wa miradi hiyo na pia kusababisha kununuliwa kwa vifaa ambavyo viko chini ya kiwango na utekelezaji wa miradi ambayo iko chini ya kiwango. Naomba Serikali isaidiane kutekeleza kazi hii ya kutoa vibali vya ajira kwa wataalam hawa wa maji ili waajiriwe na wakasimamie miradi yetu ya maji vijijini huko tunakohitaji mahitaji ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukwamisha pia upanuzi wa miradi ya maji katika miradi hii ya maji kuna madeni karibu bilioni 29 ni zaidi ya bilioni 21 Mamlaka za Maji zinadai kwa Taasisi za Serikali. Hili linakwamisha sana Mamlaka za Maji, kutengeneza miradi ya maji pamoja na kutanua hiyo miradi yenyewe ya maji huko vijijini, tunaomba madeni haya Serikali itafute mbinu ya kuyalipa au kuyakata huko huko Wizara ya Fedha ili mamlaka hizi zipate fedha zake zitekeleze miradi hii. Naipongeza sana Wizara kwa kazi iliyoanza ya kuweka prepaid mita ili kutatua tatizo hili la madeni. Lakini nashauri pamoja na kuongeza hizo prepaid mita hizo zilizokuwepo zianzwe kufungwa kwenye hizo Taasisi ambazo ni wadaiwa sugu wa maji wakawafungie huku badala ya kuwafungia wananchi, waanze na hizo Taasisi ambazo zinadaiwa mabilioni haya ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika miradi midogo midogo ya maji huku vijijini wananchi wanapata mzigo mkubwa wa kufidia au kulipia gharama za dizeli. Nashauri miradi hii mingi ya Vijijini ambayo ni miradi midogo midogo basi tuende na kutumia Solar System ambazo zitakuwa na betri zake ili hata wakati wa mvua ziweze kufanya kazi kusukuma maji katika visima hivi. Hii itapunguza gharama za uendeshaji wa miradi ya maji, pia itampunguzia mzigo mwananchi wa chini ambaye hana uwezo au kipato chake ni kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri uhamasishaji wa nguvu ufanyike pamoja na kutoa elimu kuhusu uvunaji wa maji ya mvua. Maji yetu ya mvua ni salama hayahitaji madawa, yanahitaji tu kuwekewa miundombinu ili tuyavune tuweze kuyatumia. Na katika kupanda mimea maji ya mvua yana rutuba kuliko maji mengine yoyote, hata huo ujenzi wetu uzingatie miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri uhifadhi wa vyanzo vya maji, elimu itolewe katika kuhamasisha wananchi juu ya kuhifadhi vyanzo vya maji na utunzaji wa mazingira. Na katika kuhamasiha wananchi nashauri Wizara pia itambue sasa mwananchi mmoja mmoja au vikundi, au taasisi vitakavyokuwa vinahifadhi vyanzo vya maji na vinatunza mazingira viwatambue na kuwapa tunzo au motisha maalum ili iwe hamasa kwa wengine nao kushawishika kutunza vyanzo vya maji na kuhifadhi mazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho namalizia kwa kusema kwamba maji safi na salama ndiyo yanayozaaa maji taka. Kwa hivyo kama maji safi na salama ndiyo yanayozaa maji taka ni vyema basi miundombinu ya maji safi iende sambamba na miundombinu ya maji taka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, naipongeza Serikali kwa yote yanayofanywa tuko pamoja Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri tuko pamoja kukusaidia katika kutatua changamoto hizi, kukushauri kila tunapohitajika. Naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)