Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana jkwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana, Wizara ya Maji. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kutujaalia uzima na niende moja kwa moja kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa uchapakazi. Wametutembelea kwenye wilaya yetu, lakini pia wametutembelea kwenye majimbo yetu yote mawili, tumeona mchango wao na umetusaidia sana. Nipongeze watendaji wa Wizara, wanatusikiliza vizuri na tunaomba waendelee kutusikiliza sisi wawakilishi wa wananchi pale tunapowapelekea maelezo sahihi juu ya miradi ambayo inatekelezwa kwenye majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na miradi mitatu ya Benki ya Dunia. Mmoja ni Mradi wa Kisura, Mheshimiwa Naibu Waziri aliutembelea mradi huu lakini mpaka sasa wananchi hawajapata maji. Alipokuja, tunakushukuru sana aliweza kutusaidia tukapata milioni 150 na mradi umejengeka umekwisha. Kinachotakiwa sasa ni nishati tu, sasa kile kijiji kinapata umeme lakini Wizara wametupendekezea tununue generator, sasa generator haiwezi kutusaidia kwa sasa, tunaomba hilo tusifikirie, wabadilishe mawazo ili umeme unaokuja pale watusaidie pesa tufunge mashine pale tupeleke umeme kwenye chanzo, itatusaidia sana. Ni kisima ambacho kinatoa maji mengi na ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa pili, ni Mradi wa Mpasa. Mradi wa Mpasa una maneno mengi, lakini naomba wanisikilize vizuri. Mradi ule unaenda vizuri na uko asilimia 80. Wamejenga miundombinu mizuri kabisa na unaenda vizuri kiasi kwamba unatia moyo na wakati mwingine tukiwaharibu watu wakati wana spidi nzuri ya utekelezaji tunawavunja moyo, uko asilimia 80, wamejenga matenki yote, sasa hivi wamejenga DP karibu zote. Sasa hivi bado kuunganisha tu kidogo kutoka kwenye njia kuu kupeleka kwenye vijiji. Pale ndiyo wamepata hela kidogo, tena itakuwa certificate ya mwisho na utakuwa umekwisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa yanapokuwa maneno mengi mara nyingi mradi huu unakwama wanachelewa kutupa pesa na wametuma tume nyingi kama tatu au nne, hawatuamini tukisema kwamba unaenda vizuri, DC yupo, Mkuu wa Mkoa yupo na anatufuatilia vizuri na mimi nipo. Kwa hiyo watuelewe vizuri, mradi huu unaenda vizuri. Sisemi hivi kwa kumpendelea mkandarasi, hapana, lakini mradi unaenda vizuri na spidi iko vizuri na mimi ndiyo nauangalia kwa karibu. Ulikuwa na matatizo na matatizo yanaweza yakawepo ya kawaida kama sehemu nyingine, lakini spidi ya mradi huu ni nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo Mradi wa Isale; mradi huu pia Mheshimiwa Waziri amekuja kuutembelea, ameuona jinsi unavyokwenda, tunamshukuru Mungu unaenda vizuri, mpaka sasa uko asilimia 50. Mradi huu ni wa shilingi bilioni tano na milioni mia tano, ni mradi mkubwa. Mkandarasi amejenga asilimia 50 mpaka sasa na amepokea shilingi bilioni moja na milioni mia moja na sasa wamempelekea milioni 400, kazi inaenda vizuri. Mheshimiwa DC pale anasimamia vizuri, ameshirikisha vijiji vile vya jirani, wanachimba mitaro, wanapata visenti kidogo pale na vinasaidia kwenye miradi ya vijiji. Kwa hiyo mradi huu nao unaenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatarajia mradi huu upeleke maji Nkata, upeleke maji Kitosi, Ntuchi A na Ntuchi B pamoja na Ifundwa, pamoja na Isale na Msilihofu. Kutakuwa na kakijiji kamoja kamebaki hapa China, nilimwambia Mheshimiwa Waziri alipokuja kwamba wataalam wanasema kwamba design haioneshi kwamba maji yale yanaweza yakaja pale, pana mwinuko, naomba kwa sababu ndiyo bomba linapita kwenye Kijiji hicho cha China, atufanyie utaratibu wa kisayansi utakaowezesha watu wale wapate maji, bila hivyo miundombinu inaweza ikahujumiwa jambo ambalo litatupa shida sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni Mradi wa Nkundi. Bwawa la Nkundi, la Kala Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri walilitembelea wakaona changamoto zilizokuwepo. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri juzi ametoa uamuzi, ametuletea milioni 65 na sasa hivi ninavyosema nilitembelea pale nimekuta wameweka umeme tayari, kwa hiyo nishati ile iliyokuwa inasuasua sasa tatizo lile litakuwa limekwisha. Nina imani kama kikwazo kilikuwa ni nishati, mradi huu sasa wananchi wataanza kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilikuwa naongea na Engineer, wananchi wa Kalundi wameanza kupata maji lakini Nkundi kuna tatizo, bado maji hayafiki. Sasa inaelekea Nkundi hapa kuna shida katika BOQ, inawezekana ujenzi wa BOQ haukuzingatia design ya Wizara katika ujenzi wake. Nimewahi kusikia fununu hii kwamba mkandarasi atakuwa aliwarubuni labda vijana wetu, wakaweka BOQ ambayo haikuwa imependekezwa na Wizara ili maji yaweze kufika pale, kwa sababu kuna mwinuko, wamepeleka bomba jembamba, sio kubwa, design ya Wizara inasema bomba linalotakiwa kuanzia pale kwenye chanzo mpaka kule liwe ni inchi tano, sasa nasikia wamepeleka tatu, kwa hiyo maji yanafika kwa shida na wakati mwingine una-pump siku mbili, tatu ndiyo maji yafike, hayawezi kukusaidia. Wafuatilie kwa makini kama Mheshimiwa Waziri alivyokuja wakati ule akafuatilia na Mkuu wetu wa Mkoa yuko makini sana, ataweza kufuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi mwingine wa maji wa Wampembe. Wampembe ni Makao Makuu ya Tarafa na kuna mwinuko na chanzo kizuri cha maji ya kutiririka. Wataalam wangu wamefanya utafiti wakasema kwamba wametoa mapendekezo Wizarani japo hawajafikisha hapa, tunaomba wataleta mapendekezo hivi karibuni, tukipata ule mradi utalisha vijiji karibu vitano na ni maji ya mteremko. Awali halmashauri ilikuwa imefunga huo mradi, miundombinu yake ikafa, ukifufuliwa utakuwa umetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa mwisho ambao nafikiri utatusaidia ni wa Kijiji cha Chonga; Kijiji cha Chonga kinakosa maji. Wataalam wangu wameleta mapendekezo hapo na inaonekana kwamba shilingi milioni 300 ndiyo zinatakiwa ili kijiji hiki kiweze kupata maji. Tayari miundombinu kama tenki lipo, limeshajengwa muda mrefu, ni njia tu ya maji kutoka pale Kijiji cha Nchenje kuja Chonga kama kilometa nne hivi, lakini tenki lipo na linaweza kufanya kazi vizuri. Naomba kwa unyenyekevu mkubwa na uchapakazi wao wanisaidie nipate shilingi milioni 300 ili mradi uweze kufanya kazi. Niwatoe wasiwasi, pesa za maji pia zinasimamiwa Wilaya ya Nkasi, si vile kama zinapotea potea, maana wanakuwa na wasiwasi na wakati mwingine, haziji kwa wakati, wanaunda tume nyingi nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba wakati fulani DC yupo, Mkuu wa Mkoa yupo, Usalama wa Taifa wapo, PCCB wapo, wote wapo ni watu wanaoangalia miradi ya Serikali. Hakuna mtu ambaye atakaa tu pesa zinapotea bila kuangalia, hili tuliangalie sana, lisitie Wizara kigugumizi cha kutuletea pesa Wilaya ya Nkasi. Zinasimamiwa na sisi wenyewe Mwenyekiti wa Halmashauri yupo, Mkurugenzi yupo, wote tunasimamia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii, mchango wangu ni huo. (Makofi)