Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Emmanuel Papian John

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nawapongeza Mawaziri ambao wametuletea bajeti hii ambayo inakidhi matarajio ya maeneo mengi kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze Kamati ambayo na yenyewe imesoma taarifa yake na kuainisha baadhi ya mambo ambayo na sisi tuliyajadili na tukaona kwamba yanafaa kuingia kwenye bajeti hii ya 2019/2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa namna ambavyo imejitahidi kulipa wakandarasi. Mpango wa kulipa wakandarasi unaonekana sasa uko kwenye utaratibu ambao unakwenda vizuri, wakandarasi wengi wanalipwa kwenye maeneo mengi, zaidi ya shilingi bilioni 84 zimetamkwa kwamba zinakwenda kulipa wakandarasi ili waweze kurudi site.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Wizara iweze kukaa na kuandika barua kwa wakandarasi wote nchini ambao wana miradi vijijini wawe wameripoti kwenye maeneo yao ya kazi kwa sababu wengine wamelipwa na hawajaripoti. Matokeo yake ni kwamba watalipwa watapotea na hizo pesa na mwisho wa siku miradi ya maji haitakamilika. Ili tuweze kudhibiti hali hii tunaomba Wizara iwaandikie barua wawe wameripoti kwa wakati na waweze kufanya kazi na sisi tutarudisha mrejesho kwamba hawa watu sasa watakapo- raise certificates nyingine wawe wame-qualify kwenye kupewa pesa zao nyingine ambazo zitakuwa zinabaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, naomba Serikali itusaidie juu ya jambo kuongeza shilingi 50 kwenye maji. Hii shilingi 50 tunayoiomba tumeona kwamba ni njia pekee ya kutatua migogoro ya maji nchini mwetu kwenye maeneo mengi. Niombe sasa Serikali ilione hili na Bunge zima tukubaliane kwamba hii shilingi 50 ya maji itakapokuwa shilingi 100 inaonekana miradi mingi vijijini itaweza kukamilika kwa wakati. Kuna miradi mingi na visima vya maji vimesimama, tunadhani kwamba hii shilingi 100 inaweza kusaidia ku-push miradi mengi ya maji vijijini ikaweza kukamilika kwa wakati kabla ya 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii iende sambamba na vichoteo vya mifugo. Unapotengeneza mradi wa maji unaweza kuweka na kichoteo cha mifugo kwa hiyo maji hayohayo binadamu watatumia upande mmoja na upande mwingine mifugo inapata maji. Kwa hiyo, kwenye vijiji vyetu pale ambapo wakulima na wafugaji wetu wapo wote wata- enjoy mradi uleule ambao uwezo wa pampu ni huohuo, matenki ni yaleyale, ni kiasi cha kuweka tu mbauti kwa ajili ya mifugo na yenyewe ikapata maji ili kupunguza adha ya wanayoipata wafugaji na kusumbuana kwa kwenda kwenye maeneo mengine au kufanya double projects kwenye maeneo wakati sisi tunahitaji pesa ziweze kusaidia maeneo mengi wakati hatuna pesa za kutosha. Kwa hiyo, nadhani hiyo programu inapokuwepo basi kwenye miradi ya maendeleo mikubwa kuwepo na programu ya kutengeneza mbauti kwa ajili ya mifugo halafu miradi yote iende sambamba, binadamu atumie maji lakini na mifugo yetu iweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze kwa Bwawa la Dongo. Muda mrefu tumeahidiwa Bwawa la Dongo kwamba linakwenda kujengwa, mwaka jana kwenye bajeti lilikuwepo na mwaka huu lime-appear tena. Naomba nisaidieni hili bwawa lijengwe, programu ianze, wekeni fund kwa sababu tuna shida kubwa sana katika Vijiji vya Rogoiti, Laiseri, Dongo na vijiji vingi ambapo kanda ile yote ni kame lakini vijiji hivyohivyo vinakwenda mpaka upande wa Dodoma kwa maana ya upande wa Kongwa; vijiji hivyo vinakwenda mpaka upande wa Gairo, Morogoro. Bwawa hilo ni potential kwenye kanda hiyo wa sababu litasaidia maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti yenu mnaainisha vijiji 19 lakini ni zaidi ya tarafa nne zitakazohudumiwa na bwawa hilo. Zaidi ya vijiji hamsini vitapata maji kutokana na bwawa hilo kwa sababu unaweza kuendelea kufanya extentions kwa kuunga mabomba kwa sababu litakuwa ni bwawa kubwa sana na litatosheleza maeneo hayo. Tunataka tuombe sasa Serikali ichukue initiative ianze kujenga hili bwawa angalau basi miaka miwili, mitatu inayokuja basi bwawa liwe limekamilika ili Gairo, Kiteto na Kongwa wapate maji tuweze kupunguza adha ya maji kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wetu wa Kibaya muda mrefu ni wa ukame lakini maji tunayo chini. Tunaomba Serikali itusaidie jambo moja, tunaomba DDC waje watumie maji kwa sababu tunayo, watuchimbie na yaungwe kwenye tanks ambazo sasa hivi zinajengwa ili tuweze kutosheleza ule Mji wa Kibaya kwa maji tuwe tumepunguza adha ya maji kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunayo maeneo kame kwa mfano Kata za Makame, Ndido, Rorela, ni maeneo ya wafugaji lakini maeneo yale hayana shida kubwa sana ya maji kwa maana ya maji chini ya ardhi, maji chini ya ardhi yapo, tunachotafuta sisi ni wataalam wa kuweza kuja kuchimba yale maji kwa wakati, mita ni zaidi ya 100, 150 unapata maji. Kwa hiyo, tulitaka surveyors na team work ya Wizara ije kufanya ile survey, ijiridhishe halafu inaweza kutuchimbia kwa awamu angalau na sisi wananchi wetu waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo lingine moja la miradi ya maji ambayo haikamiliki na mmeona Rais kila wakati anapotembea analalamikiwa maji, tumekuwa na wakandarasi ambao hawamalizi kazi kwa wakati. Naomba kuishauri Serikali, kama kweli Wizara ya Maji mko serious kumaliza huu mgogoro, tuumalize hivi, wakandarasi wote kwenye kila wilaya ambayo Rais anakanyaga wawe pale waeleze miradi ya maji wamefanya lini, wamemaliza lini, miradi inatoa maji au haitoi, waachane na Rais palepale. Waende kwenye site Rais anapofanya ziara akiuliza miradi ya maji wao wasimame washike microphone waeleze, maji yapo, hayapo aachane nao hukohuko magereza ili tupunguze utapeli wa wakandarasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wakandarasi wengi inaonekana kwamba ni kifo cha pesa kwa sababu unapotandaza bomba chini kwenye ardhi anakuja anakwambia mimi bomba niliweka, haya, uthibitisho mtachimbua mita 300, 400, mtachimbua kilometa? Sasa kuna uongo na udanganyifu mwingi, anaweza kuwadanganya kwamba aliweka bomba kumbe hakuweka. Sasa mimi naomba ili tumalize ubadhirifu wa pesa za Serikali kwenye miradi ya maji, kila Rais anapokanyaga waende, waseme maji yapo au hayapo waachanie magereza Rais aendelee na safari zake uone kama miradi ya maji kwa wananchi haitapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ndiyo ushauri wangu kwa Serikali, sasa hivi tuamue. Miradi inayoendelea kwenye Wilaya yangu mkandarasi kama hajatoa maji hajapokelewa mimi na yeye tutamalizana mtasikia. Ninyi mmewalea sana na mmesababisha uharibifu mwingi wa maisha ya binadamu na upotevu wa pesa nyingi za Serikali kwenye miradi mingi ambayo inaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mradi wa Matui, Naibu Waziri tulikubaliana kwamba uje Kiteto ukaishia Simanjiro. Njoo Matui uangalie mradi wa shilingi milioni 600 zimeteketea, hakuna maji, watu wanakimbizana, kichoteo ni kimoja, maji hayapatikani. Sasa uje tuamulie pale Matui, tusiache kuzungumza suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sitaki miradi viporo Kiteto, sitaki migogoro, miradi ambayo imeanzishwa kwa sasa hivi ninaisimamia na inatoa maji, ile ya nyuma njoo tumalizane kulekule ueleze wananchi imepotelea wapi, imefia wapi, umeamua nini. Njoo wewe na wakandarasi nikukabidhi wananchi uwahutubie uwaambie kwamba wanapata lini maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba aniahidi ni lini tunakwenda Kiteto, mambo mengine yamekwisha. Naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)