Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu sana Wizara ya Maji, na nianze kwa kumshukuru sana kuishukuru sana Serikali hususani Mheshimiwa Prof. Mbarawa Makame pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Jumaa Aweso kwa ushirikiano mkubwa sana ambao mmetupa wana Madaba kuhakikisha miradi yetu ya maji inafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Prof. Mbarawa na Mheshimiwa Jumaa Aweso mmekuja wenyewe mmetembelea miradi mbalimbali ya maji Madaba, mmeshirikiana na wananchi wa Lilondo kuhakikisha kwamba miradi yao ya jamii kupitia vikundi inafanikiwa kwa kuchangia pesa ninyi wenyewe, pia kwa kuwatia moyo ninawashukuruni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nishukuru miradi mingine ambayo inaendelea iliyokamilika Madaba ya maji na hii ambayo imetengewa bajeti ya zaidi ya bilioni moja kwa ajili ya kuendelea kuitekeleza. Siku ya leo nilitamani sana nitume muda mrefu kuishauri Serikali juu ya mambo kadhaa ambayo ninadhani kama hayatachukuliwa umaanani Wizara hii itawaangusha watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza naomba tulijue kwamba kama vitu ambavyo vinambeba Mheshimiwa Rais ni uzalendo wake na upendo wake kwa watanzania. Amejitoa kwa hali na mali kufa na kupona Watanzania wapate unafuu katika Nyanja zote, amekusudia kwa kufa, kupona kuhakikisha wakina Mama tunawatua ndoo vichwani ili kuhakikisha hawapati tena usumbufu wa maji. Lakini Watumishi ndani ya Wizara ya Maji ni mzigo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie kusema na hili limesemwa na Mheshimiwa Waziri mwenyewe kwenye ukurasa wa 108 wa hotuba yake. Amesema: “moja katika changamoto katika Wizara hii ni uwezo mdogo katika utekelezaji, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji” na kama ningepata fursa ya kurekebisha hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ningeiandika kama ifuatavyo: “Dhamira ndogo ya Watumishi katika idara inayohusiana na masuala ya maji kutekeleza na kusimamia miradi vizuri”. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa nyingi zimetengwa kwenda kwenye miradi, sisi Madaba pia tumetengewa na Mheshimiwa Waziri anahangaika sana kuhakikisha tunafanikiwa, lakini procedure ndogo tu ya kupata vibali vya kutekeleza miradi iliyotengewa fedha inachukua karne nzima. Mwaka mzima Mtumishi wa Madaba anaandika barua Wizarani, anasubiri majibu ya kibali cha kutekeleza mradi. Mradi umetengewa fedha, tupo ndani ya bajeti, mradi hauchukuliwi umaanani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshauri Mheshimiwa Waziri, watu kama hawa awaondoe, wanamchafua, wanaichafua Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Inawezekanaje wewe umeandikiwa barua Mwezi wa nane, Mtumishi umeipokea kutoka kwa mtaalam mwenzako, hata ku-acknowledge kwamba umeipata hiyo barua na hata baada ya kukumbushwa, inakaa miezi sita, saba mpaka Mbunge anakwenda kwa Waziri, Waziri anafuatlia ile barua, tutafika kweli na Awamu hii ya Tano? Inasikitisha sana kuona kasi ya Mheshimiwa Rais, kasi ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu Waziri wake inaangushwa na watu wadogo, watu walio katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania tumebadilika sana, Watanzania tumeakisi falsafa, tumeiishi falsafa ya Mheshimiwa Rais ya “hapa kazi tu”, wananchi wanahangaika kila siku, wanapambana kuhakikisha kwamba tunaitekeleza lakini bado baadhi ya watumishi wa umma wanaishi maisha yale yale ya business as usual. Yamesemwa haya na Mheshimiwa Adadi humu humu ndani, yamesemwa na Mheshimiwa senator hapa, yamesemwa na Mheshimiwa Keissy na mimi nayasema na naamini Wabunge wengine watayasema, wanaotuangusha naomba Mheshimiwa Waziri wa Maji akafanye nao kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto ya certificate, siyo Madaba peke yake, sehemu nyingi tunalalamika sana, Wakandarasi wametekeleza wajibu wao, walipwe ili kazi ziende, lakini nalo hilo linamhitaji Mbunge aende mguu kwa mguu mpaka Wizarani, hawa watumishi wana kazi gani?. Hili kwa kweli limenisikitisha na nimeungana na Wabunge wenzangu kulisema na naamini Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo sisi tunamwamini na tunamtegemea, atakapopitisha Bajeti yake ambayo tutaiunga mkono, aende akasafishe huko chini wanatuangusha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri, pamoja na michakato hii, vijiji saba vya Wilaya ya Madaba vimeendelea na utaratibu wa usanifu wa mradi. Mradi wa Vijiji Saba unakwenda kunufaisha wananchi 25,000. Mradi huu ngazi ya Halmashauri walishamaliza usanifu wa awali kabisa na wameomba kwa Mheshimiwa Waziri na amewakubalia, amewapa kibali lakini wameomba pia kwake kibali alichowapa ni kwa ajili ya kuweka maji ya muda mfupi kwa kutumia visima virefu. Tunamshukuru na tunaamini utaanza kutekelezwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo walilonalo ni kwamba wanashindwa kufanya usanifu wa kina kwa sababu zaidi ya miezi sita sasa wanasubiri majibu ya Wizara, waletewe wataalam kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina na pengine hili lingekuwa limeshafanyika leo tungeweza kuisoma Bajeti ya eneo hilo. Mheshimiwa Waziri tunamwomba sana, tunamwamini, tunamtegemea na tunaunga mkono hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)