Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, naomba niaze kwa pongezi mahususi kwa Mwalimu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na timu yake mahiri ya Walimu waliobobea ambao amewapa kazi ya kusimamia sekta hii ya elimu hususan dada yangu Profesa Ndalichako. Shemeji yangu Dkt. Ole-Nasha na timu nzima ya Maprofesa ambao wamekaa kule nyuma ya kioo kwa kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kabisa kwa kusema naunga mkono hoja. Kulikuwa na hoja kwamba fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, zitolewe zote kabla ya tarehe 30 Juni, 2019. Naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Fungu hili lilitengewa shilingi trilioni 1.4 na mpaka kufikia tarehe 29 Aprili, Fungu hili lilikuwa limepewa shilingi bilioni 890.58, ambayo ni asilimia 63 ya bajeti kwa Fungu hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kutambua umuhimu wa kipekee wa elimu kwa maendeleo ya nchi yetu, Serikali inapenda kuwahakikishia Watanzania kwamba katika kipindi kilichobaki, Serikali itatoa fedha kwa Vote 46 kama Sheria ya Bajeti na hususan kifungu cha 45 (b) kinavyoelekeza. Naomba nikisome ili tuelewane vizuri;Funds disbursements to Vote shall be based on performance approved budgets and funds availability.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya bajeti ya elimu inashuka na kuwa bajeti ya maendeleo imekuwa na mserereko wa kupungua, ni kweli, ukiangalia takwimu zinaonesha bajeti ya elimu inapungua katika asilimia kutoka asilimia 17 ya bajeti yote 2015/2016, asilimia 16 mwaka 2016/ 2017, asilimia 15 mwaka 2017/2018, asilimia 14 mwaka huu na asilimia 14 mwaka ujao wa fedha. Hata hivyo, si kweli kuwa bajeti ya maendeleo imekuwa na mserereko wa kupungua, uki-decompose hizi namba, unaona kwamba kilichopungua ni bajeti ya matumizi ya kawaida na imepungua kwa miaka miwili iliyopita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwaka 2015/2016, bajeti ilikuwa bilioni 3.2 na hii ni recurrent, ikaongezeka kwenda bilioni 3.7 mwaka 2016/2017, mwaka 2017/2018, ndiyo ikashuka kidogo kuwa bilioni 3.5 na bilioni 3.4 mwaka huu wa fedha na kwa mwaka kesho inashuka kidogo kuwa bilioni 3.1. Kwa hiyo, hiyo ni recurrent na hii inatokana na hatua ambazo Serikali ilichukua ikiwemo kuwaondoa watumishi hewa kutoka katika sekta ya elimu, lakini restructuring ambayo imefanyika katika taasisi mbalimbali ambayo imeondoa baadhi ya watumishi kutoka kwenye taasisi mbalimbali katika Fungu hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia upande wa fedha za bajeti ya maendeleo, hizi zimeongezeka kutoka bilioni 0.6 mwaka 2015/2016 kwenda bilioni moja mwaka 2016/2017, bilioni 1.1 mwaka 2017/2018, bilioni 1.2 mwaka 2018/2019 na bilioni 1.3 kwa mwaka ujao wa fedha. Kwa hiyo, ni vizuri kufanya decomposition ili uweze kusema kweli bajeti inateremka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu vilevile, Waheshimiwa Wabunge wakatambua mchango mkubwa wa wadau wengine katika elimu nchini na hususan wamiliki wa shule binafsi lakini pia taasisi za kidini, lakini pia ni muhimu kuzingatia kwamba sekta nyingine nazo ni muhimu kwa maendeleo ya elimu yenyewe. Kwa hiyo, ni lazima nazo zipewe fedha, kwa mfano, bajeti ya ulinzi na usalama, vyuo, vijana wetu walioko vyuoni, walioko shule za msingi na sekondari, wanaweza wakasoma pale tu ambapo tunawahakikishia ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, afya, maji, kilimo, miundombinu ya umeme na ICT nayo ni muhimu ili kuweza kuboresha elimu. Kwa hiyo, ni muhimu tuangalie mambo yote hayo ili tuweze kuona mwenendo mzuri unaofaa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa zaidi, ni ukubwa wa keki yetu, kwa hiyo, kazi yetu ambayo tunatakiwa tufanye, kwa kweli tujielekeze tupate mapato zaidi, lakini tuweke vipaumbele vizuri vya kisekta na vya kitaifa ambavyo tukivitekeleza vizuri tutakwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja kwamba fedha za udhibiti wa ubora wa shule zitolewe zote kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika. Serikali haina pingamizi kabisa na ushauri huu na kama nilivyoeleza awali, fedha zitatolewa kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti ya mwaka 2015, kazi zilizokwishafanyika hadi sasa na mpangokazi kwa kipindi cha miezi miwili iliyobaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Bodi ya Mikopo kwamba ipewe Fungu lake linalojitegemea, tunawashauri Bodi ya Mikopo kuandaa andiko la maombi ya kuwa na Fungu lake linalojitegemea baada ya kushauriana na Wizara mama. Utaratibu wa kuanzisha Fungu unazingatia majukumu na muundo ambao umepitishwa na Ofisi ya Rais (Utumishi) ili kuweza kubainisha ule mnyororo wa mamlaka za utendaji, ili tujiridhishe kwamba fedha ya umma itasimamiwa vizuri na kwa mwongozo zaidi wanaweza wakaonana na Ofisi ya Rais (TAMISEMI).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bajeti ya COSTECH; umuhimu wa COSTECH, kwa kweli unafahamika na ndiyo maana inatengewa bilioni 9.18 kwa mwaka ujao wa fedha na hili tumezingatia tu wigo wa mapato na mahitaji mengine ambayo ni lazima yagharimiwe na Serikali. Hata hivyo, ni vizuri pia kutilia maanani kwamba utafiti ni suala mtambuka na linatekelezwa kwenye taasisi nyingine, ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu, lakini pia taasisi kama TILDO, NYUMBU, TAWIR, TAFOR, CARMATEC, SIDO, VETA, ambazo nazo kwa kiasi cha kikubwa zinategemea fedha kutoka Serikalini kwa ajili ya kufanya utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuliambiwa Serikali iheshimu makubaliano ya kimataifa, ikiwemo lile Azimio lile la SADC, kwamba Serikali itenge asilimia 20 ya bajeti yote kwa ajili ya elimu. Ni kweli, lakini yapo maazimio mengine ambayo Tanzania iliyakubali, ikiwemo Azimio la Maputo ambalo linatutaka tutenge asilimia 10 ya bajeti yote kwa ajili ya kilimo, afya asilimia 15 ya bajeti yote, utafiti asIlimia moja ya pato la Taifa, asilimia 0.05 ya bajeti kwa ajili ya takwimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuliambiwa Serikali iheshimu makubaliano ya kimataifa, ikiwemo lile Azimio la SADC kwamba Serikali itenge asilimia 20 ya bajeti yote kwa ajili ya elimu. Ni kweli, lakini yapo Maazimio mengine ambayo Tanzania iliyakubali ikiwemo Azimio la Maputo ambalo linatutaka tutenge asilimia 10 ya bajeti yote kwa ajili ya kilimo; afya asilimia 15 ya bajeti yote; utafiti asilimia 1 ya pato la Taifa; na asilimia 0.05 ya bajeti kwa ajili ya takwimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Maazimio yote haya yatatekelezwa sekta tatu tu peke yake zitachukua asilimia 45 ya bajeti yote. Sijui kipi hicho kitasalia kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu yetu, ulinzi na usalama, maji, ikiwemo na bajeti ya Mhimili wa Bunge, tutafanyaje? Kwa hiyo, ni muhimu sana huko mbele pengine tukifika lazima tuweze kuyapanga vizuri badala ya kwenda tu kusema tutatekeleza Maazimio haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme moja la mwisho, niliulizwa hapa kwamba upo Waraka wa Serikali unaonesha kwamba Waziri wa Fedha alifuta baadhi ya kodi kwa wamiliki wa shule binafsi na kwamba huo Waraka uko wapi. Serikali haijawahi kutoa Waraka unaofuta kodi kwa wamiliki wa shule binafsi. Mabadiliko mbalimbali ya kodi huwa tunayafanya kupitia Sheria ya Fedha au Gazeti la Serikali kwa mwaka husika na hilo halijawahi kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)