Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, katika michango ya Waheshimiwa Wabunge kuna mambo ambayo yamezungumzwa, ambayo yanahusiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Kuna hoja zimetolewa na nimejaribu kupitia kitabu cha Kambi Rasmi ya Upinzani, wameandika data nyingi humu, lakini nyingi siyo za kweli na nilipojaribu kufuatilia nikagundua kwamba hizi zilikuwa zinaandikiwa pale African Dream, wakishirikiana na wenzao. Hizi data ni za African Dream, kwa hiyo, naomba mnisikilize niwape data za Serikali, ambaye ni custodian wa information hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walisikiliza vizuri wakati Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Utumishi anazungumza hapa, alitoa tamko la Serikali kwamba madai ya Walimu na madaraja na maslahi mengine yataanza kushughulikiwa kuanzia Mei Mosi, maana yake kesho, lakini pia kuna maelekezo yametolewa kwa vyombo mbalimbali vinavyoshughulika na utumishi wa umma, hiyo kazi itafanyika. Kwa hiyo, kimsingi hili pia halipo kwenye Wizara ya Elimu, lipo utumishi, lakini limeulizwa hapa nikasema nilitolee kauli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna hoja imezungumzwa ya elimu msingi bila malipo na kwa bahati mbaya sana nilimsikia Mheshimiwa Yosepher Komba akizungumza, kwa namna ambayo kwa kweli alikuwa anabeza, lakini kwa kweli ukifuatilia namna ambavyo mpango huu wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Awamu ya Tano umewasaidia Watanzania walio wengi, enrollment imeongezeka, watoto wa shule ya msingi na madarasa ya awali wameongezeka sana. Kila mwezi Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, anapeleka shilingi billioni 23 kwa ajili ya elimu msingi bila malipo. Kwa hiyo, siyo jambo la kubeza kwa kweli ni jambo la kupongeza na Watanzania wengi walio maskini, watoto wao wanaingia shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wamezungumza kwamba watu wanafelifeli, siyo kweli, tunao watoto ambao wamefaulu vizuri sana kutoka shule za kata na wameenda mpaka shule za vipaji na tutawapa taarifa ya majina yao kwa ajili ya kumbukumbu kwa ajili ya muda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwaka 2016/2017, Serikali iliajiri Walimu wa sayansi 3,081, mwaka 2017/2018, walimu 2,767 wa sekondari na msingi, lakini hapa tunapozungumza, tumesambaza Walimu 4,500, miongoni mwao Walimu 3,088 wote ni Walimu wa sayansi, no, ni Walimu wa shule ya msingi, lakini 1,400 ni Walimu wa sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge alizungumza, maeneo yale ambayo yalikuwa na upungufu mkubwa sana kwa upande wa masomo ya sayansi tumepeleka. Ni kweli kwamba hawatoshi lakini wameenda. Kumbukumbu ya kitabu chao hili cha African Dream, kinaonesha kwamba ni upungufu karibu Walimu 91,000, siyo kweli. Tuna upungufu wa Walimu ni kweli tunakubali, 66,485 kwa shule za msingi na Walimu 14,080 kwa shule za sekondari. Mpango uliopo, kila mwaka tutakuwa tunaajiri Walimu kupunguza gape hili na hawawezi kuchukua miaka 10 kama walivyosema, siyo kweli, itachukua muda mfupi kwa mpango ambao Mheshimiwa Rais amesharidhia, tunaziba ma-gape ya watu waliofariki dunia, watu waliosimamishwa kazi kwa makosa ya kiutumishi na mambo kadha wa kadha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile madarasa yamejengwa, kwa mfano, mpaka kufikia Februari, 2019 shule za msingi yamekamilishwa madarasa 2,840, tunaendelea kujenga madarasa 2,638, hapo yanaendelea kujengwa. Matundu ya vyoo 76,700 na yanaendelea kujengwa 3,004, nyumba za Walimu 720 na tunatengeneza madawati 135,000. Hii kazi kubwa inafanyika chini ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna mpango wa shule shikizi, tumejenga shule shikizi kupunguza umbali kati ya shule na shule 255,000 kwa kutumia bilioni 18.5 zimefanya kazi kwenye mikoa tisa na halmashauri 63, madarasa 502, 0fisi 251, matundu ya vyoo 1,255, maktaba 34 na maboma 223.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wametoa hoja hapa ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi kwamba aliahidi kutoa fedha za mabona shilingi bilioni 29, naomba nitoe taarifa kwamba juzi tulitoa fedha shilingi bilioni 29.9 kwa kuhusiana na Wizara ya Elimu na tumepeleka kujenga maboma mbalimbali zaidi ya 2,300 yanaendelea kujengwa. Hapa tulipo tunapeleka mpango mwingine wa kukamilisha maboma ya shule za msingi nchi nzima kwenye halmashauri zote na majimbo yote ikiwezekana. Hii ni kazi nzuri ambayo inafanyika ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi, chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwenye mpango wa 2019/2020 tutajenga nyumba za Walimu 364 kwa kutumia shilingi bilioni tisa, lakini sekondari maalum 26 kila mkoa kwa ajili ya watoto wa kike, kupitia mradi wa SEP, lakini EP4R tunanunua magari 26 kuratibu elimu kwa ngazi ya mkoa, kila mkoa watapata gari jipya, tunajenga majengo ya utawala 50, nyumba za Walimu 800, mabweni 300, matundu ya vyoo 1000, kumbi za kufundishia kwa maana ya kumbi za wanafunzi zile mbalimbali 2,000 zinajengwa, lakini shule kongwe zinakarabatiwa 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo ni mambo makubwa ambayo yanafanyika katika nchi hii na ni muhimu sana tukaitia moyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme jambo moja la mwisho, kuna hoja inapotoshwa kwamba Serikali imesema elimu bure, kwa hiyo, michango hairuhusiwi. Umetolewa Waraka wa Wizara ya Elimu ambao umeanza kufanya kazi Januari, 2019, mwongozo umetolewa. Tukubaliane nchi hii kwa ukubwa wa taifa hili na upungufu wa fedha uliopo, haiwezekani tukaishi kama ndege bila kuchangia chochote. Serikali ilitoa fedha, bure, tumeondoa ada na shule za sekondari zingine tumepeleka fedha na mabweni yanajengwa miundombinu inaimarishwa na Walimu wanalipwa na watumishi wengine wa Serikali, lakini wananchi wenye uwezo watachangia kadri ambavyo uwezo wao utaruhusu na Serikali imetoa huo mwongozo, kuanzia ngazi ya kijiji, ngazi ya kitongoji, ngazi ya kata, Waheshimiwa Wabunge, kwenye mikoa. Kilichozuiliwa ni kwamba, asitolewe mtoto darasani eti kwa sababu ya mchango mzazi wake au mlezi hajachanga, hapana. Kama mtoto anadaiwa, mzazi na Walimu wasimamie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tukasema Walimu wasisimamie michango, kwa sababu ilionekana kwamba Mwalimu anapokwenda kudai michango kwa wazazi anajenga chuki na usimamizi unakuwa mgumu. Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi watasimamia zoezi la michango, wenye uwezo wananchi wa kawaida, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wengine wachangie kile ambacho wanaweza. Ukichimba kisima cha maji sawa, ukijenga darasa sawa, tundu la choo sawa, darasa sawa, nyumba ya mwalimu sawa, hii kazi ni ya Watanzania wote, tushikamane, tuunge mkono kazi nzuri ya Serikali ili mambo yaweze kuboreshwa na Watanzania wote na watoto wetu waweze kusoma vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.