Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia kwenye bajeti ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama hapa. Pili, nawashukuru wanawake wa Morogoro kwa kunileta tena humu Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Charles Mwijage kwa mipango yake mizuri yote aliyoitoa kwenye kitabu chake cha bajeti. Mheshimiwa Waziri unaweza, nakuamini, naomba ufanye kazi, yale yote uliyoyaandika kwenye kitabu na Kamati yako na Wizara yako muweze kuyatekeleza kama yalivyopangwa pamoja na Wizara yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa yote, hata wewe mwenyewe unavyoendesha Bunge lako hili Tukufu. Nianze kabisa na wafanyabiashara. Hapa naanza na sekta hii kwa sababu ya wafanyabiashara wadogo wadogo na hasa akina mama na vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mmoja ni shuhuda kuwa sekta hii kwa upande wa biashara, akina mama wengi sasa hivi, hakuna mama anayelala, kila mama anafanya biashara; na biashara nyingi wanazozifanya kama tulivyosema kuwa viwanda sana sana ni usindikaji kutokana na malighafi ya kutoka kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasindika, lakini Mheshimiwa Waziri tatizo wanalolipata hawa akina mama, jambo la kwanza ni tatizo la kupata kibali cha TBS. Wanahangaika sana, mikoa yote. Watu wengi wanahangaika sana, hasa akina mama, kupata mambo ya TBS. Wanafanya usindikaji mzuri, usindikija wa mvinyo, usindikaji wa achali na mambo mengine. Kwa hiyo, naomba sana waelekezwe jinsi ya kupata TBS na minyororo yote ya kupata TBS iweze kufupishwa kusudi wapate TBS kwa urahisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa wafanyabiashara hawa wadogo wadogo, naomba waweze kujengewa mazingira mazuri hasa kwa kupata mikopo ambayo kuwawezesha kufanya hii biashara yao kwa urahisi, kwa sababu wakifanya biashara ndiyo hapo hapo wanainua pato lao na pato la nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, ni kweli Serikali haifanyi biashara, lakini tunatafuta wawekezaji. Naomba sana wawekezaji wanapopatikana, jaribuni kuwasambaza kwenye mikoa yote ya Tanzania. Kuna mikoa ambayo haijafaidika na viwanda hivi. Mikoa ya pembezoni bado haijafaidika sana na viwanda. Kwa hiyo, naomba uiangalie vizuri na yenyewe iweze kupata wawekezaji ilimradi cha msingi wawekezaji waweze kupewa miundombinu. Sana sana ni land bank, ili iweze kutiliwa maanani. Kwa sababu unampeleka mwekezaji, kwa mfano, unampeleka Morogoro, Iringa, Kagera au Pwani, lakini unakuta huko hakuna area ambapo anaweza akafanyia. Huyo mwekezaji anahangaika, mwisho anarudi na inaonekana hana pa kufanyia biashara na mwisho wake anahama anakwenda kwenye nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee kuhusu viwanda. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais, amesema kuwa nchi yetu inabidi iwe nchi ya uchumi wa viwanda. Ni kweli inawezekana sisi wenyewe tukijituma. Tukijituma inawezekana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie viwanda vilivyokuwepo, hasa miaka ya 1980, nchi yetu ilikuwa na viwanda vingi sana. Kwa mfano, nikianza na Mkoa wangu wa Morogoro, tulikuwa na viwanda vingi. Nianze na Kiwanda cha Juisi ambacho huwa nakisemea mara kwa mara kwa sababu mimi mwenyewe napenda sana juisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Juisi cha Morogoro na mikoa mingine iliyo karibu kwa mfano tumesema Mkoa wa Tanga, Muheza, Lushoto, Iringa na mikoa mingine wanalima sana matunda na mboga mboga. Kwa upande wa juisi naomba sana kiwanda hiki kiweze kuangaliwa. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana kiweze kufanya kazi. Ni kweli ni aibu kuona watu wananunua juisi kutoka Saudi Arabia ambao kweli nchi yao siyo fertile kama nchi yetu. Kwa hiyo, naomba sana hili tuliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili siku moja niliongea lakini ikaonekana kuwa hivi viwanda, pamoja na Kiwanda cha Azam nikiunganisha pamoja, wanaleta sana sana concentrate ambayo siyo nzuri. Nchi yetu ni nzuri ambapo tunalima matunda. Kama kuna tatizo la ubora wa matunda, tulifanyie kazi. Tuna watafiti wetu, waweze kufanya kazi, huu ubora unaweza ukawaje ukatoa juisi ambayo haiwezi kuchacha mara moja. Tuifanyie kazi pamoja na maabara ziweze kuwepo za ku-test shelf life ya hii juisi iweze kuendelea kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu bado niko hapo hapo, niongelee kiwanda cha ngozi. Tulikuwa na Kiwanda cha Ngozi - Morogoro ambacho sidhani kama kinafanya kazi. Kilikuwa kinatoa bidhaa ya ngozi, lakini sasa haipo. Kuna Kiwanda cha Kioo, tulikuwa tunapata sahani na vikombe lakini hakuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa upande wa kiwanda cha 21st Century hicho kinafanya kazi vizuri, lakini Mheshimiwa Waziri naomba ukiangalie mazingira yake kusudi kiweze kuzalisha kwa wingi na kitumie mazingira ambayo ni rafiki kwa mazingira, kiache kuharibu mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Mheshimiwa Waziri hivi viwanda viweze kusambaa mijini pamoja na vijijini, hasa mahali pale penye umeme. Naomba ushirikiane na Wizara nyingine kama Wizara inayoshughulika na mambo ya Nishati na Madini pamoja na Wizara ya Maji pamoja na Wizara ya Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kingine ni Kiwanda cha Magunia. Tulikuwa na Kiwanda cha Magunia Morogoro, tulikuwa na viwanda vingi Morogoro, Morogoro ulikuwa ni Mkoa wa viwanda, lakini sasa hivi viwanda vyote kwa wastani havifanyi kazi. Siyo Morogoro tu, tulikuwa na Tanganyika Packers ya Dar es Salaam, tulikuwa tunakula nyama za makopo na samaki za makopo na kila kitu, lakini sasa hivi tuna-import vitu hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kwa Mheshimiwa Waziri ambaye namuamini kuwa atafanya kazi hii, naamini kuwa viwanda vyote, kama alivyosema kwenye hotuba yake, viwanda vyote vilivyokufa atavifufua, naomba kweli vifufuliwe kusudi tuweze kupata ajira kwa vijana wetu, tuweze kupata ajira kwa akina mama, tuweze kupata masoko ya mazao ya kilimo ambayo wakulima wengi wanalima, lakini mpaka sasa hivi hawapati soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vya korosho. Kwa mfano, Kiwanda cha Korosho Kibaha (TANITA), hakifanyi kazi. Najua hakifanyi kazi lakini na wewe Mheshimiwa Waziri unaelewa kwa nini hakifanyi kazi, naomba kifanye kazi ili wananchi wa Mkoa wa Pwani waweze kukitumia kwa kuuza korosho zao kupitia kwenye kiwanda hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wenyewe naomba tuhamasishe wananchi waweze kufungua na kuanzisha viwanda vidogo vidogo hasa huku vijijini mahali ambapo kuna umeme. Tunashukuru sana kwa sababu sasa hivi vijiji angalau vingi vingi vina umeme wa REA…
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa hayo machache ambayo nimechangia. Naunga mkono hoja.