Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nipate kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana, Wizara ya Elimu. Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na vile vile napongeza sana utendaji mzuri wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi zote wanazosimamia, Mheshimiwa Rais anatembea kwenye ahadi zake, lakini nimpongeze Waziri kwa uchapakazi wake, Waziri na wasaidizi wake bila shaka. Mheshimiwa Waziri amekuwa akitusaidia sana, ukimwona anakusaidia shida mara moja, lakini pia ametutembelea, ametembelea Rukwa, ametembelea Wilaya ya Nkasi na Jimbo letu ametembelea na kutokana na ziara yake tumenufaika. Nimeona hapa kwenye hotuba yake kunaanza ujenzi Chuo cha VETA Rukwa, ni jambo jema sana tunampongeza, tunaomba tu kasi ya ujenzi iwe nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kuanza kwa ukarabati wa Chuo cha Wananchi Chala ambacho kipo Jimboni kwangu na nimekuwa nikikisemea sana hapa, tunampongeza na tunashukuru sana. Naomba nishauri hapa, chuo hiki kikarabatiwe, kinapokarabatiwa ukarabati huu uelekezwe kwenye majengo ambayo wananchi waliyatoa maana yake eneo ambalo chuo kipo ni eneo la majengo ya Baba Askofu, Jimbo Katoliki la Sumbawanga na ameonesha nia ya kutumia majengo yale na wananchi walishaamua kujenga majengo mengine eneo la Isoma kwenye shule moja ya sekondari tunayotaka tuianzishe ya Isoma na tumekubali chuo kihamie pale. Kwa hiyo naomba huo ukarabati aliotutengea hapa uelekezwe hapo, atakuwa ametusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kukushukuru kwa kutenga fedha mwaka huu kuanza ukarabati wa majengo ya kuanzisha Chuo cha Ufundi Stadi – Nkasi. Mambo haya yatasaidia sana vijana wetu wanaomaliza darasa la saba na wale ambao wanashindwa kuendelea baada ya kumaliza form four.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeomba pia pesa na umetusaidia, nishukuru Shule ya Sekondari Milundikwa umetupatia zaidi ya shilingi milioni 190 na Shule ya Sekondari ya Nkundi tumepata zaidi ya shilingi milioni 130 na Shule ya Sekondari ya Nduchi tumepata shilingi milioni 91, zote hizi ni za kujenga miundombinu ya sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile shule za msingi tumeweza kupata pesa katika Shule za Msingi Kasu na Chala. Tunaomba waendelee kutusaidia, naomba Shule za Sekondari za Sintali, Kala, Kipande, Kate na Ninde zina hali ngumu sana ya miundombinu ya majengo, madarasa pamoja na maabara. Tunaomba utakapopata nafasi uweze kutusaidia katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuone umuhimu pia wa kusaidia katika maeneo ya Shule za Sekondari za Sintali, Kala na Wampembe. Wizara inahimiza ubora wa elimu lakini katika kuhimiza ubora wa walimu, yapo maeneo katika jimbo langu ya mwambao wa Ziwa Tanganyika miundombinu ya elimu ni mibaya kabisa. Jimbo hili lina tarafa zaidi ya tano lakini Tarafa ya Wampembe miundombinu yake ni migumu sana na ni kandokando ya Ziwa Tanganyika. Kuna vijiji vipatavyo 23, katika vijiji hivi walimu wana hali ngumu sana ya ukosefu wa nyumba, madarasa ya kutosha na usafiri katika eneo lile ni mgumu sana, inafanya hata wakati mwingine wa mitihani vijana kuhama shule moja hadi shule nyingine kwenda kufanya mitihani, kwa hiyo, mazingira kwa ujumla ni magumu sana. Kwa hiyo, walimu wa eneo hili wakati mwingine wanatakiwa kuangalia kwa namna ya pekee maslahi yao. Ni hao ambao wanafuata mishahara yao umbali mrefu sana na hawana namna nyingine ya kuweza kuwasaidia kimaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule chache ambazo tumezianzisha kwa sababu ya wingi wa wanafunzi, Shule za Loleshia, Itanga, Lusembwa, Lupata na Mkiringa. Shule hizi tumezianzisha baada ya kutembelea pale kukuta vijana wengi hawana namna ya kusoma na fedha zilizoanzisha shule hizo ni nguvu za wananchi na Mfuko wa Jimbo peke yake, hatujapata pesa za kutosha. Tunaomba watengewe pesa ili shule hizi ziweze kupata kasi ya kutoa elimu kama shule zingine vinginevyo tutapata shida kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kuhusu walimu. Walimu wetu wa shule za msingi wana shida kubwa mno. Shida kubwa ambayo tunaiona hapa ni maslahi pamoja na upandishwaji wa vyeo vyao. Unakuta mwalimu anakaa katika cheo kimoja muda mrefu sana na wakati mwingine hawapati uhamisho wa hapa na pale ili kubadili mazingira na kufanya kazi vizuri zaidi na kwa kufanya hivyo unakuta kazi zinaanza kufanywa kwa mazoea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba mageuzi katika suala zima la taaluma yaanze pia kwa watendaji wenyewe hawa ambao wako shuleni. Kitengo cha Ukaguzi kiimarishwe hasa katika shule za msingi. Kitengo hiki kimeachwa bila vitendea kazi vya kutosha, hawana magari wala watumishi wa kutosha na kwa maana hiyo shule zote ambazo tunataja hapa hazitembelewi na hivyo huwezi kuona matokeo mazuri katika mitihani kwa sababu shule hizi haziangaliwi mara kwa mara na walimu wake sasa wanafanya kazi kwa mazoea. Kwa hiyo, naomba sana kitengo hiki nacho kiboreshwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni vijana ambao wanasoma elimu maalum maana yake watu wenye ulemavu, albino na watu wengine. Vijana hawa wanapata changamoto nyingi sana katika shule mbalimbali ambazo wanasoma, nyingi hazina miundombinu ya kuwasaidia lakini wanapomaliza hakuna mfumo unaoeleweka wa kuwaajiri vijana hawa japo inatajwa kwenye sera kwamba asilimia kadhaa katika nafasi zinazotolewa wawe wanaajiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kuwe na ufuatiliaji (cross check) kuona katika ajira kadhaa zilizokwishatolewa, je, watu wenye walemavu wamezingatiwa kwa kiwango gani? Kama itakuwa tu ni sera lakini waajiri hawazingatii inakuwa haina maana sana. Naomba kila nafasi za ajira zinapotolewa kiwepo kitengo cha kuhakikisha kwamba watu hawa na wenyewe wanatengewa nafasi zao na tunahakikisha kwamba wamepewa lakini siyo kuacha tu kama sera ilivyo, inakuwa haitusaidii sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nishukuru kwa mchango mzuri ambao umetolewa na wenzangu hasa katika shule za private kwamba shule hizi zina msaada mkubwa sana na kama kuna haja ya kutoa namna yoyote ya usaidizi hasa katika maeneo ambayo wameona kwamba ni changamoto waweze kufanya hivyo kwa sababu ni washika dau kama wengine, wanatoa elimu kama watu wengine. Kwa hiyo, ni wadau muhimu katika utoaji wa elimu katika nchi, isionekane kama ni wafanyabiashara tu peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naona kama ni watu ambao wanasaidia kubeba mzigo mkubwa huo wa utoaji elimu katika nchi na kwa hivyo ni wadau muhimu sana na hii ndiyo inaweza ikatusaidia kwenda kwa pamoja. Kwa sababu tunasema PPP ni muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu bila kuimarisha sekta binafsi tukaiachia Serikali peke yake sidhani kama tutaweza kufikisha malengo ya Kitaifa yanayotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)