Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana, kwa kunipa nafasi na niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu ya Wizara ya Elimu. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii leo pia naunga mkono asilimia mia hotuba ya Kambi ya Upinzani yote ambayo yamo mule, ninaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika masuala matatu nikianzia na suala la kwanza, la kupungua kwa bajeti ya Wizara hii ya Elimu. Awamu ya Nne ya Serikali yetu ilikuwa ikienda kila mwaka ikipandisha bajeti ya Elimu, lakini toka tumeingia Awamu hii ya Tano, tunaona kuna mserereko wa kupungua kwa bajeti ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukianzia mwaka 2016/2017 na chanzo cha takwimu hizi ni haki elimu, wanasema toka mwaka 2016/2017 imepungua bajeti kutoka trilioni 4.770 hadi kufikia trilioni 4.706 kwa mwaka 2017/2018. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona pia kwa mwaka 2018/2019 pia imepungua mpaka kufikia trilioni 4.628. Pamoja na hayo, tukiangalia uwiano mkubwa wa bajeti ya Serikali pia, tunaona kwamba imepungua kutoka asilimia 16.1 mwaka 2016/2017 mpaka 2018/2019 asilimia 14. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inapingana kabisa na azimio ambalo tumeridhia sisi la nchi za kusini mwa jangwa la sahara kwamba tufikie asilimia 20. Sasa tunavyopunguza bajeti ya Wizara ya Elimu, athari zake ni kubwa mno, mnaona Waheshimiwa Wabunge karibu wengi wanazungumza hapa wakilalamika jinsi ambavyo Wizara hii imekuwa haipati fedha kwa ajili ya kutatua changamoto zilizoko huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu iliyoko katika shule zetu, vyuo vyetu, ina mashaka makubwa mwaka huu kumekuwa na ongezeko la asilimia 17 ya wanafunzi wanaoingia shule za msingi, tofauti na miundombinu ambayo tunakwenda kwa asilimia moja. Sasa ukiona, miundombinu vis-a-vis hao wanaoingia mashuleni unakuta kwamba kuna wanafunzi wameingia kidato cha kwanza mwezi wa tatu, kuna wengine wameingia mwezi wa nne. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalalamika nini hapa kwamba hawa watoto wanatoka hawajui kusoma na kuandika wakati wameingia mwezi wa tatu mwezi wa nne na mtaala unataka waanze mwezi Januari.

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti,

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Nimekataa taarifa kwa sababu hazinisaidii sana, kwa muda wangu.

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Yah (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumpa taarifa kwamba.

MWENYEKITI: Hapana nimekataa. (Kicheko)

Endelea!

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hii tunavyozungumzia ni changamoto kubwa ambayo ipo katika jamii yetu, kwa Wizara hii kupunguza hiyo bajeti ya Wizara ya Elimu. Kuna upungufu wa vifaa maabara nyingi ambazo wananchi wamejenga, na Serikali haijamalizia kuna upungufu wa kemikali zinazotakiwa kwenye maabara zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunapunguza bajeti ya Wizara ya Elimu, tuna uhaba pia wa vifaa vya ufundishaji, na kufundishia, unakuta kwamba kuna walimu wengi wanalalamika kuna somo linaitwa stadi za kazi, mwalimu amepewa kitabu chake cha kiongozi, anaambiwa chukua msumeno na ubao onyesha wanafunzi waanze kukata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mwalimu ambaye mshahara hamumuongezi? Huyu mwalimu ambaye madaraja yake hayapandi, hana pesa, lakini anatakiwa awe na vifaa darasani, wanafunzi wamezuiwa wasichukue vifaa majumbani wanasema tumesema elimu bure. Sasa mwalimu anafundishaje huyu? Hivi vifaa vinatakiwa kwa ajili ya mwanafunzi kupata ujuzi wa vitendo katika kazi zake. Zamani sisi tunavyosoma tulikuwa tunaambiwa katika masomo ya sayansi kimu mwingine aje na mafuta, mwingine aje na mchele, mwingine aje na sijui na chumvi, mwingine aje na kile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanafunzi mnakaa darasani mwalimu anawafundisha kupika, mnapika, sasa hivi walimu wanashindwa kufanya hivyo? Capitation grands ambazo tulitaka zienda mashuleni zile 10,000 kwa shule za msingi na 25,000 kwa shule za sekondari kwanza haziendi, pili ziko chini hazitoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwanza napendekeza Mheshimiwa Waziri, hizo capitation grands ziende mashuleni kama zinavyohitajika kuna shule nyingi sana, ambazo hawapati, na hawapati wengine kwa wakati, lakini pia ni ndogo kama tulivyosema kwa dola, sasa dola inapanda, na sisi tumebakia na kiasi kile kile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ipandishwe kwa primary school iwe angalau shilingi 20,000/= na kwa shule za sekondari iwe shilingi 50,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende katika suala la utekelezaji wenye mashaka sana wa bajeti katika fedha zetu za maendeleo kwa Wizara hii ya Elimu. Unakuta katika bajeti ya elimu, fedha za maendeleo zilizotengwa karibia nusu, shilingi bilioni 857 zilizotengwa katika maendeleo, shilingi bilioni 427 ndizo zinakwenda katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Hizi fedha ni nyingi, zinakwenda kule lakini tunakuta Wizara hii inabakia na pesa kidogo ambayo ndiyo tunasema Wizara imepata pesa nyingi. Hii Wizara haipati pesa nyingi kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Waziri wa Fedha awaongezee fedha Wizara ya Elimu kwa sababu kile kiasi kinachobaki ni kidogo. Miradi ya maendeleo karibu 40 haijapata fedha. Nikianzia huu mradi huu wa Kitengo cha Kudhibiti Ubora. Mwaka 2017/2018 walitengewa shilingi bilioni moja mwaka 2018/2019 walitegewa shilingi bilioni 1.5 lakini miaka yote hii hawakupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge mnajua, hiki ni kitengo muhimu sana ambacho kinakagua jinsi ambavyo wanafunzi wetu au vijana wetu na walimu wetu wanatakiwa wafanye kazi, lakini hawatengewi fedha za kutosha; na tunajinasibu kwamba tunakusanya fedha nyingi, lakini fedha hazijaenda, hawa hawafanyi kazi ya ukaguzi, hawa watu wetu wa udhibiti ubora hawakagui shule zetu, lakini shule binafsi wanatoa pesa wenyewe kwa hawa Wadhibiti Ubora ndiyo maana wanaenda kukaguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona katika shule kumi bora huwa zinaongoza shule binafsi na shule za Serikali hazipo. Sasa mimi nasema hivi, if you fail to plan, you plan to fail. Wekezeni vya kutosha katika elimu. Namwomba Mheshimiwa Waziri, tuwekeze vya kutosha katika elimu, tuweke foundation ya kutosha katika msingi, twende sekondari ndio tutapata watu wazuri katika vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko vyuo vikuu tunakuta Wahadhiri wanalalamika kwa sababu hatujawekeza vizuri katika sekta hizi chini. Utaona tunazungumzia hapa, lakini tukisema elimu imeshuka Waziri haangalii Waziri wa TAMISEMI, unaangaliwa Waziri wa Elimu. Kwa hiyo, nawaomba mkae pamoja muone jinsi ambavyo mnaweza mkaboresha msingi ili huku juu tuwe na ubora unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja klatika suala la Taasisi ya Elimu Tanzania. Tunalalamika kuhusu vitabu hapa, lakini Taasisi ya Elimu Tanzania ilitengewa shilingi bilioni 40. Katika shilingi bilioni 40 miaka miwili mfululizo hawakupata fedha, wamepata mwaka huu shilingi bilioni nne ambayo ni asilimia 10. Sasa asilimia 10 tunalalamika lakini asilimia 10 Mheshimiwa Waziri mnaowapelekea inatosha kufanya kazi zote hizo za kuandaa vitabu, kiongozi cha mwalimu na kufanya kazi zote ambazo zinatakiwa pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iangalie Taasisi ya Elimu, kama wana shida ya kufanya elimu hii iwe bora. Taasisi ya Elimu iboreshwe lakini naomba mshirikiane na sekta binafsi PPP iliā€¦

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)