Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu na nikushukuru wewe kwa kuniwezesha kusimama na kuweza kutoa mchango wangu katika sekta hii muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuunga mkono hoja hii iliyo mbele yetu. Naiunga mkono kwa sababu Wizara ya hii ya Elimu ukilinganisha na tulipotoka kazi kubwa na nzuri inafanyika katika sekta hii. Naomba kabisa nimpongeze Waziri Mheshimiwa Prof. Ndalichako; Naibu Waziri, Mheshimiwa Olenasha; Katibu Mkuu na watendaji wake na timu nzima ya Wizara ya Elimu kwa kazi njema na kubwa mnayoifanya ya kuhakikisha sekta ya elimu sasa inaleta tija kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Mheshimiwa Prof. Ndalichako Mungu akubariki sana, ni mama usiyejikweza, unafanya makubwa ukisaidiana na wenzako. Leo wakati unawasilisha ulikuwa unatuonyesha kwenye picha, kwa kweli umetushangaza, tumeona maghorofa yanavyojengwa mikoani mpaka Nyasa na maeneo mengine. Wote huo ni ubunifu wako pamoja na watendaji wenzako, mimi na wenzangu tunakuunga mkono. Niungane na Mheshimiwa Rais alipokuwa kule Mtwara alitamka bayana kwamba anafurahishwa na kazi yenu, chapeni kazi na muendelee kusonga mbele, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba asitokee mtu yeyote kuwakatisha tamaa kwa sababu Waswahili wanasema vizuri vyajiuza na vibaya vyajitembeza. Maana watu wamezoea akifanya kidogo kashatoka kwenye media siyo Mheshimiwa Prof. Ndalichako na wenzake, wanafanya vitu vikubwa vinajitangaza vyenyewe. Hongereni sana, endeleeni kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na maoni ya Kamati yangu ya Huduma za Jamii. Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa hapa Serikali inafanya kazi nzuri sana ya kupeleka fedha katika sekta hii. Unaona fedha ya miradi ya maendeleo karibu asilimia sitini na kitu imekwenda, OC zaidi ya 37%, mishahara ni karibu 100%. Hata hivyo, naomba niungane na maoni ya Kamati kusema kwamba fedha inayopelekwa hailingani na kazi ya sekta hii. Naomba niishauri Serikali na Waziri wa Fedha kama yupo anisikilize, sekta hii naomba ipelekewe fedha 100% kama iliyopangwa ili miradi ya maendeleo itekelezwe na fedha za OC siweze kufanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanya ziara sisi kama wana Kamati, tumetembelea chuo cha DUCE tumeona kazi nzuri sana iliyofanywa na Serikali, fedha zaidi ya shilingi milioni 500 zimekwenda. Ukiangalia kuanzia taarifa ya Waziri na ya Kamati fedha zilizotengwa hazikwenda zote matokeo yake mradi hakuna kinachoendelea. Tumekwenda Chuo cha Mwalimu Nyerere pale Kigamboni, kuna fedha iliyotengwa kwa ajili ya mradi mpaka tunakwenda kukagua hakuna fedha iliyokuwa imekwenda. Naomba sana na bahati nzuri Waziri wakati tunaongea nawe kwenye Kamati ulituhakikishia kwamba kwa sababu bado miezi inaendelea itatafutwa fedha na kupelekwa, naomba nami nisisitize hilo kwa sababu hii ni fedha ambayo tulitenga kwenye bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ya OC ndiyo inakwenda kulipa Wahadhiri wetu. Kwa mujibu wa taarifa iliyowasilishwa na tulizozipata tena kupitia kwa Wenyeviti wa Bodi, Wahadhiri wetu wana madai yao ya kodi ya nyumba. Mhadhiri ni kiongozi, ni mtumishi, ameaminiwa, anafanya kazi kubwa lakini hana uhakika wa kuishi. Naiomba Serikali yangu Tukufu na sikivu hebu pelekeni hizi fedha za OC ziende kulipa madeni ikiwepo na fedha za watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nitoe ushauri, kazi nzuri tuliyoiona pale Mwalimu Nyerere na DUCE kupitia vyanzo vya ndani wameweza kujenga miundombinu. Naomba nitoe ushauri, vyuo vingine na kama ambavyo Kamati tumesema igeni mfano wa vyuo hivi, kwa sababu vyanzo vya mapato vya ndani vipo lakini wakati mwingine havitumiki vizuri wote tunasubiri Serikali Kuu. Naomba tuwaige hawe DUCE na Mwalimu Nyerere ili na vyuo vingine viweze kutengeneza miundombinu kwa kutumia vyanzo vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nivishauri vyuo vyote nchini vikiwepo vyuo vikuu na vyuo vya ufundi kubuni vyanzo vingine vya mapato. Sisi kwenye Kamati tuliona kuna uwezekano wa kubuni ambavyo vitafanya vyuo vijiendeshe bila kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye Chuo cha Julius Kambarage Nyerere cha Sayansi ya Kilimo ambacho kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambaye na mimi ni mdau niliyeshiriki kuiandika na kutafuta maoni ya wananchi, tulipofika Mkoa wa Mara na kwa Watanzania walituambia wanataka mawazo ya Mwalimu yatimie. Mwalimu Nyerere na wenzake walitoa eneo bure kwa Serikali, walijinyima wakatoa zaidi ya heka karibu 450 kwa ajili ya kujenga chuo. Mwalimu Nyerere akajenga miundombinu ikiwemo Bwawa la Kialando, bwawa la mfano ili kesho na kesho kutwa kijengwe chuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chuo hiki kiliwekwa kwenye Ilani, ukurasa wa 101, Ibara ya 52, kifungu cha K, kifungu cha pili kidogo kinaeleza bayana kwamba, endapo CCM itachaguliwa 2015 – 2020, Chuo cha Mwalimu Nyerere Butiama kitajengwa. Nimefurahishwa na kazi inayoendelea kwa ajili ya ujenzi wa chuo hiki. Tumeona mipango kwa ajili ya kutafuta hati miliki.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Okay.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nilitaka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba kwenye ukurasa katika Chuo kilichozungumzwa hapa cha Mwalimu Nyerere kinachozungumzwa pale ni kwamba Chuo kijiandae kufundisha wajasiriamali kiangalie watu wanaokamua na kuangalia kuku, sio kufundisha wanafunzi waliokuwepo hapa. Kwa hiyo, mambo mengine yaliyoandikwa humu ni kwamba nataka kumpa taarifa kwamba aendelee kuona kwamba hiki Chuo ni muhimu sana na wanaohusika wakione kama Chuo cha Mwalimu Nyerere sio kwenda kufundisha kuku. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, taarifa naipokea kwa sababu Mbunge Getere ni Mbunge mwenzangu wa Mkoa wa Mara, na hivi karibuni tulikuwa kwenye kikao cha RCC. Moja ya agenda zetu ilikuwa pia ni kuzungumzia Chuo cha Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza kwa haya yaliyofanyika, nimeona mmehangaika kutafuta hatimiliki, sasa tunataka tujue hivi mmeishia wapi, kwa sababu, suala la upatikanaji wa hatimiliki hata kwa mtu wa kawaida. Siku hizi kwa sababu Serikali ya CCM imerahisisha miundombinu, na tumeletewa Ofisi iko katika Kanda ambayo Ofisi yetu iko Simiyu wiki mbili unapata hati. Inakuwaje leo Chuo cha Mwalimu mpaka leo hati haijapatikana, changamoto ni nini? Tunapongeza mambo yanayofanyika kuna maandiko yameandikwa, kuna mafunzo yanaendelea pale kwa ajili ya kuanzisha hiki Chuo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijue Mheshimiwa Prof. Ndalichako mama ninaye kuamini, na mama ninaye kupenda, na kwenye Kamati pia nilikuuliza kwenye Randama yako nimeona umetenga bilioni moja, nilitaka nijue ni za nini?. Nataka kujua hizi fedha kwa ajili ya kujenga Chuo, na hasa kwa kuzingatia kwamba tunaelekea mwaka 2020 mwisho wa Ilani hii ya CCM ambayo tuliiahidi kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo hiki, ziko wapi? Na ningependa kujua chuo kinaanza lini? Kwa sababu Serikali imeshawekeza, Mbunge wetu mpendwa, Mzee wetu, Mzee Mkono na Mungu ampe Wepesi apone, arudi Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amejitahidi kujenga majengo na akayatoa bure kwa Serikali ilikuwa ni shule ya High School tukawaondoa watoto, majengo yapo na pa kuanzia palikuwepo kuna Chuo cha Kisangwa ambacho tulisema itakuwa ni sehemu ya Chuo Kikuu kile. Kuna maeneo ya Chuo cha Bweri, maeneo ya kule Rorya, tulisema yote yatakuwa ni sehemu ya Chuo, wakati tukijiandaa kujenga miundombinu. Ningependa kujua hivi Mheshimiwa Waziri, Mkakati ni nini kutekeleza ndoto za Mwalimu alizozitoa akiwa hai, na kama kweli tuna lengo la kumuenzi Baba wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua Mheshimiwa Waziri na timu yako, hivi ninyi mnaonaje, mmeshaajiri wafanyakazi tena wenye weledi, yuko Profesa pale Mkuu wa Chuo, mpaka amestaafu yule anayekaimu sasa ndiyo amekuwa Mkuu wa Chuo. Analipwa mshahara pamoja na watendaji wenzake zaidi ya kumi na nne, leo hakuna kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri, hebu utakaposimama hapa, Watiama, narudia tena Watiama, akiwemo Baba wa Taifa aliyetangulia mbele ya haki. Ninapozungumza Watiama naongelea Wazanaki wa Butiama, walio kuwa na dhamira hiyo ya kujenga Chuo, wanataka leo wakusikie kauli yako, Chuo kitajengwa na Chuo kitafunguliwa na lini, ndiyo walichotuma leo nilete hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie ujenzi wa miundombinu ya shule ninapongeza sana Serikali yangu Tukufu ya Chama cha Mapinduzi, imefanya kazi nzuri ya kujenga miundombinu ikiwemo Vyuo vikuu na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kama mama…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo Mheshimiwa Waziri kwenye suala la miundombinu na hasa katika mabweni katika Vyuo Vikuu watoto wetu wa kike wanakaa katika maisha…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa,

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanapanga kwenye majumba matokeo yake wanakuwa ni wake wanaolewa na watu.

MWENYEKITI: Muda wangu sio rafiki.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wanakosa kodi za kulipa wanatembea masafa marefu…

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na hata Vyuo vya Dar es Salaam kwenda kutafuta hiyo huduma. (Makofi)

MWENYEKITI: Muda wangu sio rafiki.

MBUNGE FULANI: Naam…

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri Ndalichako utakapokuja hapa..

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba alikuwa anatoa taarifa huku.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mmejipangaje, kujenga miundombinu kwa ajili ya hosteli ya wasichana, Chuo cha DUCE, Chuo cha Mwalimu Nyerere, Chuo cha Ardhi na Vyuo vyote nchini tumejiandaaje ili kuwanusuru watoto wetu wa kike ambao wanaingia kwenye dhahama ya kulipa kodi kiwango ambacho ni kigumu, na sio kwa watoto wa kike peke yake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Makilagi.

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naongelea na VETA, kuna VETA hapa zinajengwa nchini naomba na Kisangwa iliyoko Mkoa wa Mara hebu ipe kipaumbele kwa sababu majengo pia yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, naunga mkono hoja. (Makofi)